11 February 2011

Polisi wamnusuru Waziri Nundu TRL

Na Benjamin Masese

WAZIRI wa Uchukuzi Bw. Omari Nundu jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kupokewa na mabango na baadaye kuondolewa katika
mkutano wa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwa ulinzi wa polisi baada ya kushindwa kukata kiu yao juu ya kuvunjwa kwa mkataba wa RITES na hatma ya mafao yao.

Bw. Nundu ambaye alifika katika ukumbi wa Kapuya akimbatana na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli, Bi. Ruth Makelemo na askari wachache, baada ya mkutano ilibidi nguvu za polisi ziongezwe kumsindikiza baada ya jazba za wafanyakazi kuongezeka.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamepambwa katika ukumbi huo yalisomeka, 'hapa pesa tu', 'hapendwi mtu bila pesa', 'hapa hakieleweki kwa maneno ya ahadi labda Yesu arudi', 'penye njaa hapatawaliki', 'tunadai haki zetu kwa maslahi ya nchi, 'tunaombwa kulipwa ili amani iendelee kuwepo'.

Hali ya kutokuwepo amani ilianza kujionesha mara tu Bw. Nundu alipokaribishwa meza kuu na kuketi huku wafanyakazi wakianza kutamka maneno ya kumuomba kuwaongoza katika mapambano ya kudai mafao yao kwa njia yoyote ile.

Bw. Nundu alianza kufafanua kwamba serikali ipo katika hatua za mwisho kusaini mkataba wa kuachana na RITES, kitendo kilichoamsha munkari wafanyakazi wakidai kuwa tamko hilo limewahi kutamkwa na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Dkt. Shukuru Kawambwa na hatimaye yeye, hivyo si jambo geni kwao na halina ushawishi wala utekelezaji wowote.

Kutokana na kauli hizo za wafanyakazi zilionekana kumkasirisha Bw. Nundu na kuanza kuushambulia uongozi wa Chama cha Wafanyakazi (TRAWU) kuwa ni wanafiki kwa kuwa wanahamasisha mgomo kinyume na taratibu, huku wakifanya mambo yao tofauti na makubaliano ya vikao vinavyowakutanisha na serikali.

Bw. Nundu alisema kuwa aliwataka TRAWU kuweka unafiki wao kando na kuanza kufanya kazi ya kutafuta suluhisho la madai yao pasipo chuki huku akisisitiza kutopendezwa na maandamano na mgomo katika wizara anayoiongoza.

Hali ilizidi kumbadilikia baada ya Bw. Nundu kuelezea kuwa serikali haina mpango wa kuwalipa hivi karibuni, bali ipo katika hatua za kutafuta fedha zaidi sh. bilioni 63 za kuboresha miundombinu ya reli.

Kauli hiyo ilisabisha mkutano kuvurugika huku kukiwepo kila dalili ya kutoweka amani kutokana na kila mfanyakazi kumshambulia kwa maswali bila utaratibu.

Bw. Nundu aliendelea kushikilia msimamo huo mbali ya kuwepo ombi la kutaka fedha hizo kulipwa mafao ya wafanyakazi kwanza kabla ya kuboresha miundombinu ya reli kwa kufufua mioyo yao ili kuleta mari ya kufanya kazi.

"Ninachowaeleza sasa ndio msimamo wa serikali, hivyo hatuwezi kufanya kazi kwa kushinikizwa na watu au kikundi fulani," alisema, kabla ya kuondolewa hapo kwa ulinzi huku akisindikizwa na wimbo wa 'Tutaonana wabaya' ulioimbwa na msanii Q Chilla.

Awali, Bw. Nundu alisema kuwa kila mwezi serikali inatenga sh. bilioni 1.1 za kulipa mishahara ya wafanyakazi wa TRL, kitendo alichokiita ni mzigo kwa serikali, kwa kuwa hivi sasa haipokei fedha zozote kutoka kwenye kampuni hiyo inayotengeneza hasara.

Alisema kuwa hadi sasa serikali imetumia sh. bilioni 28 kwa kuwalipa wafanyakazi wa TRL ambapo kila mwezi huongezeka, pia jumla ya sh. bilioni 45 zinahitajika kuwalipa mafao wanayodai.

Baada ya Bw. Nundu kuondolewa, Katibu Mkuu wa TRAWU, Bw. Slyvester Rwegasira alizungumza na wafanyakazi hao na kukubaliana kukutana leo kutoa tamko lao.

3 comments:

  1. Serikali ya tanzania inayo matatizo makubwa sana na haya matatizo yanasababishwa na watu wasio makini, shirika la reli kubinafsishwa tulifikiri litatengeneza faida leo hii shirika limezama kwenye tope zito kwasababu mwekezaji alikuwa makini kuibia nchi tu hapa nani wa kulaumiwa wafanyakazi au serikali? Waziri Nundu na serikali wacha ubabe lipa kwanza wafanyakazi alafu tafuta hela za kufufua shirika na muundo mpya, tafuta hela benki ya dunia, benki ya maendeleo Africa na mashirika mengine ya kimataifa ya fedha na kuwepo na usimamizi wa kutosha faida itapatikana vizuri tu. Prudence kahatano.

    ReplyDelete
  2. Serikali itatawala kwa kutumia polisi mpaka lini? Hili ni swali la kujiuliza wenyewe: Je alama ya udikteta hii?

    Kwanini wananchi wanahasira na serikali yao hivi?

    ReplyDelete
  3. Enyi Ndugu zangu wapendwa, nawaombeni mnisikilize tu katika ujinga wangu,
    Tanzania kama tanzania ilikuwa na mtazamo mzuri saana hasa ukiwa uliwasikiliza wanga wetu, tulikuwa na Motto..
    <<Ujamaa na kujitegemea, Njia kuu za uchumi kumilikiwa na wananchi, watu wote sawa.. na mengi zaidi ya hayo. hayo tunayakubali. wakati wa kuyatekeleza ndipo tatizo lilianza sababu ni kukosa viongozi wenye kuipenda nchi yao. TRL inafikwa na hayo kutokana na kukosa Kiongozi mwenye uelekeo. musimlaumu huyo waziri bali tujilaumu wenyewe kwani tunachagua ambao wameshachaguliwa badala ya kutafuta kiongozi mwenye kufaa? angalia Malaysia walikuwa maskini wa kutupwa sasa vipi? viongozi wao wanataka maendeleo na si kujinufaisha. ushauri tukae chini na kuanza kutengeneza Kiongozi, kutengeneza sio kupewa bali kutoka jasho kwenye magoti tukiomba MUNGU atupe wa kutoondoa kwenye shida hii

    ReplyDelete