24 December 2010

CHADEMA yatoa masharti mgogoro wa mameya

Na Reuben Kagaruki

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa masharti ya kumaliza mgogoro ya uchaguzi wa mameya katika maeneo yote yenye utata vinginevyo kitaitisha maandamano ya amani nchi nzima ifikapo Januari 5, mwaka huu.Katika
masharti hayo, kimependekeza uitishwe mkutano wa majadiliano baina yake na viongozi wa juu wa serikali, ikiwezekana ahusike Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, viongozi wa TAMISEMI na kusitishwa kwa chaguzi za wenyeviti na mameya katika maeneo yenye utata.

Maeneo yenye utata yametajwa kuwa ni pamoja na Mwanza, Arusha, Hai, Kigoma Ujiji, ambako chama ghicho kimedai uchaguizi umevurugwa katika mazingira yanayoashiria kuwapo maelekezo kutoka ngazi za juu.

Barua ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa ya Desemba 22, mwaka huu ilieleza kwamba, iwapo madai hayo hayatatekelezwa hadi Januari 4, 20211 chama kitaitisha maandamano siku inayofuata bila kujali yana kibali cha polisi au la.

Masharti ya chama hicho ni pamoja na kutaka usifanyike  uchaguzi wowote wa mameya au wenyeviti wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Manispaa ya Arusha na Hai.

"Kama unavyojua, uchaguzi wa wenyeviti na mameya hao umevurugika kwa sababu ambazo zina utata na kwa vyovyote vile kuonesha dalili ya kuwa na maelekezo kutoka ngazi za juu, jambo ambalo limeleta utata mkubwa ikiwa ni pamoja na uvunjifu wa amani," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;

"CHADEMA tumejitaidi kutuliza wapenzi wetu hata baada ya wananchi kupigwa mabomu na polisi bila sababu," alisema Dkt. Slaa

Chama hicho kimesema polisi ni watuhumiwa katika matukio ya Arusha, hivyo kama hakutakuwa na maridhiano serikali itakuwa imewalazimisha kuchukua hatua ya kuandamana.

Pia kimetaka masharti yote yaliyotolewa Arusha yaendelee, yaani Mkurugenzi wa Manispaa ajiuzulu kwa ukiukwaji wa kanuni za halmashauri na kusimamia uchaguzi kinyume na taratibu, uongozi wa TAMISEMI uliingilia uchaguzi hasa Kigoma/Ujiji, hivyo wahusika wote wachukuliwe hatua.

Chama hicho kimeitaka serikali kumchukulia hatua OCD wa Arusha kwa kuingia na kumkamata mbunge ndani ya kikao halali kinyume na kanuni za uendeshaji wa halmashauri. Kwa mujibu wa barua hiyo, chama hicho kinamtaka OCD huyo ajiuzulu au aondolewe.

"CHADEMA sasa tumefikia mahali tumechoka na unyanyasaji, serikali ijue hivyo. Ni imani yetu kama serikali inataka haki itendeke, hatua stahiki ziwe zimechukuliwa kwa wahusika kabla ya terehe 4 januari, 2011," ilieleza barua hiyo.

Katika barua yake Dkt. Slaa alieleza kuwa chama chake kinaheshimu mazungumzo yake na Bw. Tendwa na yale ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Bw. Said Mwema.

"Kama tulivyokubaliana kati ya Dkt. Slaa na Bw. Tendwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaratibu mkutano huo na kuwajulisha wahusika juu ya malalamiko ya CHADEMA," ilieleza barua hiyo.

Alisema chama hicho kitaitisha mkutano wa waandishi wa habari kuomba wananchi wa Arusha watulie hadi watakapojulishwa hatua zaidi, iwapo serikali haitakuwa imechukua hatua.

10 comments:

  1. Chadema wananchi watanzania tupo nyuma yenu kwa ajili ya mapambano na utawala wa mafisadi wa CCM. Wao hawakuzaliwa wawe watawala na wengine watawaliwa! Nchi hii ni yetu sote siyo yao pekee yao. Mapambano lazima yaendelee mpaka ushindi upatikane. Tanzania itakuwa Ivory Cost kwa ajili ya uroho wa madaraka wa watu wa CCM. Ni nani asiyejua Chadema ina madiwani wengi Arusha? Hivi inawezekanaje CCM washinde ikiwa kura zitapigwa kwa uhalali? Wabunge wa CCM wapo wengi ndani ya bunge dunia ingeshangaa kama Anne Makinda asingepita hivyo hivyo lazima dunia ishangae kwanini mgombea wa CCM apite mahali ambapo kuna madiwani wengi wa Chadema. Jamani hii CCM inatupeleka pabaya Tanzania na huo ni mwanzo wa CCM kusambalatika kama wananza kutumia nguvu kuchukua madaraka ya halmashauri ndio maana tunaamini hata Kikwete alichakachua matokeo. Watanzania wameichoka CCM. Hata kama itanyaje. Dawa ni wao kuachana na ufisadi unaofanya maisha ya wengi yaendelee kuwa ya ufakala wa kutpwa. Na wao na watoto wao wakineepa. Tanzania ni yetu sote siyo ya kikundi cha wana CCM.

    ReplyDelete
  2. Ebwana umenena mtu mzima wasitufanye Watanzania ni mataahira hiyo amani wanayoisema haitakiwi tu mdomon ila ni kwa vitendo wasifikiri amani ya Tanzania inajengwa kwa mazoea bali kwa haki na matakwa ya wananchui yanaheshimiwa hivi wao wanapanda bangi wantegemea kuvuna mihogo waache upumbavu la sivyo mahakama za uhalifu za kimataifa zinawasubiri.

    ReplyDelete
  3. Ningependa kuona amani ikiendelea katika nchi yetu Tanzania, na si kutoweka kwa manufaa ya wachache,CCM lazima wakubali kila lenye mwanzo halikosi mwisho na hasa kwa sasa.Kwamtazamo wa kina wananchi wa Tanzania wamechoshwa na ukiritimba wa muda mrefu unaofanya na viongozi wa chama CCM.Waswahili wanasema wengi wape,sawa kusoma hatujui basi hata picha.Wingi wa madiwani wa chama cha CHADEMA mkoani Arusha, unatoa picha kamili ya nafasi ya umeya katika mkoa uwo.Chonde AMANI ndio rasimali kubwa tunayojivunia na kuna dalili zote zinazoashiria utokomeaji wake .TUSIPO ZIBA NYUFA TUTAJENGA UKUTA...........CCM someni alama za nyakati watu wameamka sasa kila sehemu mnataka kuchachua hata nafasi zisizo chakachuliwa .............

    ReplyDelete
  4. Mh.Dr.slaa,ukumbuke kuwa polisi niwa serikali ya CCM.Itakuwa ni vigumu sana serikali kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika uliowataja hapo juu.Chamsingi mwambie mungu aingilie kati suala hilo.Suala la maandamano lisahau hutopewa kibali cha maandamano kwa sababu ya ubabe wa CCM na serikali yake.

    ReplyDelete
  5. Kwa nyakati hii iliyopo sasa hivi ni kuingia barabarani tu watapiga wangapi, wataua wangapi, na hapo ndipo dunia itajua mahali CCM ilipotufikisha. Tumechoka na kiburi cha CCM, Kama FFU NA POLICE watafanya watakavyoagizwa basi na wafanye lakini tunaomba maandamano ya amani tueleza dunia kilio chetu kama hawataki kutusaidia sisi masikini.

    Wanasema tufanye kazi, kazi gani? Wao wanafikiri wamachinga kukimbaa kimbia na maduka mkononi ni wao wamependa, na ninani amewafikisha hapo. Mtu unamkuta amesoma vizuri anaelimu nzuri aituie wapi kila kona ni wazee hawataki kustaafishwa na ndio maana TANESCO INASUMBUA HII NI KASUMBA YA HAO WAZEE. WAACHE VIJANA WENYE TECHNOLOGY YA KISASA WAFANYEKAZI. HAO WAZEE WALISHAZOEA MGAO. Na kama sio hivyo basi kutakuwa kuna mtu anataka kuuza genereta zake hilo la umeme ni biashara.

    Serikali lazima mjiulize haki ya mtanzania ipo wapi? Akiwa na lengo lolote mnamzuia ni kwa nini? Yaani maandamano ya amani hata sikumoja hayazuiliwi kwa sababu lazima yatakuwa na ujumbe fulani, na ule ujumbe lazima utafutiwe ufumbuzi kama inawezekana. Mbona nchi zilizoendelea maandamano kwao ni kama kawaida na wanapewa ulinzi mkali mbele na nyuma.

    ReplyDelete
  6. Nyie Chadema wahuni tu hamna lolote, kitu kiko wazi mnachoshindwa kufuata taratibu za kisheria ni nini? Nafikiri mmelewa sifa na hii inaonyesha hata nyie mkipata madaraka hamtataka kufuata sheria, mnataka muingie mitaani ili watu waibiwe mali zao waharibiwe mali zao na wahuni wenu waliokimbia kazi za maana vijijini na kuja mjini kuwaibia watu usiku mchana wameshika pini wanauza?

    Mkiendelea na huo upopulist wenu watu wenye akili timamu watawachoka. Kama mko makini na ushahidi mnao kwanini hamuendi mahakamani? Mbona Mtikila yeye asiporidhishwa na kitu anakwenda mahakamani nyie kinawashinda au kuwaogopesha nini? Yaani naona hapa ni suala la maslahi zaidi na si kutaka kuleta mabadiliko, haya sasa mkiingia mtaani huyo Meya ndio atang'oka kwa maandamano? Hovyoo!

    ReplyDelete
  7. Wewe ulieto hiyo comment hapo juu, ni mnafiki, kama unataka kuburuzwa uburuzwe wewe sio watanzania. Kwani huyo Mtikala amefanikiwa mangapi au CCM wanamburuza tu. Na mahakama unayo sema ni ipi hii ya CCM. Sasa kama nyinyi wa CCM ni vidume mruhusu katiba mpya tuone hali ya hewa.

    Kama mahakama inatenda haki kwa nini wafungwa wanakataa kushuka kwenye karandinga, wanasusa kula, jiuliza. Tunataka maandamano nchi nzima hata wiki nzima ili dunia ijue vizuri kilio chetu. Na wewe na ufisadi wako ndio uende huko mahakamani.

    ReplyDelete
  8. njia pekee ni suluhisho na malumbano kwa siasa
    za Afrika zimetawaliwa na uroho wa madaraka kwa masilahi binafsi ,na si kwa maslahi ya umma.Angalia Raila alichochea kila aina ya maandamano na wakenya wengi walipoteza mwelekeo na wengi walikufa wakidai haki.lakini baada kiongozi huyo kupewa uwaziri akawasahau na kuanza kuwakejeli kwa kuwataka wasahau yaliyopita.Tuangalie tunandama kwa maslahi ya taifa au ya Mtu au KIONGOZI fulani.

    ReplyDelete
  9. Wewe uliyemwambia mnafiki wewe mnafiki zaidi wacha kila mtu atoe maoni yake

    ReplyDelete
  10. MAREHEMU JULIUS KAMBARAGE NYERER ALISEMA HUKO IKULU KUNA NINI HATA WATU WANAPAGOMBEA HIVYO? WATANZANIA CHUNGENI HILI MSITUMIKE HOVYO. HAPA KWENYE MAONI KUNA MAMLUKI WA VYAMA KWA HIYO LINALOANDIKWA HAPA SIO MAONI YA MAJORITY. WACHAGA NI MAFIA.HICHO CHAMA CHA CHADEMA KIMEZUNGUKWA NA WAFANYA BIASHARA KAMA CCM. HAMNA JIPYA HUMO. CHAGUENI VIONGOZI WANAOISHI KATIKA MAISHA YA KAWWIDA MTAPATA MAENDELEO.OLE WENU

    ReplyDelete