31 March 2011

Kikwete aagiza mahindi yapunguzwe bei

Na Mwandishi Maalumu

RAIS Jakaya Kikwete ameanza kuchukua hatua kupunguza bei ya chakula nchini, na hasa jiji la Dar es Salaam, kwa kuagiza chakula cha akiba cha taifa kuingizwa katika
masoko ya mijini mara moja na kupunguza makali na gharama ya maisha kwa wananchi.

Agizo hilo limekuja baada ya kilio cha muda mrefu cha wananchi kikikolezwa na maandamanao ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wakimtaka Rais Kikwete kuingilia kati suala hilo ili kupunguza ugumu wa maisha.

Katika agizo hilo, Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema Rais Kikwete amesema kuwa kazi hiyo ya kuingilia soko na kupunguza bei ya chakula iwe ya nyongeza na ya kudumu ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na Wakala wa Akiba ya Chakula ya Taifa (NFRA).

Alisema kuwa miji ya Tanzania ina masikini wengi na kuwa gharama kubwa ya maskini hao ni bei kubwa ya chakula na kuwa ni wajibu wa serikali kuchukua hatua za makusudi kuwapunguzia wananchi gharama hizo za maisha kwa kuingia chakula cha bei nafuu katika masoko ya mijini.

Rais Kikwete alitoa maagizo Jumatatu alipotembelea maghala ya NFRA mjini Dar es salaam kama mwendelezo wa ziara zake na Wizara mbalimbali za Serikali na taasisi za wizara hizo.

alisema kuwa kama hatua za kuingilia soko zingechukuliwa tangu Oktoba mwaka jana wakati bei ya mahindi ilipokuwa sh 300 kwa kilo mjini Dar es Salaam, bei hiyo isingepanda na kufikia sh 430 kwa bei ya sasa.

“Hii ndiyo kazi yetu kuanzia sasa yaani kuhakikisha kuwa tunaingilia soko, kuingiza chakula cha kutosha na hasa mahindi kwa sababu hiki ndicho chakula kikuu cha Watanzania na kuhakikisha kuwa tunaishusha bei hiyo ya mahindi hadi sh 300 katika kipindi kifupi iwezekanavyo,” Rais amewaambia maofisa wa Wizara na Wakala huo.

Alisema kuwa lazima viongozi waelewe kuwa hata mijini kuna upungufu wa chakula. “Tafsiri ya njaa ni kama mji haupati chakula cha kutosha basi kuna njaa. Hivyo tujipe mamlaka ya kuingiza haraka soko ili kuwalinda wananchi kwa sababu hatuwezi kuwaacha wananchi mikononi mwa wafanyabiashara binafsi wa chakula ambacho kichocheo chao kikubwa ni faida,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Hii sasa ni kazi yetu ya kila siku yaani kufuatilia masoko na kuhakikisha kuwa kinakuwepo chakula cha kutosha kupunguza bei. Chezeni na soko la Dar es Salaam ili kuhakikisha kuwa bei zinakwenda chini haraka iwezekanavyo. Twendeni katika masoko yote Tandale, Tandika na kwingineko siyo kujua bei ya chakula lakini kujua ni kiasi gani cha chakula kinahitajika kushusha bei kwa ajili ya wananchi.”

No comments:

Post a Comment