22 March 2011

Magufuli acha ubabe-Kikwete

*Yeye asema ataendelea kulinda sheria kama alivyoapa

Na John Daniel

RAIS Jakaya Kikwete amesema kasi ya utendaji ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara iliyosababisha bomobomoa chini ya Wizara ya
Ujenzi imetawaliwa na ubabe na kumwagiza Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. John Magufuli kuangalia upya suala hilo.

Amewamwagiza Dkt. Magufuli kuendesha bomobomoa kwa kusimamia haki za wananchi kupewa muda wa kutosha kuhama, kulipwa fidia na kubomoa nyumba pale tu ujenzi unapotakiwa kuanza na si vinginevyo.

Akizungumza na watendaji wa wizara hiyo na taasisi zilizo chini yake jana, Rais Kikwete alisema kazi hiyo inaendeshwa kinyume cha taratibu kwa kuwa baadhi ya barabara zinazodaiwa kuvamiwa na wananchi zimepandishwa hadhi muda si mrefu.

“Wakati mwingine mnatumia ubabe mno, ndio maana hata 'meseji'  zinanifikia, hakuna mtu anayeweza kuvunja nyumba yake kwa saa 48, serikali haiwezi kutafuta nafuu kwa haki za wananchi.   

“Mnafanya hata watu wanachukia hizo barabara, watu wanaostahili fidia walipwe. Lazima muangalie historia ya barabara imetoka wapi,…siyo kuja na kubomoa maana hakuna mtu anayeweza kubomoa nyumba yake kwa saa 48,” alisema Rais Kikwete.

Aliendelea “Mtu anachimba msingi, anamwaga zege mko wapi? Ni ajabu! Hawa watu mnaowabomolea kila siku watendaji wanapita katika barabara hizo hizo na wanaona wanavyojenga bila kuchukua hatua, mtu akimaliza nyumba yake mnafika na kumbomolea, hili hapana,” alisisitiza.

“Hakuna sababu ya kuwabomolea watu kama barabara haijajengwa, wapeni hata miaka miwili au mitatu wajiandae kwanza,“ alisema Rais Kikwete.

Alisema yeye mwenyewe aliwai kushuhudia baadhi ya wananchi katika Mkoa wa Pwani wakitakiwa kubomoa nyumba zao na kuhama kwa madai kuwa wamejenga katika hifadhi barabarani kinyume na hali halisi.

Alisema katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Chalinze-Segera eneo la Msata zipo nyumba zilizowekewa alama za X zikitakiwa kuvunjwa kwa madai kuwa zimejengwa katika hifadhi ya Karabara Kuu ya Bagamoyo wakati eneo hilo kulikuwa na nyumba za zamani za wakoloni zilizojengwa takriban miaka 200 iliyopita.

Alisema katika eneo hilo barabara inayotakiwa kujengwa ndiyo iliyofuta wananchi, hivyo wana haki ya kuthaminiwa mali zao na kulipwa fidia na kunyume chake ni uonevu na ubabe wa watendaji.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aligiza Wizara hiyo kuhakikisha wanafuatilia kwa umakini mkubwa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara hususan na halmashauri kupitia Mfuko wa Barabara.

“Issue kubwa ni kuhakikisha fedha zinatumika kama  ilivyokusudiwa, tatizo ukaguzi wa CAG unazingatia sana vitabu vilivyoandikwa, vitabu vinaweza kuandikwa vizuri lakini hakuna barabara, mimi pale ….waliwahi kuandika vitabu vizuri kweli sh. milioni 400 zimetumika kujenga daraja lakini hakuna daraja wala!.

"Waziri Mkuu alienda pale ikabidi wengine awafukuze kwenye mkutano maana hali ilikuwa mbaya, ndio maana nimesema tuwe na ukaguzi unaoangalia value for money (miradi ilingane na fedha zilizotumika) taarifa ya vitabu tu,” alisema.

Pia Rais Kikwete alihoji matumizi mabya ya ardhi bila kujali viwanja vya michezo na kutaka wizara hiyo kuangalia pia suala la kuacha maeneo yaliyotengwa kwa jili ya michezo hususan uwanja wa Jangwani.

Kuhusu kilio cha Dkt. Magufuli kuwa wizara yake inakabiliwa na changamoto kubwa la ukosefu wa fedha kwa wakati iliyosababisha jumla makandarasi 35 kusitisha huduma huku wengine wakisitisha kabisa mikataba, alisema tayari serikali imechota sh. bilioni 250 kutoka katika bajeti za wizara mbalimbali na kuipa ujenzi.

Aliungana na Waziri Magufuli kuhusu kuanzishwa kwa usafiri wa reli kutokea kati ati ya mji hadi Ubungo hadi Kimara-Temboni kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.

“Msitegemee sana usafiri wa mabasi yaendayo kasi inaweza kusaidia katika kipindi hiki hadi miaka mitano 10 hivi, lakini kumbukeni kuwa idadi ya watu katika jiji hili inaongezeka kila kukicha, jaribuni kuangalia na njia nyingine kama reli kutoka pale Ttesheni hadi hata kule Temboni,” alisema.

Kuhusu ombo la Waziri Magufuli kuhusua muundo wa wizara yake kukwamisha kutoa nafsi kwa watendaji katika Taasisi zake Rais Kikwete aliahidi kusaidia kuhakikisha wahusika wanakamilisha kazi hiyo haraka.

Kwa mujibu wa taratibu muundo wa wizara ni kazi ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kwa upande wake Waziri Magufuli alimuhakikishia Rais Kikwete kuwa atahakikisha anatimiza wajibu wake na kusimamia sheria bila kulegea kama alivyoahidi siku alipoapishwa na atalinda na kusimamia sheria.

“Mheshimiwa Rais tutaendelea kusimamia kwa kuhakikisha wote waliojenga kwenye hifadhi ya barabara wanaondoka, tulipoapishwa tuliapa kulinda sheria na nitaendelea kusimamia sheria.

Malalamiko madogo madogo yaweke tu pembeni mheshimiwa rais hasa kwa kuzingatia kuwa katika kipindi chako ndio miradi mingi ya barabara zinajengwa, sisi tutafanya kazi kweli kweli hatutarejea ila oganazesheni ya wizara ndio tunasubiri, ndio maana umesikia watendaji wengi wanakaimu nafasi zao,” alisema Dkt. Magufuli.

Alisema hadi sasa Idara ya Ufundi na Umeme TEMESA inadai taasisi mbalimbali za serikali sh. bilioni 4. 1 kutokana na kazi mbalimbali hali inayokwamisha utendaji wa idara hiyo na kwamba tayari amemwandikia Waziri Mkuu barua juu ya tatizo hilo.

Licha ya gizo hilo pia Rais Kikwete alimpongeza Waziri Magufuli na watendaji wake kwa kazi.

3 comments:

  1. Kumbe muheshimiwa rais unayajua mengi kuhusu changalamacho, watanzania wa sasa wanaelewa, na wameenda shule kwa kupitia vyombo vya habari watu wanajua ni kiasi gani cha pesa zinatolewa katika miradi kama ya barabara, mashule, maji,nk. Sasa kama viongozi mtakaa kungoja taarifa kuwa pesa hizo zimetumika kwa kuangalia vitabu mjue kabisa mifisadi itachekelea na kuona viongozi wote hamna akili.Muheshimiwa rais wahamasishe watu wako uliowaweka madarakani kuacha kufanya kazi kwa simu wafatilie pesa zetu kujengewa mabarabara BOM, madaraja BOM ukiangalia miundombinu yetu na pesa zinazotumika huamini. SASA swali Langu muheshimiwa Rais hawa viongozi wavivu wasiothamini matumizi ya pesa zetu wanini hawa? fukuza hawa watu hawatufai waangalie mifano ya Muh.Magufuli Muh,Tibaijuka hawa wako( front line) na siyo kuvaa suit kukaa maofisini kwa nchi kama tanzania ambayo tunalia na miundombinu yetu lazima viongozi mbadilike na muende na wakati.

    ReplyDelete
  2. Nchi yetu inao wataalam wa kutosha na wanakatishwa tamaa na utendaji mbovu wa mabosi wasiowajibika. mtalaamu anaweza kuleta ripoti kuhusu hujuma kama kazi mbaya ya mjenzi, na bosi anazima tuhuma hizo kwa kishindo cha kufuatilia rushwa kutoka kwa Contractor. Vitendo kama hivyo vinakatisha tamaa.

    Nchi yetu itajengwa na wananchi wenye uchungu wa nchi yao. Tatizo kubwa la ujenzi ni kutowaendeleza na kuwawezesha wataalamu wetu na makondorasi kutenda kazi. Bado tumekumbatia makampuni ya nje hata kama hayafai kwa kila hali (kifesdha, kiutaalamu). Ndio maana utasikia kampuni ya nje wamechukua pesa na kuishia au kufanya kazi hovyo hovyo(mifano halisi ipo, haihitaji kuambiwa). Tunapindisha taratibu ili kutimiza mahitaji binafsi na sio ya nchi!

    Makampuni yanayopewa kazi mengi ni ya nje na yale ya wazalendo wanaishia kujaza tenda kila siku na kukosa (wanakuwa wasindikizaji ktk miradi). Yale makampuni machache ya wateule ndio yanapewa kazi kila siku hadi wanazidiwa (wanavimiwa na kazi) na wazalendo wanakufa kwa unyafuzi/ukata! Waulizeni TANROADS na NFFS watawaeleza makampuni yaliyoko kwenye "inner circle" ya kuvimbiwa na kazi..hata mheshimiwa unafahamu. Sasa hawa wazalendo wataendelezaje nchi kwa kuishia kujaza tenda bila kazi???

    ReplyDelete
  3. Kumbe muheshimiwa kikwete unayajua mengi kuhusu changalamacho na matumizi feki, mbona hujaongelea kwa undani, na kumkalipia mshikaji wako Rostam Aziz kwa kufanya deal feki na serikali yako. kuwa jasiri ongea na swala hilo pia

    ReplyDelete