22 March 2011

Mtoto wa Gaddafi adaiwa kuuawa

TRIPOLI, Libya

Taarifa za kifo hicho, ingawa zimekanushwa na Serikali ya Libya ikisema kuwa ni 'habari potofu', zinasema kuwa Khamis ambaye ni mtoto wa sita wa Gaddafi, alipatwa na
ajali hiyo baada ya rubani wa ndege hiyo, Mohamed Mukhtar kuiangusha kwa makusudi katika moja ya kambi za majeshi ya Libya, ya Bab al-Aziziya, Jumamosi iliyopita.

Hata hivyo, vyanzo vya habari katika Serikali ya Gaddafi vimenukuliwa vikakanusha vikali taarifa hizo, vikisema kuwa ni 'habari zisizokuwa na maana yoyote'.

Vyanzo mbalimbali vya habari katika mtandao jana vilisema kuwa Bw. Mukthar alikuwa ameamuriwa kushambulia eneo la Agedabia, lakini ghafla akabadili uelekeo kwenda Kambi ya Bab al-Aziziya.

Kambi hiyo ya jeshi ya Bab al-Aziziya inasemekana ndiyo mahali ambapo Kiongozi wa Libya, Kanali Gaddafi amejificha na jamaa zake kadhaa.

Habari hizo za kifo cha Bw. Khamis, (32) zimesema kuwa alikufa katika hospitali moja mjini Tripoli, ambako alikuwa chini ya uangalizi maalumu. Kijana huyo wa Gaddafi imeripotiwa kuwa alikuwa ndiye Kamanda wa Brigedia ya 32, inayopambana na waasi wa Libya, wanaotaka kuondoa madarakani utawala wa miaka 40 wa kiongozi wa baba yake.

Baadhi ya mashuhuda pia wamenukuliwa wakikanusha kuwepo kwa ulipuliwaji wa mabomu katika Mji Mkuu Tripoli asubuhi ya jana, ambapo mwandishi mmoja alisema kuwa maisha katika mji huo yalikuwa yakiendelea kama kawaida.

Wakati huo huo, imeripotiwa kuwa ndege za kijeshi, zimeshambulia makazi ya kiongozi wa huyo yaliyopo mjini Tripoli na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye jengo moja.

Habari kutoka nchini humo zinaeleza kuwa mashambulizi hayo  yalifanyika usiku wa kuamkia jana na viongozi wa muungano wa majeshi hayo wanasema jengo lililoharibiwa lilikuwa linatumika kuamrisha majeshi ya Libya yanayopigana na waasi.

Ilielezwa kuwa baada shambulizi hilo waandishi wa habari walitembezwa kwenye eneo hilo lakini hakuna taarifa yoyote iwapo kuna maafa yaliyotokea.

Naibu Mkuu wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani, Bw. Bill Gortney alisema mashubulizi hayo hayajamlenga Kanali Gaddafi.

Televisheni ya Libya ilionesha maiti na magari ya kijeshi yaliyoteketea kwenye barabara ya kuelekea mji wa Benghazi ambao ni shina la wapinzani wa serikali.

Msemaji wa serikali alieleza kuwa watu 64 wameuwawa katika mashambulio yaliyofanywa na mataifa ya Magharibi, lakini hakuna njia ya kuthibitisha taarifa hiyo.

Awali Ofisa Mkuu wa Jeshi la Marekani,Bw. Mike Mullen, alisema ndege kutoka Qatar zinapelekwa nchini Libya tayari kushiriki katika operesheni dhidi ya nchi hiyo na nchi nyingine pia zimetoa ahadi kusaidia.

Bw. Mullen alieleza kuwa agizo la Umoja wa Mataifa, la kuzuia ndege za serikali kuruka katika anga ya Libya, sasa limetekelezwa, na majeshi ya Kanali Gaddafi, katika mji wa Benghazi, unaodhibitiwa na wapinzani, sasa hayawezi kusonga mbele.

Katika hatua nyingine, Urusi imetoa wito kwa Uingereza, Ufaransa na Marekani, kuacha kushambulia maeneo yasiyokuwa ya kijeshi na ikasema kuwa majeshi hayo pia yanawashambulia raia.

Naye Mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu, Bw. Amr Moussa alisema kuwa  mashambulizi hayo yamekwenda mbali, kushinda lengo la kulinda tu anga ya Libya, ambalo jumuiya yake iliyotaka.

No comments:

Post a Comment