24 July 2012

Wanunuzi wadogo walivyosaidia kuinua kipato cha wakulima wa pareto nchini


Na Rashid Mkwinda

MKAKATI wa kumkomboa mkulima kunufaika na kilimo kwa kujikita na kilimo cha kisasa utasaidia kupunguza umaskini.

Pia imepania kukuza uchumi na kusaidia ongezeko la kipato kwa wakulima kwa nia ya kufuta umaskini kuegemea katika kilimo cha kibiashara hatimaye kuelekeza nguvu kwenye sekta ya viwanda inayohudumia kilimo.

Nguvu hiyo imeelekezwa zaidi kwa wadau wa kilimo kwa ushirikishwaji ili kukuza ushindani wenye tija na kipato kwa wakulima  wa Tanzania ambao hutegemea uzalishaji wao wa mazao ya biashara katika soko la dunia la utandawazi.

Mkakati huu unaibua dhana ya uwekezaji katika sekta ya kilimo hususani kwa mazao ya kibiashara ambayo mara kadhaa yamekuwa yakikosa soko la uhakika na hivyo kusababisha wakulima wa mazao ya biashara kukata tamaa ya kulima mazao hayo kwa hofu ya kukosa soko.

Katika kauli yake Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa Tamko la Kilimo Kwanza lenye azma maalumu ya kuongeza kasi ya kuleta Mapinduzi ya kilimo nchini, anasema kuwa utekelezaji wa mkakati huu utakuwa mhimili muhimu kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea  mwaka 2025.

Anabainisha kuwa kwa kutumia fursa zilizopo, mafanikio katika kuleta maendeleo ya kiuchumi yataweka msukumo zaidi  kufanikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Pareto ni moja ya mazao ya biashara nchini ambalo hulimwa ukanda wa juu kuanzia mita 1900 kutoka usawa wa bahari ambalo huhitaji mvua kati ya milimita 1800 na zaidi kwa mwaka ambapo kadri inavyopanda juu na ongezeko la mvua nyingi.

Ipo mikoa michache iliyopo katika ukanda wa juu unaolima pareto nchini ikiwemo mkoa wa Mbeya katika maeneo ya Ileje, Mbeya na Rungwe, Iringa katika wilaya ya Kilolo, Njombe katika wilaya ya Makete na Mikoa ya Arusha na Manyara.

Zao la pareto linajumuisha aina ya maua yenye sumu ndani yake ambayo yakichujwa kitaalamu na kutengenezwa dawa husaidia kuzuia wadudu waharibifu kama vile kunguni, chawa, inzi, viroboto na wengine wa aina hiyo ambapo pia ikitumiwa kwa kufuata maelekezo haina madhara kwa binadamu.

Thamani halisi ya pareto inatokana na  kiwango cha sumu(Pyrethrins) iliyoko ndani yake ambapo zao hilo huzalishwa kwa wingi katika mikoa ya nyanda za juu kusini ya mikoa ya Mbeya na Iringa na kiasi kidogo kinachozalishwa kuzalishwa kanda ya kaskazini katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Aidha zao hilo la biashara limekuwa likiingia dosari na kukatisha tamaa wakulima kutokana na aina na mfumo wa ununuzi wa zao hilo ambalo kimsingi ni tofauti na mazao ya chakula ambayo asilimia kubwa ya soko lake linapatikana miongoni mwa wananchi waliopo karibu na eneo linalolimwa zao husika.

Thamani yake iko katika maua yenye sumu ambapo maandalizi yake ya kilimo sanjari na utunzaji wake, palizi, uchumaji wa maua ni hatua ambazo zinalifanya zao hilo kuongezeka thamani yake na kumpatia tija na kipato cha kutosha mkulima.

Msisitizo wa uthamini wa zao hili ni kuliwekea mazingira bora zao hilo ambapo maua yanatakiwa  kujazwa kwenye magunia yenye ujazo wa kilo 30 huku upakiaji na usafirishaji wake ukizingatia muda na wakati wa kuchuma maua hayo shambani na kutakiwa kusafirishwa kupelekwa kiwandani kwa muda usiozidi siku saba.

Bw.Bona Mboma (63) mkulima wa kijiji cha Ilembo wilaya ya Mbeya anaelezea athari itokanayo na kukosekana kwa soko la uhakika na wanunuzi wasio waaminifu ambapo kwa mtazamo wake ni kwamba soko huria limeibua changamoto kwa makampuni mengi kujitokeza na kushindana katika bei.

Bw. Mboma anasema kuwa awali alikuwa analima eneo dogo katika shamba ambalo hata hivyo lilikuwa na mazao mengine kama vile ufuta, viazi na ulezi na kwamba hivi sasa anamudu kulima ekari mbili anazoweza kutunza na kupata kati ya kilo 800 hadi 1000 kwa uwiano wa kila hekari moja kuvuna kati kilo 400 hadi 500.

Kulingana na taratibu za utunzaji wa zao la pareto, mkulima akilima na kutunza vizuri anaweza kujipatia kilo 500 ambapo kwa utunzaji hafifu anaweza kupata kilo 200 hadi 300 na kuchuma kila baada ya wiki mbili.

"Ushindani wa makampuni kwetu una manufaa, ukiendelea tutanufaika zaidi, tulianza kukata tamaa kulima pareto baada ya kuona tunadhulumiwa malipo yetu mara nyingine tunakopwa tunalipwa malipo ya mwanzo malipo ya pili hakuna," anasema Bw.Mboma.

Anasema, ameanza kulima pareto mwaka 1974 ambapo kwa wakati huo alimudu kujenga nyumba, kuoa na hata kusomesha watoto na kwamba amekuwa mkulima tangu akiwa kijana ambapo hadi sasa ana jumla ya watoto sita  ambao wote amewasomesha hadi ngazi ya chuo baadhi yao wakiwa chuo cha Ualimu na mwingine chuo cha Kilimo.

Naye Bi.Yonas Anania (65) mkulima wa Ilembo anasema kuwa ana uwezo wa kulima ekari moja na nusu ambazo anamudu kupata hadi kilo 600 hadi 750 zilizotunzwa vizuri na kwamba anajivunia kulima pareto kwa kuwa ndiyo pekee ambayo ni mkombozi wa maisha yake baada ya kupatikana wanunuzi wengi.

"Hivi sasa tuna uhakika wa soko, tukilima tunaweza kuuza, wanunuzi wanashindana kununua pareto kwa bei ya nzuri mwaka jana tulikuwa tunauza kilo moja sh. 1,200 sasa hivi tunauza kilo moja sh.2,300 tunashukuru ujio wa makampuni ya ushindani yametusaidia kujikwamua kiuchumi,"anasema Bi Anania.

Wakulima hawa ni baadhi ya wakulima wa maeneo mbalimbali ambao awali walianza kukata tamaa kutokana na kuwepo kwa ukiritimba wa ununuzi wa zao la pareto hali ambayo wanadai kuwa ilisababisha kunyonywa na kupunjwa malipo yao ya pili ambapo kutokana na msimamo mpya wa serikali kuamua kutoa leseni ya ununuzi wa pareto kwa makampuni mengi wameanza kuona faida ya kilimo hicho.

Bw.Leo Bwana ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanunuzi Wadogo wa Pareto nchini ambaye anawakilisha makampuni manne yaliyopata leseni ya ununuzi wa zao hilo katika mikoa ya Arusha, Iringa, Mbeya, Manyara na Njombe ambayo ni Tarkis Tanzania Ltd, Kati General Enterprises, Tabeco International na Actro General Business.

Anasema kuwa makampuni hayo yanaongozwa na wakurugenzi ambao ni Bw.Leo anayeongoza kampuni ya Tarkis, Bw.Ipyana Mwalukasa anayeongoza kampuni ya Kati, Tabeco International inayoongozwa na Bw.Simon Byanyuma na Bw.Saxon Luhanjo anayeongoza kampuni Actro General General Business.

Bw.Leo anasema kuwa awali makampuni yao yalipata leseni Oktoba 2011 katika kipindi cha mwishoni mwa msimu na kutumia kwa takribani miezi mitatu kabla msimu haujamalizika ambapo hata hivyo walifanikiwa kununua jumla ya tani 400 na kufanikiwa kuongeza pato la serikali kwa kuliingizia fedha za kutosha kwa msimu huo.

Anasema kuwa katika msimu huo bei elekezi ya serikali ilikuwa sh. 1,700  ambapo makampuni hayo kwa kuthamini mchango wa wakulima na kukifanya kilimo cha pareto kuwa endelevu walinunua pareto kwa bei ya sh.2000 ambayo iliwahamasisha wakulima kurejea kwa kasi katika kilimo hicho baada ya kuona thamani yake.

Hata hivyo Bw.Leo anasema kuwa ongezeko hilo la bei ya pareto limeanza kuwafanya baadhi ya wakulima kutozingatia utunzaji wa zao hilo ambapo baadhi yao wamekuwa wakivuna pareto zaidi ya mara mbili kwa wiki na kusababisha kukosekana kwa pareto yenye ubora katika soko la kimataifa.

"Tulipata maua mengi yasiyo na sumu na hivyo kusababisha tuingie hasara, hii ilitokana na wakulima kuanika pareto chini na kukutana na unyevunyevu na mchanga na kukosekana ubora wa zao hilo," anasema Bw. Eden Katininda mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Kati General Enterprises iliyopo jijini Mbeya.

Bw.Katininda anasema kuwa ili kuweka ubora wa zao hilo wameweka mkakati wa kushirikiana na serikali za Halmashauri za vijiji na wilaya kupitia maofisa ugani ili kuweka mpango endelevu wa kusaidia kuboresha kilimo cha pareto kwa wakulima.

Anafafanua kwa kuwa zao hilo ni miongoni mwa mazao yanaloliingizia pato Taifa wakulima wanaokiuka taratibu za uandaaji, utunzaji na uuzaji mfuko wa Bodi ya Pareto usimamie na ikiwezekana wanaokiuka wachukuliwe hatua za kisheria ili kujenga nidhamu ya uthamini wa zao hilo.

Akizungumzia ushiriki wao na manufaa ya wakulima katika kutunisha mfuko wa uendelezaji wa zao la  Pareto nchini  Mwenyekiti wa Vikundi vya Wanunuzi wadogo Bw.Bwana anasema kuwa kila kampuni inayonunua pareto kwa mkulima inachangia asilimia 6 ikiwa ni asilimia 3 anayochangiwa mkulima na asilimia 3 ya Bodi kwa ajili ya mbegu.

Anasema kuwa wanawachangia wakulima badala ya kujichangia wenyewe kama ilivyo katika utaratibu wa kawaida ili kutoa hamasa waendelee kuzalisha bila kukata tamaa na hata kukatwa katika bei elekezi ambayo kwa sasa imefikia kiasi cha sh. 2000 hadi 2200 ambapo makampuni yananunua hadi sh.2300 ili kuwasaidia wakulima.

Kuhusu kiwango cha uzalishaji wa zao hilo Bw. Bwana anasema kuwa kiwango kinachozalishwa hakilingani na mahitaji katika soko la kimataifa na kwamba iwapo wakulima wanaweza kuzalisha hadi tani 10,000 kwa mwaka lipo soko la uhakika katika nchi za Marekani, nchi za Bara la Asia na Rwanda.

Anasema kuwa matarajio kwa msimu huu wa kilimo ni kukusanya na kusafirisha zaidi ya tani 20,000  ambapo kupitia umoja wao wa wanunuzi wadogo anaamini tatizo la ununuzi na kupunjwa bei kwa wakulima kutatoweka hivyo wakulima waongeze uzalishaji wakaribiane na ununuzi.


No comments:

Post a Comment