Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya soka ya AFC Leopards ya Kenya, inatarajia kutua nchini leo ikiwa na wachezaji 20, huku sita wakiwa wa kimataifa kwa ajili ya kuumana na Simba katika mchezo utakaopigwa keshokutwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.Mbali na
mchezo huo, AFC Leopards pia itaumana na Yanga Jumapili kwenye uwanja huo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa michezo hiyo, George Wakuganda alisema timu hiyo itatua nchini ikiwa na kikosi kamili kwa ajili ya michezo hiyo.
"AFC LeopardS itakuja na wachezaji 20, sita ni wa kulipwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ambao ni Itugu Indemu na Kanyanga Mangili, Abdlallah Koki na William Rashidy kutoka Liberia, Ekene Eneka na Ari Jento kutoka Nigeria," alisema Wakuganda.
Alisema mbali na wachezaji hao pia ina wachezaji wengine watano kutoka timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars', ambao ni Paul Were, Martine Imbala, Laurance Wero, Bernad Mangori na Bryan Mwakyoro.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Clifold Ndimbo akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, alisema yanaendelea vizuri ila wachezaji Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Patrick Ochan bado hawajafika nchini kutokana na sababu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment