30 May 2011

Heche aibuka kidedea BAVICHA

*Aahidi CHADEMA kuchukua dola 2015
*Rushwa, kujuana vyatawala uchaguzi


Na Edmund Mihale

HATIMAYE uchaguzi wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) ulimazika jana kwa kumpata Bw. John Heche kuwa
Mwenyekiti wa umoja huo.

Pamoja na kupatika kwa kiongozi huyo, uchaguzi huo uligubikwa na mizengwe mbalimbali ikiwemo rushwa na mambo ya 'kujuana' yaliyooneshwa wazi na viongozi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa uchuguzi uliofanywa na Majira juzi usiku, uchaguzi huo ulifanyika huku kukiwa na makundi matatu, makundi hayo ni yale yanayomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Zitto Kabwe na lile lisilomuunga mkono  mtu yeyote katika chama hicho.

Uchunguzi huo ulibaini kuwa kundi linalomuunga mkono, Bw. Mbowe ndilo lilokuwa na nguvu zaidi na ndilo lilochukua kiti hicho kutokana na mwanzilishi wa chama hicho, Bw. Edwin Mtei kuliunga mkono kwa asilimia mia.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Baraza la Wazee kilidokeza kuwa, maamuzi ya kufanya uchunguzi wa wagombea yalifikiwa baada ya kugopa kivuli cha Bw. Zitto ambaye ameonekana kuungwa mkono na vijana wengi ndani ya chama hicho.


Kilisema kuwa baada ya kubaini uwezekano wa kundi hilo kushinda, baraza la wazee lilikubaliana kutafuta mambo yatakayowamaliza wagombea hao ili wasipitishwe katika kugombea kiti hicho.

"Ndugu yangu napenda kusema kuwa chama hiki sasa kinaenda pabaya walitafuta kila njia ya kuwamaliza vijana na njia waliyoipata ni kuwatutafutia tuhuma zitakazowafanya waondoke katika kuwania nafasi hiyo...lakini tulipigana na ikashindikana," alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

Alieleza kuwa tuhuma hizo ni kundi hilo kutaka kuunganisha nguvu katika uchaguzi huo ili kumpigia kura mtu moja jambo ambalo kamati ya wazee ilipingana na suala hilo ikidai kuwa ni jambo linalowagawa vijana ndani ya chama.

Chanzo hicho kilisema kuwa katika uchaguzi wowote makundi lazima yawepo ndo maana mgombea hawezi kupata kura kwa asilimia mia moja hata akiwa pekee yake.


Alisema tuhuma nyingine zilizofanya kuenguliwa kwa wagombea hao ni  kupokea wajumbe kutoka Zanzibar  jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote lakini kutokana na mizengwe iliyoandaliwa na kamati hiyo ilibidi watu hao waadhibiwe.


Alisema kuwa tuhuma nyingine ilikuwa ni kupiga kampeni kabla ya muda uliopangwa na tume hiyo hali iliyosababisha kuenguliwa dakika za mwisho katika uchaguzi huo.


"Tuhuma nyingine iliyoelezwa ni wagombea hao kutaka kupindua chama hicho kwa kuhamisha agenda za chama hicho na wengine walihofiwa kuwa ni usalama wa taifa," kilisema chanzo chetu.

Hata  hivyo Mjumbe huyo wa baraza la wazee alisema kwa upande wa Bw. Heche nako kulikuwa na tuhuma za  kupokea wajumbe ambao kamati haikutaja kuwa wanatoka katika mkoa upi lakini alijitetea kuwa ni ndugu zake.    

"CHADEMA tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anapokosea tunataka awajibishwe, sisi leo mtu anakosea wakati wa mchakato wa uchaguzi lakini tunasema tunafanya uchunguzi je akipata madaraka tunamchukulia hatua gani kwani atakuwa tayari amepata madaraka," kilisema chanzo.

Chanzo hicho kiliendelea kuhoji ni kwa nini mgombea huyo aachwe na kuchukua madaraka huku akiwa na tuhuma hivyo akataka haki itendeke kwa wote.

Naye Tumaini Makene anaripoti kuwa;

Kamati ndogo maalum, kwa ajili ya uchunguzi wa uchaguzi huo iliyoundwa na kamati kuu ya chama hicho ilibaini kuwepo kwa vitendo vichafu ikiwemo baadhi ya wagombea kutaka kuundwa makundi ili kudanganya wapiga kura  kwa nia ya kutaka ashinde mtu wanayemtaka kwa hila zao.

Akizungumza na majira jana akiwa katika uchovu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, pamoja na kutotaka kuzungumzia tuhuma hizo za rushwa kwa undani akisema "mengine yanahitaji maamuzi ya juu", alisema kuwa wagombea hao watatu walioenguliwa baada ya kuthibitisha kuwa wamekwenda kinyume na katiba na kanuni za chama, kifungu cha 10, wamekiri pia kuwa wao walijihusisha kutengeneza agenda ya BAVICHA.

"Sasa hilo ni suala kubwa agenda ya BAVICHA ni suala la mkutano na haliwezi kuwa la wao watatu lakini walibainika kujihusisha na kundi la Bw. Habib Machange ambapo ilibidi chama kiingie gharama ikiwemo wajumbe wa kamati hizo kufanya kazi tangu saa saba usiku wa juzi mpaka asubuhi jana na baadhi ya wajumbe walishindwa kurejea kwao," alisema Dkt. Slaa.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Majira ilibainika kuwa mmoja wa wabunge wa chama hicho alijihusisha na kusimamia vikao vya usiku wa manane vilivyokuwa vikitumika kuwalubuni wajumbe kugawa fedha, kuwanunulia pombe usiku wa kuamkia uchaguzi akitaka kuweka mtandao unaodaiwa kuwa na lengo la kusambaratisha chama hicho.

Mbunge huyo machachari kutoka Kanda ya ziwa ametajwa pia kutoa udhamini wa mmoja wa mgombea aliyeenguliwa kwa lengo hilo ambapo imeelezwa kuwa suala lake pamoja na vituko vingine vitafikishwa mbele ya Kamati Kuu kwa maamuzi zaidi.

Alipoulizwa juu ya tuhuma kwa mbunge huyo (jina tunalo), Dkt. Slaa hakuwa tayari kulizungumzia na kusema kuwa liko ngazi ya juu ya kamati kuu.

Wakati hayo yakiendelea Bw. Heche alisema yuko tayari kufanya kazi katika nafasi hiyo akishirikiana na wenzake ili BAVICHA iwe sauti ya kupigania maslahi ya wananchi wanyonge.

Akizungumza na majira jana, Bw. Heche alisema kuwa BAVICHA itasimama kwa maslahi ya nchi na chama hicho kwa jitihada za kuchukua dola kwa ridhaa ya wananchi.

Bw. Heche alipata kura 147 sawa na asimilia 56 ya kura zote zilizopigwa 267 ambapo kura tatu ziliharibika.

Walioenguliwa katika uchaguzi huo ni Greyson Nyakarungu, Mwampamba na Bernard Saanane.

7 comments:

  1. hakuna kitu hapo.hebu angalia hii undugu,kujuana, Rushwa na Viongozi kupanga Safu yao. Hawa wa Mbowe, hawa wa Zito. Waliobaki lazima walikuwa wa Slaa. angalia pia hili CHADEMA kila siku kelele kuhusu Rushwa, hivi kweli Mtu kama Mbowe ataacha hiyo? kama kwenye kampuni zake halipi kodi na kwenye Chama anawachakachua kwa kuwauzia Magari Chakavu itakuwa kwenye Uchaguzi wa Vijana? hakuna Demokrasia ndani ya Chadema ni Uhuni tu na Undugu uliojaa huko. Watanzania hatuwezi kufanya kosa kuwaweka Madarakani Chama kama hiki. Mbona Visiwani hamtii Mguu huko? inaeleweka Wazanzibar hawataki ubabaishaji walishawakataa Mapeema kabisa. hiyo pia inawanyima sifa ya kutawala. haya ni Machache tu, Siri na Mambo wanayoyafanya tunayo na tunayajua. 2015 kiboko ni kama 2010.

    ReplyDelete
  2. Ndugu zangu tusidanganyike, Tanzania kwa sasa hakuna Chama cha wala viongozi wapenda watu. Karume, Nyerere na Sokoine wameondoka na upendo wa nchi tmebakiwa na ukoko wa ubwab wa wa juzi tupu.

    Hehehe,Jamani ee! mliokataliwa rudini kwenye chama changu, kinaitwa TANU-ZNP mpya.
    Najua mtaenda CCM na mkikataliwa huko mtajiunga na Tadea na nk nk nk, all is pumba +fu!

    ReplyDelete
  3. This can only catch a fool! Fortunately they are many out there!

    ReplyDelete
  4. Viongozi wa siasa ni walewale na mbinu ni zile zile chafu. Anayekamatwa ndo anakuwa mbaya. Tusidanganyike na tusidanganywe na wana siasa. Wote wana uchu wa madaraka, na hayo madaraka wanayapata kwa kutudanganya sie wananchi. Haya, kwanini uniambie niandamane kama hata wewe mambo yako ni yale yale?

    ReplyDelete
  5. Chadema nawasifu sana kwa kulishugulikia swala la rushwa as soon as lilivyojitokeza hapo mmeonyesha kuwa mnachukukia rushwa. mambo ya kusema kujuana na kupendeleana alikuwepo kwa maana wapiga kura walikuwa wengi na ni kutoka mikoa mbalimbali kwahiyo kusema fulani alipewa kwa kupendelewa halina ukweli. kwa ujumla kama msomaji unavyoona habari hii imejaa vyanzo vilivyofichwa(havipo) kwa maana ni vya kutunga.

    ReplyDelete
  6. Ni nani wa kuikomboa nchi yetu na haya makundi. Kila sehemu matabaka matabaka tu, nyie wanasiasa wanafiki na walafi wa mali na madalaka mwatupeleka wapi, machinjioni au jahanamu? Watanzania tuna kazi kubwa sana, Nyerere alipigania ujinga lakini sasa umerudi tena unaongezeka na kutisha kama malaria na UKIMWI, uwiiiiiiiii!

    ReplyDelete
  7. mUNGU IBARIKI chadema!!!

    ReplyDelete