04 March 2011

Tisa wafa ajalini Pwani, Dodoma

Na Waandishi Wetu

WATU tisa wamekufa papo hapo na wengine 63 kujeruhiwa vibaya katika ajali mbili zilizotokea katika mikoa ya Pwani na Dodoma jana.Katika tukio la
kwanza, ajali ilitokea katika Kijiji cha Kilimahewa Wilayani Mkuranga mkoani Pwani saa nane mchana na kuua watu sita, na kujeruhi wengine 43.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Bw. Absalom Mwakyoma,
alisema ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Mining Nice yenye namba T 357 BMF lililokuwa likitokea Mtwara kuelekea Dar es Salaam.

Alisema gari hilo liliacha njia na kupinduka kufuatia dereva Bw. Ally Bakari (33) kujisahau wakati akizungumza na simu ya mkononi wakati akiendesha.

Kamanda Mwakyoma, alisema miili ya watu wanne kati ya sita waliokufa katika ajali hiyo imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa taratibu za mazishi.

Aliwataja waliotambuliwa kuwa ni Bw. Issa Johari (33) mkazi wa Ukonga Dar es Salaam, Bi. Zainabu Rajabu (65) mkaziwa Mikumi na Bi. Sauda Haji (25) aliyekuwa amembeba mtoto Hawa Tamimu mwaka mmoja ambaye pia amefariki, wote ni wakazi wa Mitweru mkoani Lindi.

Alisema majeruhi 19 hali zao zilikuwa mbaya zaidi na kulazimika kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Alisema majeruhi wengine 27 wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga.

Kamanda Mwakyoma alisema jeshi lake linamshikilia dereva wa basi hilo ambaye inasemekana alikuwa 'deiwaka' aliyekabidhiwa usukani na dereva wa basi hilo aliyekimbia mara baada ya ajali hiyo.

Habari kutoka Dodoma zilisema kuwa ajali nyingine ilitokea Wilaya ya Kongwa na kuua watu watatu ambao hawajatambuliwa na kujeruhi wengine 20. Kati ya waliojeruhiwa watatu waliruhusiwa na 17 hadi jana jioni walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo.

Daktari wa Kitengo cha upasuaji, Dkt. Chilongola Robert alidai wamepokea maiti hizo saa 2:00 kutokana na ajali ya lori aina ya Fusso kufeli breki na kupinduka.

No comments:

Post a Comment