02 February 2011

Walimu 32 wagoma Arausha

Na Glory Mhiliwa, Arusha

WAALIMU zaidi ya 32 wamegoma kuingia madarasani na kuandamana hadi  Manispaa ya Arusha, wakishinikiza kulipwa fedha zao za kujikimu za
siku 14, ambazo hawajalipwa tangu walivyoripoti Januari 24 mwaka huu.

Wakizungumza nyakati tofauti huku wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti na kuiimba wimbo 'kama siyo, juhudi zako Nyerere, Mkurugenzi ungekuwa wapi'.

Mmoja wa walimu hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kuwa walifika katika vituo vyao vya kazi, wakiwa katika  shule tofauti tofauti, lakini hadi  leo halipwa fedha hizo.

 Sisi tutaishi vipi, tunadaiwa madeni, imefikia hatua hadi vyeti vyetu tumewapa wenye nyumba wavishike, ili wasubiri fedha, tutaishi hivi mpaka lini, maisha Arusha magumu. mikoa mingine wamelipwa, iweje Arusha bado, kuna nini Manispaa, alisema.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka kuwa, Serikali fedha za kulipa Dowans zipo, lakini posho za kujikumu waalimu hakuna, huu ni ufisadi wa hali ya juu.

Mwalimu Antony Pius Mganule, alisema kuwa yeye amepangwa Shule ya Sekondari ya Felix Mrema, ila anashindwa kufundisha wanafunzi kwa sababu ya njaa kali.

 Alisema hivyo Januari 31 walilazimika kufika Manispaa kudai posho zao za kujikimu, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 00 jioni, lakini waliambiwa na Mkurugenzi wasubiri wafike waalimu wote ndipo walipwe fedha hiyo.

Tutasubiri vipi, kama wenzetu hawatafika, wamekwenda sehemu zingine au shule za watu binafsi tutakaa kusubiri ili tufe njaa” alisema Mwalimu Mganule.

Naye Mwalimu Andrew Paul wa Shule ya Sekondari Kaloleni, alisema kuwa wanasikitishwa na kitendo cha
manispaa kuwanyima posho zao ambazo wana uhakika hazina ilishazituma, ila zinabanwa tu kwa sababu zao za kiufisadi.

Alisema kuwa waalimu wa stashahada  wako  zaidi ya 80 na wa shahada wako 89, lakini hadi jana walikuwa wamefika waalimu 32 tu.

Aidha alisema fedha anayodai kwa kila mwalimu  wa shahada ni shilingi 630,000 na mwalimu wa Stashahada
ni shilingi 910,000.

Kwa upande wa mwanafunzi wa shule ya sekondari Kaloleni, Joseph Kimambo, alisema kuwa, kitendo cha serikali kutowalipa waalimu wao, ni cha kusikitisha, kwani kinachangia kuzorotesha elimu.

Sisi wanafunzi tupo darasani, ila tangu jana waalimu wako manispaa wanadai haki yao, kwa hali hii tutaendelea kufeli na kudidimiza elimu, lazima ifike mahali serikali ijali waalimu wetu, alisema Kimambo.

Hata hivyo akijaribu kuwatuliza waalimu hao, Mkurugenzi wa  Manispaa ya Arusha, Estomiah Changah, aliwaomba waalimu hao kukubali kupokea nusu fedha wanayodai, baki wasubiri hadi hazina itume tena. 

Jamani nawaomba mpokee fedha nusu, kwani hata hivyo Halmashauri hii ya Manispaa ya Arusha, tumejitahidi kukopa kila mahali, ili msiadhirike, huku mkisubiri zingine, sasa msigome ndugu zangu waalimu, au wengine  hamna nia ya kufundisha nini, maana naona kuna hizo dalili, mnataka kupokea fedha  muondoke, alisema Bw. Changah.

Aidha alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa aliyonayo waalimu wa stashahada wako 46 na Shahada wako 24, waliofika Arusha tangu Januari 28 mwaka huu. Alishauri wasubiriwe pia.

Hata hivyo alisema kuwa mpaka sasa anafanya mawasiliano na Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Jumanne Sagini, na amesikitishwa na kitendo cha waalimu kugoma na hakufikiria watachukua hatua hiyo.

1 comment:

  1. Tulipofikia ni dalili tosha ya kitakachotokea siku za usoni!Mara migomo vyuo vikuu,mara maandamano ya walimu kushinikiza kulipwa ,mara mauaji Arusha,mara Dowans,
    Hivi nini hatma ya Taifa letu?Chonde chonde mliopo madarakani angalieni msijutie viti mlivyokalia visiwatokee puani mkaikimbia nchi!Hivi kwanini walimu hawasaminiwi kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa!Our Government plants the seeds for its own distruction\Grave!

    ReplyDelete