04 March 2011

Pinda aanza ziara Kagera leo

Na Mwandishi Maalumu

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda leo anaanza ziara ya siku nane kwenye mkoa wa Kagera ambako atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kutembelea
wilaya zote za mkoa huo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri Mkuu ataanzia Manispaa ya Bukoba, ataenda Muleba, Chato, Biharamulo, Ngara, Karagwe, Missenyi na kumalizia Bukoba Vijijini.

Baadhi ya shughuli ambazo Waziri Mkuu amepangiwa kufanya wakati wa ziara hiyo ni pamoja na kuzindua barabara ya Zamzam na mkutano wa hadhara kwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba katika uwanja wa Mayunga (Uhuru Platform).

Akiwa wilayani Muleba, Waziri Mkuu Pinda atakagua shamba la mkulima bora wa kahawa katika Kijiji cha Ilogero kabla ya kwenda Buganguzi ambako atakagua mashamba ya migomba ambayo yameshambuliwa na magonjwa ambayo mpaka sasa hayajajulikana kisayansi. Pia ataweka jiwe la msingi katika mradi wa umwagiliaji wa Kijiji cha Buyaga na kuhutubia wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Kasharunga.

Akiwa wilayani Chato Jumapili, Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi katika jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kufungua SACCOS ya Mshikamano kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Shule ya Msingi ya Chato.

Jumatatu Bw. Pinda atakagua mnada wa ng’ombe wa Lusahunga, wilayani Biharamulo, kukagua ujenzi wa wodi katika hospitali hiyo na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya St. Clara huko Rukaragata na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa CCM.

Wilayani Ngara Jumanne ijayo, Bw. Pinda atafungua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Ngara Farmers kabla ya kwenda kwenye mgodi wa Nickel wa Kabanga. Pia atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara huko Muurusagamba.

Waziri Mkuu pia atatembelea Karagwe Jumatano ambako atakagua bwawa la samaki huko Kishoju na kusalimiana na wananchi kisha kwenda Kayanga kuzindua jengo la masjala ya ardhi. Mchana ataweka jiwe la msingi katika Chuo cha Ualimu cha Katera kabla ya kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Isingiro.

Akiwa Missenyi, Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo. Baadaye ataelekea Kiwanda cha Sukari cha Kagera kuona mitambo ya kisasa ya umwagiliaji mashamba ya miwa. Pia atakagua shughuli za kiwanda hicho na kisha kuzungumza na wananchi katika uwanja wa Mashujaa wa Bunazi.

Akiwa Bukoba Vijijini, Waziri Mkuu ataenda Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku kutembelea maabara na baadhi ya vijishamba vya utafiti wa kilimo. Pia atakwenda Izimbya kuzindua majengo ya OPD, ya watoto, maabara, chumba cha upasuaji na jengo la ushauri nasaha na upimaji VVU (CTC).

Jumamosi ijayo, Waziri Mkuu atafanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu Mkoa kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam mchana huo.

5 comments:

  1. Mh.Pinda nimefurahi sana kusikia unakwenda mkoani kagera.Ninaomba utakapofika Wilayani Ngara ninaomba uunde tume au ufanye uchunguzi kuhusu mwenyekiti wa kijiji na serikali wanakula Rushwa wanataifisha mashamba ya wananchi wanawapa watu wenye fedha(Matajiri)Suala Mh.Dc analijua analifumbia macho.

    ReplyDelete
  2. Mheshimiwa ukimaliza ziara hizo tupe taarifa yako uliyoiona huko hasa kuhusu mpangowa bara bara ya rami, maendelo ya shule za msingi na sekondari, kilimo cha kahawa na migomba.

    ReplyDelete
  3. Mheshimiwa Pinda usisahau kuwaliza wahusika wa Wilay aya Muleba kwa nini umeme upitishwe Kimwani badala ya Ngote corridor kwenye watu na si mapori.

    ReplyDelete
  4. Kama kipinda kinafanya ziara kwanini CHADEMA wasifanye ziara lazima kieleweke tu mafisadi nyie

    ReplyDelete
  5. pinda pole sana hata wewe huna msimamo bado unatetea mafisadi.chiligati kauli zako na za kikwete ndio zinachochea vulugu siyo chadema kwani kukijenga chama si wakati wa uchaguzi tu na wewe wasira utamshughulikia nani wakati wananchi wamechoka na uongo WA CCm.wanaona kweli chadema kitawakomboa.tufike wakati tukubali mabadiliko ukianza kuwaambia wananchi hayo yalipita kwenye kampeini ni ujinga angalia uingereza na marekani kina obama wamepoteza viti vingapi na wanaongoza msifikiri watu wapo gizani bado.

    ReplyDelete