07 February 2011

Manchester yapata kipigo cha kwanza

LONDON, Uingereza

MENDE ameangusha kabati! Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea kuhusu kufungwa kwa vinara wa Ligi Kuu England, Manchester United ilipocheza na timu ya
mwisho kwenye msimamo, Wolves.

Mwiko wa Manchester United, kutofungwa katika Ligi Kuu msimu huu hatimaye ulivunjwa na timu ya Wolves, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 wakiwa ugenini katika Uwanja wa Molineux.

Wenyeji walilazimika kutoka nyuma kwa kukumboa bao waliloanza kufungwa na United katika dakika ya tatu, kupitia kwa Luis Nani.

Wolves inayonolewa na kocha, Mick McCarthy imeweza pia kuvunja rekodi ya Manchaster united ya kutofungwa mechi 30 katika Uwanja wa Molineux.

Baada ya kutagulia kufungwa, Wolves ambayo ni ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ilikuja juu na kusawazisha kupitia kwa George Elokobi, dakika ya 10 kabla ya Kevin Doyle kufunga goli la ushindi dakika ya 40.

United ilianza kupata pigo mapema baada ya Rio Ferdinand, kuumia wakati wa maandalizi ya mechi.Jonny Evans, alichukua nafasi ya mchezaji huyo na kucheza sambamba na Nemanja Vidic.

Kuumia kwake hakukuonekana kuathiri timu ya Mashetani hao Wekundu baada ya Nani, kufunga bao la kuongoza mwanzoni mwa mchezo.

Elokobi aliiletea furaha Wolves kwa kufunga goli kwa kichwa baada ya kupata mpira kutoka kwa Matt Jarvis.

United ilionekana kuchachamaa kutaka kurejesha goli, ambapo washambuliaji Ryan Giggs na Berbatov walionekana kuwa tishio.

United ilifungwa bao la ushindi kutokana na makosa ya Evans na kufanya Doyle, akwamishe mpira wavuni.

Nenad Milijas naye nusura afunge goli baada ya kuchezewa faulo na Rafael.

Baada ya mapumziko huku United ikiwa nyuma kwa kufungwa mabao 2-1, United ilikuja juu na kipa wa Wolves Wayne Hennessey aliokoa mpira wa krosi wa Nani.

Wolves ilikuwa imara kuokoa mipira iliyokuwa ikipigwa na Rooney, Giggs  na Berbatov.

Javier Hernandez alimpasia mpira mzuri
Berbatov, lakini alishindwa kufungwa.

Kipa wa United Van der Sar katika dakika ya 74 alifanya kazi ya ziada kookoa goli kwa mpira uliopigwa langoni mwake.

Dakika ya 85, United ililalamika kwa kunyimwa penalti baadaya, Evra kupiga mpira na Karl Henry aliunawa kwenye eneo la hatari.

Kwa matokeo hayo United, imeendelea kuwa kileleni ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza mechi 25 ikifuatiwa na Arsenal, yenye pointi 50 ambayo nayo ilitoka sare ya mabao 4-4 dhidi ya Newcastle United.

Manchaster City ambayo ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi West Bromwich, yote yakiwekwa kimiani na Carlos Teves iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49.

No comments:

Post a Comment