16 March 2011

Hakuna amani kwenye umaskini-Balozi

"...amani haiwezi kuwepo kama kuna umasikini, watu wanalala na njaa, watoto wanashindwa kwenda shule, hakuna ajira"

Na Grace Michael

BALOZI wa Rwanda nchini Tanzania Bi. Fatuma Ndangiza amesema kuwa nchi yoyote
haiwezi kuwa na amani endapo haijapunguza kiwango cha umasikini wa wananchi wake.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa suala la amani lisiachwe kwa serikali peke yake bali kila mdau ashiriki kwa nafasi yake kuhakikisha anaongeza sauti katika kuleta amani na maendeleo kwa ujumla.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kufunguliwa kwa kongamano la uundwaji wa Jukwaa la Taifa la Asasi za Kiraia ambalo mchakato wake unatokana na tamko la Dar es Salaam pamoja na mkataba uliosaniwa na viongozi wa nchi za maziwa makuu.

“Kuwepo kwa jukwaa kutasaidia kuzuia machafuko wakati yanapoonesha dalili za kujitokeza, lakini amani haiwezi kuwepo kama kuna umasikini, watu wanalala na njaa, watoto wanashindwa kwenda shule, hakuna ajira...hivyo suala hili haliwezi kuachwa kwa Serikali tu bali ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha analinda amani au kupaza sauti ili kuleta maendeleo,” alisema Bi. Ndangiza.

Naye Balozi Mstaafu na Mdhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Brigedia Jenerali (mstaafu) Hashim Mbita alisema kuwa kukosekana kwa majadiliano kati ya serikali na raia wake kunasababisha kutoweka kwa amani na hayo yanajionesha katika nchi mbalimbali, hivyo kuwapo umuhimu mkubwa wa kutoa kipaumbele katika jukwaa hilo ili liweze kusimamia mambo yaliyoanishwa.

“Magomvi katika nchi mbalimbali yanatokana na kukosekana kwa majadiliano kati ya raia na serikali na tukumbuke kuwa wakati tukifanya kongamano hili la kuunda jukwaa, nchi kadhaa amani yake inaelekea kutoweka hivyo tuone umuhimu wa jambo hili,” alisema Balozi Mbita.

Mkataba uliosaniwa na wakuu wa nchi na serikali wanachama wa mkutano wa kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu, walitambua umuhimu wa kuheshimu demokrasia na utawala bora, misingi muhimu iliyoainishwa ndani ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa kuanzishwa Umoja wa Afrika, ambayo ni kuheshimu mipaka ya nchi, uhuru wa nchi kujiamulia mambo yake bila ya kuingiliwa na nchi nyingine na kuondokana na vitendo vya uchokozi.

Viongozi hao pia walisisitiza dhamira ya kujenga uhusiano kati ya nchi zao kwa kufuata misingi iliyoainishwa katika hati za kisheria za kimataifa na kanuni na misingi inayokubalika duniani, vipaumbele vya kisiasa na kufuata misingi kama ilivyoelekezwa katika Azimio la Dar es Salaam ambalo linasisitiza amani na usalama wa kudumu, eneo tulivu kisiasa na kijamii, pia kuwa na eneo lenye uchumi unaokua na maendeleo ya pamoja kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya watu wao.

Akifungua kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule alisema kuwa jukwaa hilo lina umuhimu mkubwa kwa kuwa litafanikisha upatikanaji wa wajumbe watakaoshiriki mikutano mbalimbali katika kusimamia amani na kuleta maendeleo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Usu Mallya akizungumzia kongamano alisema kuwa vurugu nyingi katika nchi mbalimbali zinasababishwa na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi husika hivyo mchakato huo wa kuwapata watu watakaowakilisha katika mkutano mkuu wa kimataifa wa ukanda wa maziwa makuu utasaidia kuwasilisha mawazo ya wananchi kwa makundi yao.

No comments:

Post a Comment