18 November 2010

Kikwete awateua Nahodha, Meghji wabunge.

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete ameteua wanasiasa watatu kutoka Zanzibar kuwa wabunge, ikiwa ni hatua ya kujaza nafasi 10 alizopewa kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.

Uteuzi ambao umefanyika siku moja baada ya kuteuliwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na siku chache kabla ya kuteuliwa kwa Baraza la Mawaziri, ni ishara kuwa wateule hao watakuwamo kwenye baraza hilo linalotarajiwa kuteuliwa kuanzia kesho.

Walioteuliwa ni aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kipindi kilichopiota, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa na aliyekuwa Waziri wa Fedha katika baraza la kwanza la Rais Kikwete, Bi. Zakia Hamdan Meghji.

Bi. Meghji aliondolewa katika wadhifa huo baada ya Rais Kikwete kuvunja baraza lake la mawaziri kutokana na kujizulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa baada ya kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richnond, akidaiwa kushinikiza kampuni hiyo ipewe zabuni, licha ya kutokuwa na uweoz wa kufanya hivyo.

Kabla ya hatua hiyo, Bi. Meghij alijikuta katika wakati mgumu baada ya kutoa majibu yenye kukang'anya kwa wakaguzi kuhusu malipo ya sh. bilioni 40 za Benki Kuu ya Tanzania kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kwa kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, pale alisema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya usalama wa nchi, na siku chache baadaye akafuta majibu yake akisema Gavana wa Benki alikuwa amemdanganya.

Akiwa Waziri wa Fedha mwaka 2007/08, Bi. Meghji alitoa bajeti ya kihistoria iliyopingwa na wananchi na vyama vya upinzani, hivyo kuwalazimu mawaziri kuzunguka mikoani kutetea uzuri wake.

Kwa upande wa Bw. Nahodha, akiwa amedumu madarakani kwa miaka 10 chini ya Rais Aman Abeid Karume, alikuwa akitarajiwa kuteuliwa katika serikali ya sasa ya Rais Ali Mohamed Shein, lakini haikuwa hivyo, kwa kile wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema alikuwa kipingamizi cha serikali ya umoja wa Kitaifa iliyoasisiwa na bosi wake na hatimaye kuundwa Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, jana, ilisema kuwa Rais Kikwete atateua wabunge saba waliosalia siku zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete ameshawasilisha majina ya wateule hao kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Anne Semamba Makinda kwa ajili ya hatua zipasazo.

3 comments:

  1. HAKUNA UDINI WALA NINI,NI UTEUZI TU

    ReplyDelete
  2. Kweli serikali hii Makini. Vyeo havipendelei uislamu. Hongera JK

    ReplyDelete
  3. Lah haula! 'Kibibi' kidanganyifu hako!Kalisha toa-za-kutoa kuhusu pesa za EPA. Eti bilion 40 zilitumika kwenye usalama wa Taifa wakati sivyo.Jamani, hivi ni lazima sura hizi hizi tu? Hata kama si Adilifu? Namshangaa JK....na uteuzi wake!Vijana wapo 'mzee',watumie wakufanyie mambo ya kufaa.Achana na vikongwe.

    ReplyDelete