15 July 2011

Manispaa yazindua mradi wa kutokomeza malaria

Na Heri Shaaban

MANISPAA ya Ilala inatarajia kuzindua mradi wa kupambana  na maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa wakazi wa Kata ya Tabata Wilaya ya Ilala Mkoa wa Ilala.Hayo
yalisemwa na Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dkt. Aisha Mahita, wakati wa maadhimisho ya siku ya afya manispaa hiyo iliyoadhimishwa Dar es Salaam juzi. Maadhimisho jayo yalienda sambamba na uzinduzi wa Kituo cha Afya Tabata Kisiwani.

Dkt. Mahita alisema kuwa kampeni hiyo ya mradi wa kudhibiti malaria itakapoanza katika kata hiyo itatolewa elimu kwa kushirikisha jamii na wajumbe wa kamati ya mazingira.

"Mradi wa udhibiti wa malaria unatarajia kuanza hivi karibuni hivyo nawaomba wananchi kushirikiana na idara ya afya pamoja na halmashauri katika kufanikisha malengo haya kwa kutumia kikamilifu huduma zilizopo ili tuweze kufanikiwa,"alisema Dkt.Mahita.

Alisema kuwa kituo hicho kinatoa huduma zote za mama na mtoto (MCH) pamoja na ushauri wa magonjwa mbalimbali, hivyo amewataka wazazi kuwapeleka watoto wao kupima katika kituo hicho.

Aliongeza kuwa kuanzia leo yaani (juzi) kituo hicho kitatoa matibabu kwa kupima bure magonjwa mbalimbali, hivyo alitoa mwito kwa wakazi wa Tabata Kisiwani na maeneo ya jirani kupima afya zao karibu na maeneo wanayoishi.

Pia aliwaagiza wanawake wajawazito wawe wanawahi mapema katika vituo vya afya au hospitalini ili kuepuka madhara yanayojitokeza au kuepuka  kujifungulia kwenye  teksi au mapokezi. Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa lawama.

Naye Meya wa Manispaa ya Ilala, Bw.Jerry Silaa, aliagiza wanaume wawe na tabia ya kwenda katika vituo vya afya na wake zao ili kujua afya zao mapema na si kuwaachia wao peke yao.

Bw.Jerry alisema kuwa mwanaume unapoteua siku moja kumsindikiza mkeo katika kituo cha afya ni vizuri kwa kuwa unajua maendeleo ya mke kipindi anapobeba ujauzito.

No comments:

Post a Comment