01 November 2010

Makada CCM wajeruhiwa Geita.

Na Faida Muyomba, Geita

MAKADA wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nkome, Jimbo la Geita, wamejeruhiwa vibaya kwa kukatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa
ni wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).

Akithibitisha tukio hilo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Simon Sirro alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 30 saa 3 usiku.

Alisema kuwa watu wanaosadikiwa kuwa ni wa CUF kuwakata mapanga katibu wa Umoja wa Vijana wa kata ya Nkome, Bw. Timoth Msomi na mwenzake Costantine Kurwichumila ambaye ni katibu wa tawi hilo.

Kamanda Sirro alisema kuwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea na ambapo mkuu wa polisi wilayani Geita alikuwa eneo la tukio hilo kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.

Katibu wa CCM Kata ya Nkome, Bw. Furaha Bwire ambaye alikuwa eneo la tukio alisema kuwa wavamizi hao walimkaba katibu wake huyo wakati akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake na kumkata kwa panga vidole vyake viwili vya mkono wa kulia.

"Walimkata vidole vya mkono wa kulia na wakati tunaelekea kituo cha afya ili akapate matibabu tukiwa njiani tulikutana na kundi jingine tena likiwa na mawe na mapanga ambapo walimvama Katibu wa tawi la Nkome, Bw. Costantine na kumjeruhi kwa panga kichwani, ndipo tulitoa taarifa kituo cha polisi," lisema Bw. Bwire.

Alisema polisi walipofika katika eneo hilo walilazimika kufyatua risasi kadhaa hewani ili kuwatawanya wafuasi hao na majeruhi walikimbizwa katika kituo cha afya cha Nkome kwa matibabu.

Wakati huo huo, wananchi wa Kata ya Buselesele, jimbo la Chato, wameshindwa kuwachagua wagombea udiwani katika kata hiyo baada ya karatasi za kupigia kura kukosewa.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chato, Bi. Hamida
Kwikwenda, alisema kuwa sababu iliyosababisha kuahirishwa kwa upigaji kura za udiwani zilitokana na kuwepo kwa majina mawili badala ya matatu katika karatasi za kupigia
kura.

"Katika kata hiyo, watachagua wagombea ubunge na urais pekee ya udiwani itafanyika baadaye kwani kitabu cha majina ya udiwani kilikosewa, kilikuwa na picha mbili za wagombea udiwani badala ya tatu," alisema.

No comments:

Post a Comment