28 January 2013
Njama za kumng'oa meya Bukoba zagonga mwamba
Na Livinus Feruzi
Bukoba.
KITENDAWILI cha madiwani kumi wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba akiwemo Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini Balozi Khamis Kagasheki cha kutaka kumg'oa Meya wa manispaa hiyo Dkt. Anatory Amani katika wadhifa wake kimeshindwa kuteguliwa, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa,Bw.Philip Mangula kuwataka viongozi hao kufuata taratibu za chama kabla ya kumng'oa.
Kitendawili hicho kimeshindwa kuteguliwa kufuatia ziara ya siku tatu ya makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Taifa Bw. Philip Mangula kutoa agizo la kutaka madiwani hao kufuata kanuni na taratibu za chama kabla ya kumg'oa.
Kwa miezi kadhaa sasa umeibuka mgogoro kati ya meya wa manispaa ya Bukoba na mbunge wa jimbo la Bukoba mjini Balozi Kagasheki baada ya kutofautiana juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na halmashauri hiyo chini ya meya, ambapo mbunge huyo anapinga baadhi ya miradi kwa madai kwamba haiko wazi.
Kufuatia mgogoro huo madiwani hao waliandaa waraka na kisha kuusani wakimtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura cha baraza la madiwani ili kumwondoa meya katika nafasi yake .
Akizungumza na waandishi wa habari katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Bw. Hamimu Omary alisema baada ya makamu huyo mwenyekiti kufika mkoani hapa na kufanya mikutano mbalimbali ya ndani, aliagiza madiwani kufuata kanuni na taratibu za kumng'oa meya
huyo.
Kwa mujibu wa katibu huyo Bw. Mangula alisema hana tatizo na hoja ya kumng'oa meya,lakini katiba, taratibu na kanuni za chama zinatakiwa kufuatwa kwa maslahi ya chama.
"Makamu mwenyekiti alichosisitiza ni kufuata kanuni na taratibu kwani chama kinaendeshwa kwa mujibu wa katiba, kanuni na sheria... alisisitiza hoja hiyo kuletwa kwa kufuata kanuni ili kushughulikiwa kichama kwanza," alisema Bw. Omary
Kuhusu taarifa za baadhi ya madiwani kudaiwa kutaka kurejesha kadi baada ya agizo la Mangula, Mwenezi huyo alisema katika vikao alivyoudhuria hakusikia watu hao wakitaka kurejesha kadi,"unajua hata mimi taarifa hizi nimezisikia kama nyie mlivyozisikia,"
aliongeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment