15 April 2011

Mapato na matumizi yazua kizaa zaa Mlimba

Na Deodatus Myonga, Morogoro

MWENYEKITI Mtendaji pamoja na Halmashauri ya kijiji cha Mlimba, Tarafa ya Mlimba wilayani Kilombero imesimamisha mkutano wa kijiji kutokana na wanakijiji
kutoridhishwa na taarifa ya mapato na matumizi.

Mkutano huo Mkuu wa kijiji ulifanyika Aprili 13, mwaka huu ambapo kwa pamoja wanakijiji waliamua kuwasimamisha Mwenyekiti, Bw. Ramadhani Mkumba na Mtendaji, Everesto Botha pamoja na Halmashauri ya kijiji kwa kutoridhishwa na utendaji wao na kutotoa taarifa ya kuridhisha ya mapato na matumizi.

Kwa mujibu wa mmoja wa wanakijiji waliokua kwenye mkutano huo, Bw. Shaban Mikongoro, mkutano huo ulikuwa wa pili baada ya wa awali kufanyika na kusomwa taarifa ya mapato na matumizi ambayo haikukubaliwa na wanakijiji.

Mkutano wa awali uliazimia kuundwa kwa kamati maalumu ya kuchunguza vyanzo vya mapato ya kijiji na matumizi kabla ya kufanyika mkutano mwingine.

Hata hivyo kamati hiyo ilipoundwa ilipata wakati mgumu katika kufanya kazi kutokana na kile kilichodaiwa kuzuiwa na Mtendaji wa Kijiji, lakini wajumbe wengine walifanya kazi hiyo kwa ugumu kwa kufutilia vyanzo vya mapato kama mashine ya nafaka ya kijiji na ushuru.

Mkutano huo umeazimia kutayarisha taarifa na kuituma kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero  na kueleza muhtasari wa mkutano na maamuzi waliyofikia.

No comments:

Post a Comment