31 July 2012
Mgomo wa walimu watikisa nchi *Mikoa mbalimbali yaunga mkono, serikali yatoa tamko
Na Waandishi Wetu
WAKATI mgomo wa walimu ukiwa umeanza jana katika baadhi ya shule za msingi na sekondari nchini, Serikali imesisitiza mgomo huo ni batili na kutoa onyo kwa walimu ambao wanawatisha, kuwapiga na kuharibu mali za wenzao wasiogoma, waache mara moja.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawamba, alisema mgogoro huo uko mahakamani hivyo walimu hawapaswi kugoma.
Alisema Serikali imepokea taarifa za kunyanyaswa kwa walimu ambao hawajagoma pamoja na uharibifu wa mali za Serikali unaofanywa na baadhi ya walimu waliogoma kufundisha.
“Tunatoa onyo kwa walimu wote wanaofanya vitendo vya kunyanyasa wenzao ambao wanaendelea kufundisha,” alisema na kuongeza kuwa, baada ya kupata taarifa za mgomo jana asubuhi, alipita katika baadhi ya shule ili kufanya ukaguzi na kukuta walimu wapo madarasani wakiendelea na kufundisha.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu sheria ya ajira na mahusiano kazini yapo masharti ambayo mtumishi anatakiwa kuyafuata anapotaka kujiunga na mgomo ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wote kuunga mkono.
“Wale wote ambao watashiriki kwenye mgomo hawatalipwa mshahara kwa muda watakaokuwa wamemgomea mwajiri ambaye ni Serikali,” alisema na kuongeza kuwa, mgomo una athari kubwa katika jamii na kusababisha uvunjifu wa amani sehemu za kazi, wanafunzi kukosa haki yao ya msingi ya kufundishwa na hatimaye kusababisha matokeo mabaya ya mitihani.
Alisema kwa mujibu wa CWT, mgomo huo ni matokeo ya serikali kushindwa kutimiza madai ya walimu.
Wilaya ya Tarime
Katika hali isiyo ya kawaida, wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, jana waliandamana hadi kwenye Ofisa Elimu Wilaya wakidai haki zao za kupata elimu baada ya walimu kugoma kuingia madarasani na kuwataka wanafunzi warudi majumbani mwao.
Wanafunzi hao waliimba nyimbo mbalimbali ambapo Ofisa Elimu wilayani humo, Bw. Emanuel Jonson, alisema kitendo cha walimu kugoma kufundisha, kinaathiri wanafunzi na kusababisha wengi wao kumaliza shule wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.
Mkoani Morogoro
Jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, jana lilizima maandamano ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari waliokuwa wakiandamana kwenda Ofisi za Mkuu wa Wilaya kupinga kitendo cha walimu kugoma.
Gazeti hili lilishudia wanafunzi hao wakiwa na mabango wakihimba nyimbo mbalimbali zinazoitaka Serikali kuwalipa walimu stahiki zao.
Mkoani Ruvuma
Walimu katika shule mbalimbali mkoani Ruvuma, walishiriki mgomo huo usio na kikomo ili kuishinikiza Serikali kushughulikia madai yao huku Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Joseph Mkilikiti akitishia kuwafukuza kazi walimu waliogoma.
Baadhi ya shule za msingi ambazo walimu wake wamegoma Sabasaba, Mwembechai, Makambi, Mahilo, Majimaji, Sokoine, Bombambili, Sabasaba, Matarawe na Makambi.
Wilaya ya Bunda
Katika Wilaya ya Bunda, Mwenyekiti wa CWT Bw. Ruhumbika Francis, amewataka walimu washirikiane pamoja na kutoogopa vitisho vinavyotolewa na Serikali.
Alisema Serikali mkoani Mara imeanza kutoa vitisho kwa viongozi wa chama hicho ambapo walimu waliitikia mgomo kwa asilimia 95 kwenye shule za msingi na sekondari.
Mjini Moshi
Walimu 8,098 sawa na asilimia 95 ya walimu wote mkoani Kilimanjaro wameungana na wenzao nchini katika mgomo uliotangazwa na CWT.
Katibu wa CWT mkoani humo, Bw. Nathanael Mwandete, alisema walimu 8,525 walipigira kura kati ya hao, 8,098 waliunga mkono mgomo huo na wengine 425 sawa na asilimia tano walikataa.
Mjini Mbinga
Mgomo wa walimu ambao hauna kikomo wilayani humo, jana ulichukua sura mpya baada ya baadhi ya shule kuchukua hatua ya kuwarudisha wanafunzi majumbani kwao na milango ya shule hizo na ofisi za walimu ilifungwa kwa kufuli.
Lushoto
Katika baadhi ya shule za msingi na wilayani Lushoto, jana ziliathirika kwa kiwango kikubwa, baada ya walimu kuitikia wito wa mgomo.
Habari hii imeandaliwa na Veronica Modest, Joseph Mwambije,
Timothy Itembe, Kassian Nyandindi, Yusuph Mussa, Gift Mongi, Deogratius Chechele, Rashid Mkwinda na Agnes Mwaijega.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
i like this blog. thanks for sharing
ReplyDeletenice blog
ReplyDelete