Na Yusuph Mussa, Lushoto
IMAMU wa mwalimu wa dini wa Kijiji cha Mkuzi, Kata ya Kwai wilayani Lushoto Bw. Amir Kijangwa (47) amefikishwa mahakamani akituhumiwa kuiba Nyaya za umeme zenye uzito wa kilo 19 huku zikiwa na thamani ya sh. 285,000.Akisoma
mashtaka hayo mwishoni mwa wiki kwenye Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, Mwendesha Mashtaka, Bw. Evarist Mwamengo alisema Desemba 18, mwaka huu saa moja asubuhi Bw. Kijangwa alikamatwa na kiroba cha nyaya hizo nyumbani kwake.
Hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, Bw. Yona Wilson alitoa dhamana kwa mtuhumiwa huyo, mara baada ya Bw. Kijangwa kukataa kosa lake na kesi inatarajiwa kutajwa tena Januari 4, mwakani.
Wakatu huo huo, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Lushoto Bw. Said Mhando amesema wimbi la wizi wa nyaya za umeme limezidi kuongezeka baada ya watu wasiofahamika kuiba nyaya usiku wa kuamkia Desemba 20, mwaka huu.
Bw. Mhando alisema nyaya hizo zenye urefu wa mita 800 na thamani ya sh. milioni mbili ni muendelezo wa matukio hayo yaliyoanza Septemba, mwaka huu na kuwa hadi sasa yameshatokea matukio saba yaliyosababisha wikiwa nyaya zenye urefu wa mita 2,740 zenye thamani ya sh. milioni 6.8.
"Wananchi lazima waelewe TANESCO au Jeshi la Polisi hawana uwezo wa kulinda miundombinu ya umeme, na jukumu hilo ni la wananchi wenyewe kwa kuwa matokeo yake ni kukosekana huduma ya umeme.
"Lakini pia shirika linapata hasara kwa kuweka miundombinu mipya maeneo ya wizi na kuacha kuwawekea wananchi wengine wapya, lakini pia wafanyakazi wanaacha kufanya kazi mpya na kuziba mapengo ya wizi, matokeo wananchi wanalalamikia huduma inachelewa kwao," alisema Bw. Mhando.
No comments:
Post a Comment