22 July 2011

Aisha Madinda aanza kwa kishindo Extra Bongo

Na Addolph Bruno

MNENGUAJI mpya wa bendi ya Extra Bongo, Aisha Mohamed 'Aisha Madinda', juzi alionesha umahiri wake jukwaani wakati wa onesho la bendi hiyo lililofanyika
kwenye ukumbi wa Club Masai, Ilala jijini Dar es Salaam.

Aisha aliyeihama African Stars 'Twamga Pepeta; na kutua Extra Bongo, alizikonga nyoyo za mashabiki waliohudhuria onesho hilo, ikiwa ni mara yake ya kwanza kupanda jukwaani akiwa na bendi hiyo.

Mnenguaji huyo alionekana kuwavutia mashabiki alipokuwa akicheza sambamba na wenzake, akiwemo mnenguaji mwingine aliyetokea Twanga Pepeta, Otilia Boniface.

Aisha alionekana kumudu vyema mitindo ya bendi hiyo ya kujinafasi, kizigo na kujishebedua, wakiongozwa na Hassan Mussa 'Super Nyamwela'.

Mara baada ya kumalizika kwa onesho hilo, Aisha alisema kuwa, mashabiki wa bendi hiyo watarajie kupata mambo mengi mazuri kutoka kwake.

"Nawashukuru mashabiki kwa kunipokea vizuri Extra Bongo, tarajieni mambo makubwa katika maonesho yetu," alisema Aisha.

Mbali ya Aisha, kivutio kingine alikuwa mwimbaji Ramadhani Masanja 'Banza Stone',  aliyepanda jukwaani na kuimba wimbo aliotunga wa Watu na Falsafa ya Maisha.

No comments:

Post a Comment