15 April 2011

Mzimu wa Meremeta wamsumbua Pinda

Na Edmund Mihale, Dodoma

MZIMU wa Kampuni ya Meremeta uliibuka tena bungeni Dodoma jana, baada ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika kumtaka Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda
kuwataja wahusika wa kampuni hiyo lakini akaambulia patupu.

Wahuska katika kampuni hiyo ambao hawajawahi kutajwa hadharani wanatuhumiwa kuchota  Dola za Marekani 118,396,460.36 fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hayo yaliibuka katika kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu, ambapo Bw. Mnyika alimuuliza Bw. Pinda kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimtangaza kujivua magamba ilikujisafisha na ufisadi hivyo kumtaka kuwataja wahusika wa Kampuni hiyo.

"Mheshimiwa Mkuu uliwahi kulieleza  Bunge hili tukufu kwamba usingetaka kabisa kuzungumzia masuala ya Meremeta kwa sababu ni siri za Jeshi. Baada ya kauli hii ya Rais na dhamira hii ya kujivua gamba kuhusiana na masuala ya ufisadi. Je, uko tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu kutaja wahusika wa Kampuni ya Meremeta na kuelekeza serikali kuchukua hatua zinazostahili kuhusiana na tuhuma hizo?" aliseama Bw. Mnyika.
     
Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema: "Rafiki yangu Mnyika hilo umerukia, hayo ni mambo ya ndani ya CCM la kujivua magamba kwa CCM ni kwa kuwa hayo ni mambo ya ndani ya chama, kwa hiyo halikuhusu na wala hapa si mahali pake."

Pamoja na majibu ya Waziri Mkuu, Bw. Mnyika, alisema katika ytaarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, kwa nafasi yake ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini anaitaka serikali itoe kauli ya kuruhusu ukaguzi maalumu kufanyika katika mahesabu ya kampuni ya Meremeta na kueleza hatma ya mgodi wa Buhemba ambao mali zake zinaendelea kuibwa.

Katika Orodha ya Mafisadi (List of Shame ) iliyotolewa na CHADEMA Septemba 15, 2007 katika Uwanja wa Mwembe Yanga, Dar es salaam ilielezea kuwa katika Ufisadi wa Meremeta Ltd kuwa malipo ya Dola za Marekani 118,396,460.36 zilizopelekwa katika akaunti isiyojulikana ya Benki ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini kama malipo ya madeni ya kampuni muflisi iliyokuwa inachimba dhahabu katika eneo la Buhemba wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara.

Awali, serikali ilikuwa ikisema kwamba Meremeta Ltd. ilikuwa ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Kibaha, Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, nakala ya usajili iliyotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales inaonyesha kwamba kampuni hiyo iliandikishwa nchini Uingereza Agosti 19, 1997 na ilifilisiwa huko huko Uingereza Januari 10, 2006.

Aidha, taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ya Mei 31, 2005 inaonesha kwamba Meremeta Ltd. ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania kama tawi, Oktoba 3, 1997. Vile vile taarifa hiyo inaonesha kwamba hisa 50 za Meremeta Ltd. zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini na hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa kupitia kwa Msajili wa Hazina katika Wizara ya Fedha. 

Hata hivyo, kuna utata mkubwa juu ya nani ni mmiliki hasa wa Meremeta Ltd. kwa kuwa taarifa ya BRELA inaonesha pia kwamba kampuni mbili za Kiingereza – London Law Services Ltd. na London Law Secretarial Ltd. – nazo zinamiliki hisa moja kila moja, za Meremeta Ltd. Kampuni hizo zinatumia anwani moja iliyoko 84 Temple Chambers, Temple Avenue, jijini London.

Benki Kuu iliruhusu fedha za umma kutumika kulipia madeni yote ya kampuni ambayo Serikali ilikuwa inamiliki hisa 50 tu wakati makampuni mengine ya kigeni yalikuwa yanamiliki hisa 52. Na kama ilivyosema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, uhalali wa Serikali kulipa madeni ya Meremeta Ltd. kwa Nedbank Ltd. badala ya kuiacha benki hiyo kudai malipo hayo kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo sawa na wadeni wengine haujulikani; 

Kwa mujibu wa barua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Benki Kuu iliruhusu au kunyamazia malipo mengine ya Dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kampuni ya Tangold Ltd. Katika hotuba yake bungeni ya tarehe 27 Juni 2007, Waziri wa Madini na Nishati Bw. Nazir Karamagi alidai kwamba"… mali na madeni ya MEREMETA yamehamishiwa kwenye kampuni mpya ya TANGOLD ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.”

Hata hivyo, barua ya BRELA ya Julai 4, 2007 inatamka wazi kwamba “Tangold Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius, na baadaye kuandikishwa nchini Tanzania kama tawi la kampuni ya kigeni.” Barua hiyo inaongeza kwamba kampuni hiyo ilipewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania Februari 20,  2006 na kwamba Katiba ya kampuni hiyo haikuonyesha “majina ya wanahisa wa kampuni na mgawanyo wa hisa.”

Barua hiyo ya BRELA inaonyesha kwamba wakurugenzi wa Tangold Limited ni pamoja na Gavana Balali (Marehemu), Bw. Gray Mgonja na Bw. Andrew J. Chenge. Aidha fomu Na. 1F inayohusu usajili wa kampuni za kigeni iliyowasilishwa BRELA na mawakili wa Tangold Limited na kusainiwa na Gavana Balali Mei 20, 2005 inaonyesha kwamba kampuni hii ilitokea “Jamhuri ya Mauritius” na anwani yake iko Suite 520, Barkly Wharf, Le Caudan, Waterfront, Port Louis, Mauritius.

Akijibu swali la Mbunge Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, alitaka kujua serikali imechukuwa hatua gani baada ya ripoti ya Ofisi ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikili kuhusu taarifa ya upotevu wa sh. bilioni 48 zilizotolewa na serikali kusaidia walioathirika na mdorodoro wa uchumi, Bw. Pinda alisema kuwa hadi sasa hana taarifa ya jambo hilo, hivyo yuko tayari kulitolewa ufafanuzi baada ya kupata taarifa.

8 comments:

  1. CCM ni mafisadi hakuna cha kujivua gamba wala nini ni usanii mtupu. Hakuna hata kiongozi mmoja wa CCM mwenye mapenzi mema na nchi hii. CCM ni genge la majambazi na wanafanya usanii tu.

    ReplyDelete
  2. CCM msitudanganye wananchi ya kuwa mmejivua gamba kwa kujiudhuru kwa akina makamba pamoja na sekretariet yake wakati gamba kuu bado lipo katika chama chenu ambao ni akina Rais Kikwete pamoja na wadau wake wa karibu bado mna kazi ngumu na mpango mliouweka wa kufanya ziara nchi nzima ili kupinga ufisadi ni moja ya danganya toto kwani wananchi wamechoka na wizi wenu pamoja na hali ngumu ya mwisha tuliyonayo watanzania kama mnataka kujisafisha vizuri katika chama chenu ni lazima Kuvua gamba kuu ambalo ni KIKWETE PAMOJA NA WASHIRIKA WAKE la sivyo chama chenu bado kinatoa harufu uvundo mkali

    ReplyDelete
  3. Gamba la ccm mme ligusa tu wala hamjalivua, kama kweli mnataka kujivua hebu ondoeni huyo kilanja wenu wa chama, maana huyo ndiyo mwenye hayo magenge yote mnayo hangaika nayo, yeye ndo alipanda hizo mbegu na zimeota.mmeacha viongozi wazuri kwa kulinda maslahi binafisi mkasahau maslahi ya taifa. Angalieni aibu mnayotupa hapo bungeni!!!! sipika asiyejua hata kanuni za bunge, mwabieni kiburi si uongozi, uongozi ni busara na hekima, mwabieni adese kwa mh.sitta. ccm mtamkumbuka sana mh.sitta kwa uongozi wake wa busara aliweza kulimudu bunge na hatimae matunda yake mnajivua gamba.Chuki binafisi za akina makamba ndo zimepelekea kuacha viongozi wazuri na waadilifu na kukumbatia mafisadi ambao wamewafikisha hapo mlipo, hebu angalieni vizuri mlipojikwaaa na pia mrudieni mungu mkatubu. ccm hoyeeee!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  4. gamba ni neno la ushabiki, halina maana kivile,unavua baya na wabaya unawaacha unaendelea kula nao?wanaogopana wale kama nini hawezi kusemana maana wamebebana wakafika walikofika,kila gamba anamwonea aibu gamba mwenzake,atamwanza wapi na wanakula wote?walipanga wajipangue kiaina kupotezea ili tujue wamejivua,hamna kitu,wako pamoja wanazidi kushikamana,ile ni staili ya kupumbazana,watembee mikoa yote,wamalize pesa kwa ushabiki?ujue ni pesa za nchii wanachezea tu,wanasubiriwa watazomewa na mawe watapigwa,ya Arusha tunayakumbuka.tunawangoja,mawe tu,jino kwa jino, basi.

    ReplyDelete
  5. Hivi ni sasa ndio wanatambua kuwa walikuwa na magamba? Walisubiri wapigiwe kelele ili watambue kuwa mambo si sawa ndani ya serikali na chama chao?

    Je ni kwa nini walimaka sana na kubeza wapinzani kuwa yote yaliyokuwa yakisemwa na wapinzani yalikuwa ni uzushi, matusi na uchochezi? Kwamba wapinzani si wakweli? Eti ni wabaguzi wa udini na ukabila?

    Kitu gani kimewafanya waamnini yale waliyokuwa wakiyakanusha pale yalipokuwa yakisemwa na hawa wabaguzi wa dini na ukabila (wapinzani)?

    Kwa hali hiyo basi, CCM pia ni wabaguzi na ni wadini. Kwa kuwa wanachukua hatua na kutekeleza yale yote yaliyofichuliwa na CHADEMA (wabaguzi), ha ha haaaa!!

    Watanganyika inabidi kufumbuka macho sasa. CCM wameishiwa. Walitumia nguvu za ziada kuwafanya Chadema waonekane waongo na no hatari. Walitumia hata nguvu za mkundu kwa lengo la kupakazia uchochezi wa ukabila na udini, ili kutupumbaza.

    Chaguo ni letu, kusuka au kunyoa!!

    ReplyDelete
  6. Waacheni na Magamba yao, wakiyavua wakabaki uchi ndo watajua bora wangeyaacha wakafa nayo bila aibu ya kubaki uchi kwani wataonekana kuwa walichanganyikwa kabla ya mauti ya kisiasa kuwafika ndo maana wakaanza kuvua na nguo zao (Magamba) Na huyo Pinda sijui ni mtoto wa mkulima wa aina gani, labda wanatumia matrekta kwa mitaji mikubwa kwani na yeye ni shabiki tu wa kina kikwete Fisadi, kwanza kiongozi gani hajiamini anahofia walioko juu kwa hofu ya kunyang'anywa tonge mdomoni. Wakafie mbali huko na Magamba yao.

    ReplyDelete
  7. Kama ccm walijua wana gamba, walishindaje uchaguzi? Kumbe waliiba kura! Walishindaje wakiwa na gamba? Wizi mtupu. Tena Makamba ukome kutumia maneno ya Biblia, eti unaenda kuandaa makao. Makao ya gamba au makao gani? Umeikufuru biblia. Ukome haraka kutumia maneno mazuri ya Bwana Yesu kwa kuhalalisha uchafu wako.

    ReplyDelete
  8. hivi pinda ni waziri mkuu wa nani?????????????????

    ReplyDelete