Na Mwandishi Wetu
MSAFARA wa Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete umepata ajali na iliyohusisha magari matatu katika eneo la Ruvu Darajani mkoani Pwani na
kusababisha kifo cha dereva wa gari la usalama, Bw. Ramadhan Mkoma (58).
Katika ajali hiyo watu wengine 14 walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, watatu kati yao hali zikawa mbaya zaidi na kukimbizwa Hospitali ya Taifa (MNH) kwa matibabu zaidi.
Waliokimbizwa MNH kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Tumbi, Dkt. Andrew Lwari, ni Hassan Hamidu (36) aliyekuwa anatapika damu, Charles Sebastian (31) aliyevunjika mfupa wa nyonga na Nassoro Mgeni (30) aliyevunjika mifupa miwili ya miguu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani pwani, Bw. Absalom Mwakyoma, ajali hiyo ilitokea saa 6:00 mchana wakati Mama Kikwete akitoka Dar es Salaam kwenda nyumbani kwake Msoga kupumzika.
Bw. Mwakyoma alisema ajali hiyo ilisababishwa na basi la Moro Best T 267 BHC lililokuwa linatoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam kugonga basi dogo aina ya Toypta Hiace lililokuwa limeegeshwa pembeni kupisha msafara wa Mama Kikwete, na kuserereka hadi kugongana na uso kwa uso na gari la usalama T 846 AKP lililokuwa linaongoza msafara.
Katika ya majeruhi 14, watatu walikuwa kwenye gari la msafara, saba mwenye Hiace na wanne kwenye basi la Moro Best.
No comments:
Post a Comment