31 July 2012
Na Charles Mwakipesile, Mbeya
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo, amesema chanzo cha migogoro na migomo katika vyuo vikuu nchini ni Wenyeviti wa Mitaa na vijiji kupitisha fomu za watoto wa vigogo ili kuomba mikopo na kuwaacha watoto wanaotoka katika familia zisizojiweza kukosa mikopo hiyo.
Bw. Mulugo aliyasema hayo juzi katika hafla ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Watoto Yatima cha Kanisa la Moravian nchini, Jimbo la Kusini Magharibi, Ushirika wa Itili, jijini Mbeya.
Alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, imejipanga kusomesha watoto yatima na wenye wazazi lakini hawana uwezo bila matatizo yoyote lakini jitihada hizo zinakwamishwa na viongozi wa mitaa pamoja na wale wa vijiji.
Aliongeza kuwa, viongozi hao ndio wenye dhamana ya kupitisha fomu za kuomba mikopo ya wanafunzi baada ya kupewa rushwa na kuwaacha watoto ambao ndio walengwa.
“Ufisafi huu unasababisha watoto yatima kukosa mikopo na kupewa watoto ambao wazazi wao wana uwezo tena waliosoma katika shule za gharama kubwa hivyo kuwa chanzo cha migogoro, maandamano vyuoni na kuvuruga amani ya nchi iliyodumu tangu uhuru.
“Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine, tumejipanga kuhakikisha tunasomesha watoto yatima na wale ambao familia zao hazijiwezi ili wapate elimu,” alisema.
Alipongeza jitihada za ushirika huo na kutaka ufanye maombi maalumu kwa ajili ya viongozi wa Serikali ambao baadhi yao wamejiingiza kwenye pepo la ufisadi na kusababisha kamati moja wapo ya Bunge kuvunjwa.
Kwa upande wake, Mchungaji Nosigwe Buya, alimsifu Bw. Mulugo kwa kuuwakilisha vyema Mkoa huo akishirikiana na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrson Mwakyembe na kuwataka wasimame imara kutetea rasilimali za Watanzania ili zitumike vinginevyo.
Mwenyekiti wa ujenzi katika ushirika huo Bw. Anosisye Mbalwa alisema lengo la harambee hiyo ni kupata sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na kituo cha watoto yatima.
Alisema ushirika huo umekuwa ukifanya huduma hiyo kila mwaka bila kujali dini za watoto hao ambapo hivi sasa wameamua kujenga kituo ambacho kitakuwa na msaada zaidi kwa watoto hao.
Katika harambee hiyo, Bw. Mulugo alichangia sh. milioni mbili ambapo jumla ya michango yote ni zaidi ya sh. milioni 24
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment