24 February 2011

CHADEMA kufunika Mwanza leo

Na Daud Magesa, Mwanza

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeruhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya maandamano na mkutano wa hadhara leo
kupinga malipo ya Dowans ya sh bilioni 94 na kupanda kwa gharama za maisha.

CHADEMA wamepanga kufanya maandamano ya amani kushiniksza Serikali kutoilipa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans,maandamanop ambayo yataongozwa na viongozi wake wa Kitaifa na baadaye kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha jijini
hapa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari kuhusiana na mandaamano hayo ya CHADEMA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Bw. Simon Sirro alisema jeshi hilo halina pingamizi na maandamano hayo ukiwemo mkutano wa hadhara kama walivyoomba katika barua ya chama hicho ilimradi kisikiuke makubaliano na baada ya mkutano wafuasi wake watawanyike.

Alisema kuwa wao kama taasisi ya serikali yenye dhamana na ulinzi na usalama wa raia na mali zao, wamejipanga vizuri kuhakikisha maandamano hayo yanafanyika na kumalizika kwa amani na watatoa ulinzi wa hali ya juu.

"Kimsingi tulipokea barua ya CHADEMA wakitufahamisha kuwa watafanya maandamano ya amani kuishinikiza TANESCO kutoilipa kampuni ya Dowans, hatuna pingamizi isipokuwa wasikiuke makubaliano kama walivyoomba kwenye barua yao na hatutegemei iwe kinyume. Tutatoa ulinzi wa uhakika," alisema Bw. Sirro.

Alisema watajipanga katika maeneo ambako maandamano hayo yatapita na kuwataka wafuasi wa chama hicho kutawanyika baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Furahisha, kwani ipo tabia ya watu kufanya maandamano yasiyo halali, na kufanya hivyo itakuwa ni uvunjifu wa sheria.

Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Mkuu wa Chadema mkoa wa Mwanza, Bw. Willy Mushumbusi alisema maandamano hayo ni ya kuishikiza serikali kutoilipa kampuni ya Dowans ambayo ilirithi mkataba hewa wa kufua umeme wa dharura nchini.

Adha alisema mbali na hilo wataishinikiza serikali ipunguze bei ya nishati ya umeme kwani kupanga kwa bei ya nishati hiyo kumesababisha kupanda kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei nchini.

Bw. Mushumbusi alisema kuwa mbali na hayo pia watatumia maandamano hayo kuitaka serikali iagize uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha ufanyike upya kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa.

"Tunaandamana kwa mambo matatu, kwanza kuishinikiza serikali kutoilipa Dowans ni kampuni ya kitapeli na iliririthi mkaba hewa. Tunaitaka serikali kupunguza bei ya nishati ya umeme, imesababisha wananchi kuishi maisha magumu kutokana na gharama za maisha kuwa juu. Pia Tunataka uchagzi wa Meya wa Arusha urudiwe na kufanyika katika misingi ya kanunina taraibu" alisema Bw. Mushumbusi

Mandamano hayo ambayo yataongozwa na viongozi wa Kitaifa wa CHADEMA wakiwemmo mwenyekiti, Bw. Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dkt. willibrod na wabunge wa chama hicho, yataanzia ofisi ya CHADEMA, Buzuruga majira ya saa 7:00 mchana na kuishia katika viwanja vya Furahisha.

Kutoka Buzuruga maandamano hayo yatapita katika barabara ya Nyerere, Pamba, Kenyatta na Makongoro hadi uwanja wa Furahisha ambako viongozi wa kitaifa watahutubia wafuasi wao baada ya maandamano.

Akizungumzia maandamano hayo juzi, Bw. Mbowe alisema mateso wanayopata Watanzania yanasababishwa na viongozi walioko madarakani kukosa utashi wa kisiasa kuyakabili na kutolea mfano mfumuko wa bei unaosababisha bidhaa kupanda bei kila kukicha wakati uwezo wa mwananchi wa kawaida kununua bidhaa hizo ukipungua, lakini viongozi wakipita na kutamba kuwa uchumi umekua na kuimarika.

Watanzania hawahitaji uchumi unaokuwa kwenye makaratasi na takwimu za wataalamu. Kinachotakiwa ni ukuaji huo kuonekana katika maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida na hii inahusu uwezo wa kununua bidhaa na mahitaji muhimu. Uchumi utakuaje wakati mtu hana uhakika wa bei ya sukari dukani kwani inapanda kila siku licha kujengwa viwanda vingi vya sukari nchini kuliko kipindi kingine chochote?

"Mwaka 2005 wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, bei ya kilo moja ya sukari ilikuwa sh. 600. Lakini kiasi hicho kwa sasa kinauzwa kati ya sh. 1,700 hadi 2,000 ambayo ni karibia ongezeko la asilimia 150 ndani kipindi cha miaka sita tofauti na kipindi cha awamu ya tatu chini, Bw. Benjamin Mkapa ambapo bei ya bidhaa
ilidhibiti kwa karibu miaka yote kumi aliyokaa madarakani.

"Pamoja na sukari baadhi ya bidhaa zingine za mahitaji ya kila siku zilizopanda bei mara dufu na bei za zamani na mpya kwenye mabano ni pamoja na paketi moja ya kiberiti (sh. 20 hadi 50), kipande cha sabuni (sh. 100 hadi 350), pakiti moja ya chumvi (sh. 50 au 100 hadi sh. 200 au 300), kilo moja ya nyama ya ng'ombe (sh.
2,000 hadi 4,000 au 5,000). Hii ni mifano michache kwani orodha ni ndefu," alisema.

6 comments:

  1. na bei ya mafuta katika soko la dunia ilikuwaje na sasa ipo vipi? je bei hiyo ya mafuta imepanda kwa asilimia ngapi? inabidi watueleze wananchi kwa undani jinsi kupanda huku kwa gharama kuna uhusiano gani na bei bidhaa katika soko la dunia hasa mafuta ipoje. hama sivyo tutakuwa tunapoteza muda kwa maandamano kila siku na hakuna kinachobadilika. na hayo maandamano na kauli zinazotelewa katika mikutano ya hadhara hivi zinawafikia hao wahusika au ndiyo kupiga kelele tuuu. mwisho wa yote mambo yanaendelea kuwa vile vile?

    ReplyDelete
  2. Naungana na Wanachadema kufanya maandamano ya amani kudai au kuashiria hali ya maisha ya Watanzania. Ninakubali ya kwamba hali ya maisha katika nchi yetu ni ngumu kwa ujumla. Lakini ninapenda kujiuliza pia kama Watanzania wanazifahamu hali za nchi nyingine? Mara kwa mara watu wamekuwa wakizungumzia umaskini wetu lakini hawaoni umaskini wa Marekani ambao wapo wanatafuta riziki kwa taabu; hawaangalii Mexico, India: Ukifika leo jijini Frankfurt; Hamburg na hata mji mkuu Berlin utawakuta ombaomba wanaoitwa Obdachlose na wasio na kazi. Kupanda kwa bei ya mafuta si swala la Watanzania pekee yao leo Ujerumani lita moja ya petrol imefikia Euro 1,51 badala ya 1,30. Kweli kuna mambo ya kuwalaumu viongozi wasiotekeleza majukumu yao vema na pia sisi wananchi yapo majukumu yanayotupasa kuyatimiza. Nimepita katika mitaa mingi katika miji yetu, wananchi wale wale waliotengenezewa mitaro ya kupitisha maji ndio haohao wanatupa taka zao mitaroni na baada ya muda inaziba na hao hao wanaanza kulaumu Halmashari ya Mji.Huko milimani wanaharibu vianzo asili vya maji na baadaye maji kukosekana (Muheza)miti kukatwa ovyo bila kuwa na kata mti panda mti-
    Je ni kweli ya kwamba hayo yote ni mapungufu ya CCM na JK? Magufuli, Tibaijuka wanasakamwa sasa na baadhi ya watu kwa sababu wanatekeleza wajibu wao lo mbona ajabu? Watanzania wenzangu wengi wamekuwa katika hali ya kulaumulaumu tu, shule zikifunguliwa kwa wingi wanalaumu, zikipungua wanalalamika je tutafika? Yaliyo ya kweli kukosoa tufanye hivyo bila kuahidi ahadi ambazo ni vigumu kuzitekeleza kwa masaa lengo na liwe kuboresha maisha kila mmoja kwa majaliwa ya Mungu. Ustaarabu hauendewi shule ila ni kuzaliwa nao.

    ReplyDelete
  3. suluhisho mnalijua, tupeni nje CCM na kuweka chama cha upinzani(CHADEMA); naamini hata viwanja vya michezo na sehemu za wazi za kuchezea watoto wa shule na vingine; zitarudishwa kwa wananchi.

    ReplyDelete
  4. usitueleze habari za umaskini wa Marekani, Frankfurt; Hamburg na kwingineko, elewa swali hili kichwani mwako. ukitaka kufagia unaanzia mbele ya miguu yako kuleta takataka miguuni au unaanzia miguuni kupeleka takataka mbele yako?
    kama umepata jibu msemaji wa tatu wewe si mwana mapinduzi, ila wewe ni mapungufu.

    ReplyDelete
  5. Bila kufahamu hali ya nchi nyingine kiuchumi na kisiasa hata kijamii huwezi kuwa mwanamapinduzi. Kama ni hivyo basi watu wasingelikuwa wanasikliza taarifa za habari au kusoma magazeti. Kama mimi ninaishi Bariadi au Mwanaza, Dar ni lazima nijue matukio mbalimbali ya sehemu nyingine nchini kwa maendeleo yangu.Ndio maana naingia kwenye Blog MICHUZI,MTAA KWA MTAA, MZEE WA MATUKIO ili kuona kinachendelea nchini mwangu. Binadamu yoyote yule duniani hawezi kuishi bila mapungufu. Bila shaka mfano wa kufyagia ulioutoa mtoa maoni wa nne kama swali jibu unalo wewe mwenyewe. Mbona hukusema habari ya mitaro na vianzio vya maji umerukia ya Frankfurt tu? Nakutakia mema.

    ReplyDelete
  6. Umaskini wa kipato kwa wastani ni k iasi gani (sisi ni chini ya dola tena watu asilimia 37% tena kwa data za kupika najua tuko maskini wengi walio chini ya dola; angalia TZ kwa umaskini ni ya ngapi; usilete habari za mitaa michache ya ujerumnai au USA; ongelea kwa ujumla umaskini wetu ni sawa na wao (ambao thamani ya mlo wa mbwa tu ni zaidi mara mbili ya thamani mlo wa mtanzania. Jamani acheni ushanbiki ktk hili; maisha yamekaba tena kwa upumbafu wa viongozi wetu

    ReplyDelete