Na Tumaini Makene
SHIRIKA la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) limetoa ripoti na kutahadharisha kuwa idadi ya watu mijini barani Afrika inatarajiwa kuongezeka mara tatu miaka 40, hivyo kuwataka
wapanga mipango na watunga sera kutilia maanani suala la makazi hasa kwa watu maskini, kuepuka makazi holela.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kitengo cha habari cha UN-HABITAT jijini Nairobi, Ripoti hiyo iliyopewa jina la 'Hali ya Miji ya Afrika 2010; Utawala, Tofauti ya usawa na Soko la Ardhi Mijini' ilizinduliwa juzi jioni, Mjini Bamako, Mali katika mkutano wa tatu wa mawaziri wanaohusika na masuala ya nyumba na maendeleo ya makazi (AMCHUD III).
Imeelezwa katika ripoti hiyo kuwa kote barani Afrika, watu takribani milioni 24 waliokuwa wakiishi katika makazi duni, maisha yao yameboreka katika muongo mmoja uliopita.
Hata hivyo, imezidi kufafanuliwa kuwa pamoja na miji ya nchi za Kaskazini mwa Afrika kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya watu wanaoishi katika makazi duni kutoka asilimia 20 mpaka 13, katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ilipungua kwa asilimia 5 tu, (takribani watu milioni 17).
Ripoti hiyo imeeleza kuwa Bara la Afrika litaendelea kusumbuliwa na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi, mathalani kutotabirika kwa hali ya hewa, pamoja na kuwa bara hilo linachangia pungufu ya asilimia 5 katika uharibifu wa hewa duniani.
Imetoa mifano halisi kama vile mvua kubwa iliyoonesha hivi karibuni nchini Burkina Faso ambapo takribani watu 150, 000 waliachwa bila makazi, huku pia sehemu zingine za Afrika, zikikabiliwa na ukame wa muda mrefu, ulioambatana na njaa, hivyo kusababisha uhamaji wa watu kutoka vijijini kukimbilia mijini, unaosababisha ongezeko la watu mijini.
“Ukuaji wa miji utaendelea kuwepo, ndani ya miongo michache ijayo, sehemu kubwa ya Afrika itakuwa ni miji...changamoto sasa ni wadau wote kuungana pamoja kuhakikisha ufanisi katika usimamizi wa ukuaji huu wa kasi. Kunahitajika sera murua kuleta manufaa na kuliokoa taifa katika umaskini," amenukuliwa akisema Mkurugenzi Mtendaji wa UN-HABITAT, Bw. Joan Clos.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, ripoti ya UN-HABITAT pia imeangazia ugumu uliopo katika kupata idadi kamili ya namba ya watu wanaoishi katika makazi duni katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara;
Nadhani huu ndio muda muafaka kwa Tanzania kujipanga. Swala la vijana wengi kuhamia mjini ni jambo ambalo serikali inao uwezo mkubwa wa kuudhibiti.
ReplyDeleteKila mtu anajua kwamba, kukimbilia mijini kwa vijana kunaambatana na kusaka ajira. Lakini ni kwa nini waje mijini?
Ukiwauliza hawa, hakuna hata mmoja ambaye atakwambia kazi anayotafuta ni ya ukarani au meneja, sanasana watakwambia kazi yoyote, " hata kufagiafagia, mjomba!" ndiyo kauli ya wengi.
Ukweli ni kwamba wako tayari kufanya kazi yoyote ile ilimradi mwisho wa siku ina malipo.
Hawa hawachagui kazi, wala hakuna kazi maalum waliyoifuata mjini, ila ni kwamba wameikimbia tu dhiki kule kijijini; kwa nini? Kwa sababu wameamini kwamba serikali imewasahau!
Basi kwa nini serikali isiwakumbuke sasa? Kwa CCM, huu ni wakati tete, kuna haja kubwa kuwarudia watu kule vijijini ambako ndiko kuliko na mashabiki wakubwa wa chama ili huko mbele na wao wasije wakageukia vyama vingine.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba hawa wanaposema wanatafuta ajira ya namna yoyote, wanataka kujikimu kwa pesa kwa kufanya kazi, hata kile kilimo wanachofanya huko kijijini, kama kingekuwa kinalipa, kwao ni ajira.
Nenda kule Mbuyuni, Ilula, na sehemu kubwa mkoani Iringa na Morogoro, kandokando ya barabara ya Morogoro, utaona jinsi vijana wanavyochangamkia ukulima wa vitunguu na nyanya kwa kumwagilia. Wako kule, wala hawana habari na mjini, wakija mjini, ni kutumia tu!
Hebu tujifunze kitu hapa.
Ninaamini baraza jipya la mawaziri, wengi wao wakiwa ni wenye upeo wa kupambanua mambo, kwa kushirikiana, waliangalie hili kwa kina. Ajira zianzie kule kijijini, siyo kwa kupeleka tu matrekta, bali kwa kuwatafutia wakulima hawa masoko yenye uhakika, ambayo Mkulima atakuwa na uhakika wa kujipangia mwenyewe malengo hata ya miaka mitatu minne mbele, akiwa na uhakika wa kuuza BILA KUCHELEWA KULIPWA, kila atakachopeleka sokoni. Matumizi ya pesa ya serikali katika bajeti yake, hebu na yaelekezwe pia kijijini, vijana wafurahie kazi zao kulekule badala ya kuja mijini na kuishia kujiingiza kuwa vibaka na wabwia unga.
Mama Tiba, tule tunyumba twa bei poa tunafaa hata kule chijijini jamani, leo si upo hapahapa, hebu tuendeleze kale ka- idea ka HABITAT.
Kazi pia Mh. Maghembe, Mathayo, na karibu baraza zima la mawaziri. Kuna kila sababu ya kupunguza msongamano wa watu mijini kwani kwa Tanzania hakuna sababu. Fursa za kujiajiri ni nyingi sana vijijini na wilayani, ukichukulia kwamba mbali na kilimo, uvuvi, migodi, ufugaji n.k., ni pesa ya uhakika kabisa kwa vijana walio wengi.
KARIBU BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI, NGOMA HIYOO, NA TUICHEZE Tanzania iondokane na umasikini usio na uhalali wowote kuwepo. Ahsanteni.