05 April 2011

Simba yamkosha kocha TP Mazembe

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa timu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Lamine Ndiaye ameisifia Simba kutokana na kiwango cha juu
walichokionesha licha ya kuifunga mabao 3-2.

Timu hizo zilikutana juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo uliokuwa wa vuta nikuvute wa kuwania kufuzu kucheza mtoani wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Ndiaye alisema mchezo ulikuwa mgumu kwani Simba ilidhamiria kushinda mchezo huo na ndiyo maana muda wote walicheza kwa nguvu.

"Simba imecheza vizuri, ilivyocheza leo (juzi) ni sawa na ilivyocheza ilivyokuwa ugenini (Lubumbashi), ila tatizo hawakuwa makini katika kuzuia mashambulizi," alisema Ndiaye.

Alisema kabla ya mchezo wachezaji wake waliapa kuifunga Simba katika hali yoyote na ndiyo maana walipoona kila bao wanalofunga linarudishwa, ikabidi waongeze juhudi zaidi.

Akizungumzia timu yake, alisema ilicheza vizuri licha ya kwamba si katika kiwango alichotarajia kwani mabeki hawakuwa makini kwa kuruhusu mabao mawili yaingie.

Alisema timu yake hiyo inayotetea ubingwa huo, inaundwa na wachezaji 12 kutoka nchini humo, saba kutoka Zambia na mmoja kutoka Nijeria, hivyo mchanganyiko huifanya timu yake kuwa nzuri zaidi.

TP Mazembe imefuzu hatua ya mtoani kwa jumla ya mabao 6-3 ambapo katika mchezo wa awali uliopigwa Lubumbashi nchini Congo, wiki mbili zilizopita iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

3 comments:

  1. timu za Tanzania zinashiriki tu

    ReplyDelete
  2. hizi sifa sababu wameshinda ingalikuwa wamefungwa wasingesifia wangeelezea mchezo tu

    ReplyDelete