22 February 2011

Magufuli apigilia msumali mabango barabarani

Na John Daniel

WAZIRI wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli amewashangaa wanaopinga kuondolewa mabango yaliyowekwa katika hifadhi za barabara kuu na kuweka
wazi kuwa wanapoteza muda badala ya kutii agizo hilo na kuyaondoa mapema.

Amesema watu hao wanapaswa kutafakari kiapo chao cha kulinda sheria kwa kuwa agizo hilo linatokana na sheria halali namba 13 ya mwaka 2007 na sheria zingine za nchi.

Dkt. Magufuli alitoa msimamo huo jana katika Kikao cha Kamati ya Bunge ya Miundombinu na wizara yake pamoja na wadau mbalimbali wa barabara kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam.

"Hata mabalozi wamelalamikia mabango yaliyowekwa barabarani, mengine yanaweza kusababisha ajali, mimi niliapa kulinda sheria za nchi na kumalizia na Mungu nisaidie, hayo mabango lazima yaondolewe.

Hatuwezi kukiuka sheria na kuweka mabango kukusanya pesa za kulipa posho halmashauri, lakini katika barabara zinazosimamiwa na halmashauri waweke mabango hata katikati ya barabara," alisema Dkt. Magufuli.

Alisema kitendo cha halmashauri kuweka mabango hayo katika hifadhi ya barabara ni sawa na mtu kujenga nyumba yake kisha jirani yake kuingiza mpangaji bila kumshirikisha mwenye nyumba, jambo ambalo ni kosa.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi alisema ujenzi wa vituo vitano vya kulaza magari hayo, kupakia abiria na kugeuzia pamoja na uhamasishaji nguzo za umeme umeanza.

Alitaja vituo hivyo kuwa ni kituo cha kulaza mabasi na kupakia abiria Ubungo itakayogharimu sh. bilioni 14.67, kituo cha kulazia mabasi Jangwani sh. bilioni 12.86 pamoja na kituo cha kugeuzia na kupakia abiria Kivukoni sh. bilioni 5.02.

Alitaja vituo vingine kuwa ni kile cha kugeuzia mabasi na kupakia abiria cha Kariako sh. bilioni 6.35 na vituo vya kupokelea abiria (feeder stations) sh. bilioni 4.4.

Alisema uhamasihaji  wa nguzo za umeme utagharaimu sh. bilioni 5.6.

Kuhusu ujenzi wa daraja la Kigamboni utakaogharimu dola za Marekani milioni 130 unaotekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamuu (NSSF) tayari asilimia 60 zimeshatengwa kwa mradi huo na kwamba asilimia 40 bado zinatafutwa.

Alitaja mkakati mwingine wa kupunguza msongamano katikati ya mji wa Dar es Salaam kuwa ni kubuni usafiri wa majini kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.

Alisema hatua za haraka za (Quick wins) za kupunguza msongamano kuwa zinaendelea vizuri katika barabara zinazojengwa kwa sasa na kusisitiza kuwa waliojenga ndani ya hifadhi za barabara hawatalipwa fidia kwa kuwa walikiuka sheria.

"Tulianza kwa kuvunja Ofisi ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam ili yeye mwenyewe apate uchungu kuvunja nyumba zote zilizojengwa ndani ya hifadhi ya barabara.

Hata Wizara ya Maji nayo ipo ndani ya hihadhi ya barabara, ikifika wakati tunataka kujenga barabra, jengo la TANESCO litabomolewa bila kulipwa fidia, hakuna cha CCM, CUF, CHADEMA, kiongozi wala raia ni sheria tu ukijenga ndani ya hifadhi ya barabara tutavunja, hatutasubiri eti mtu mmoja akwamishe jamii kupata huduma ya barabara safi," alisisitiza Dkt. Magufuli.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Peter Serukamba, alisema imefika wakati wa nchi kufanya kazi kwa vitendo na kwamba maneno ya kisiasa sasa yametosha.

"Hatuwezi kuwa taifa la maneno tu kila siku, ni lazima sasa utekezaji uonekane, tumechoka na foleni ya Jiji la Dar es Salaam, gharama ya ujenzi wa daraja la Kigamboni ni sh. bilioni 100, lakini kivuko moja ni bilioni saba tu.

"Tukinunua vivuko vitatu kwa sh. bilioni 21 tu pale tutamaliza kabisa tatizo la usafiri pale majini," alisema Bw. Serukamba akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundo mbinu.

Awali katika kikao hicho Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama  barabarani Mkoa wa Dar es alaam walilalamikia utendaji mbovu na kuweka wazi kuwa wanapata wakati mgumu kuongoza magari mvua ikinyesha kwa kuwa barabara zijaa maji.

Walisema hata mashimo wanalazimika kuziba wenyewe na kwamba taa za kuongozea magari zinapozima wanajibiwa kuwa LUKU imesha na kwamba si mbovu jambo ambalo ni tatizo la kiutendaji tu.

4 comments:

  1. Hongera Magufuli.

    Tukitaka maendeleo katika hii nchi ni lazima tuwe wakweli na tufuate na kutekeleza kila jambo kwa mujibu wa sheria bila kuogopa.

    Tungepata mawaziri kumi kama Magufuli ndio tungeweza kuuzika umasikini na kuona uzuri na utajiri wa hii nchi yetu.

    KEEP IT UP DR. MAGUFULI.

    ReplyDelete
  2. Hauitwi "msumali" unaitwa msumari. Nyie waandishiwa habari uchwara mnaharibu lugha yetu ya Kiswahili. Rudini shule

    ReplyDelete
  3. MAGUFULI ABAATISHI YEYE NI MTAALAM HEBU WAMUACHE AFANYE KAZI YAKE

    ReplyDelete
  4. Yako wapi aliyoyasimamia Mwaka 2011 yeye ndiye wa kwanza ameweka mabango kila kona.....

    ReplyDelete