Na Jovither Kaijage, Ukerewe
MWENDESHA pikipiki mmoja ameuawa na wananchi katika wilaya ya Ukerewe, Mwanza baada ya kugongwa na baiskeli, katika ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja kati ya wawili waliokuwa wamepanda baiskeli hiyo.Mwendesha
pikipiki aliyeuawa kikatili ni Eric Elius (34) mkazi wa Kijiji cha Buhima wakati aliyekufa katika ajali hiyo ni Martha Kanyago (20) Mkazi wa Kijiji cha Chankamba, Ukerewe na mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Igombe, Ilemela jijini Mwanza.
Akithibitisha tukio hili Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Simon Sirro alisema limetokea juzi saa 12:00 jioni kati ya kijiji cha Igalla na Chankaba wilayani Ukerewe.
Alisema mwendesha baiskeli aliyetambuliwa kwa jina la Muoja Mabagara, mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Igalla ambaye ametoroka, alishindwa kuimudu kutokana na mwendo kasi katika mteremko, hali iliyosababisha ayumbe na kugonga pikipiki.
Katika ajali hiyo Martha aliyekuwa abiria wake, alipoteza maisha.
Kamanda Sirro alifafanua kuwa baada ya ajali hiyo kutokea, kundi la watu lilijitokeza na kumpiga kwa fimbo na mawe mwendesha pikipiki huyo, kisha wakamfunga mikono na kumchoma moto pamoja na pikipiki yake.
Kamanda huyo alisema tayari jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwapata waliohusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment