22 July 2011

Chaka Khan kupagawisha hafla ya Club E kesho

Na Mwandishi wetu

MWANAMUZIKI nyota kutoka Marekani, ambaye pia ni gwiji wa miondoko ya soul, Chaka Khan, ameahidi kutoa burudani nzuri katika hafla ya Club E itakayofanyika
kwenye Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, kesho.

Chaka Khan, ambaye aliwahi kupata tuzo ya BET Lifetime Achievement mwaka 2006, jana wakati wa ziara yake katika Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), alisema amejiandaa vizuri kuhakikisha anazikonga nyoyo za mashabiki wa klabu hiyo.

Msanii huyo alipiga picha za pamoja na wafanyakazi  wa kampuni hiyo na baadaye kupewa maelezo kuhusu shughuli mbalimbali za kampuni hiyo.

Katika mahojiano yake na waandishi wa habari, Chaka Khan alisema analeta Tanzania ujumbe wa amani, upendo na uponyaji.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 58, aliwasili nchini Jumatatu mchana.

Baadhi ya nyimbo za Chaka Khan zilizovuma zaidi miaka ya nyuma  ni Tell Me Something Good, Sweet Thing, Ain't Nobody, I'm Every Woman, I Feel for You na Through the Fire.

Club E huandaa shughuli mbalimbali za burudani kila mwaka kwa wanachama wake kama mojawapo ya njia ya kuwakutanisha, kuburudika na kuwashukuru.

No comments:

Post a Comment