24 July 2012
Kukamilika awamu ya pili mkongo wa Taifa kutasaidia mawasilino-Prof Mbarawa
Na Darlin Said
UWAJIBIKAJI ni majukumu yanayotakiwa kufanywa na watawala na wataliwa ili kuwa na maendeleo endelevu.
Viongozi wana wajibu wao kama watawala na wananchi wana wajibu wao kama watawaliwa ambayo hutegemeana ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
Watawaliwa wanatakiwa kuwajibika kulipa kodi, kutii sheria za nchi, kudumisha amani na kufuata kanuni zilizowekwa kulingana na mazingira waliyopo.
Watawala wanatakiwa kutimiza wajibu wao kwa kuwahudumia wananchi na kusimamia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya Taifa na wananchi wao.
Hivi karibuni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa alifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam na kueleza mafanikio na changamoto katika wizara hiyo.
Anasema mfanikio hayo yamepatikana kutokana na kila mmoja wao alivyoshiriki kikamilifu kutekeleza majukumu yake mahali pa kazi.
Anasema, mafanikio hayo ni pamoja na utekelezaji wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano ambao umekamilika kwa awamu ya kwanza na ya pili.
Anasema awamu ya kwanza ilianza kutekelezwa Februari 2009 na kukamilika Juni 2010 wakati awamu ya pili ilianza kutekelezwa Agosti 2010 na kukamilika mwezi machi 2012.
Anasema kukamilika kwa ujenzi wa Mkongo wa Taifa awamu ya kwanza na pili kunaufanya kuwa na jumla ya kilomita 7,560 na umeunganisha Makao Makuu ya mikoa yote Tanzania bara na baadhi ya makao makuu ya wilaya.
"Kukamilika kwa awamu hizi mbili kunaufanya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwa na mizunguko mitatu, yaani mzunguko wa kaskazini (Northern ring), mzunguko wa kusini (Sourthern ring) Mzunguko wa magharibi (western ring)," anasema Prof Mbawara.
Anasema kukamilika huko kunaufanya kuwa na huduma ya uhakika isiyotetereka kirahisi kwani hata pale inapotokea mkongo kupata hitilafu katika upande mmoja huduma zitaendelea kuwepo bila ya matatizo yeyote kwa kupitia upande mwigine.
Anaongezea kuwa, Kimataifa umeunganishwa na mikongo ya Baharini ya SEACOM na EASSy na unatoa huduma za maunganisho ya mawasiliano kwa nchi jirani za Kenya (Namanga, Sirari na Horohoro), Uganda (Mutukula), Rwanda (Rusumo), Burundi(Kabanga na manyovu), Zambia(Tunduma), na Malawi (Kasumulo)ambayo imeunganishwa na mitandao ya simu ya nchi hizo.
Bw.Mbawara pia alizungumzia kukamilika kwa mradi wa 'Video Conferncing' ambayo ni hudumu muhimu katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu serikalini kwa kupunguza gharama na muda unaotumika katika mawasiliano na vyombo vya usafiri.
Anasema, faida katika huduma hiyo ni pale watendaji watakavyoweza kufanya kazi kwa kushirikiana na kuwasiliana na wadau wengine wakiwa katika sehemu za kazi bila ya kulazimika kusafiri kutoka sehemu zao za kazi na kwenda sehemu zingine na hivyo kupunguza gharama za usafiri na muda ambao ungeutumika kwenda sehemu za mikutano.
Anasema katika kutekeleza usalama wa matumizi ya TEHAMA, serikali imeamua kuanzisha timu ya wataalam wenye weledi juu ya usalama wa mitandao ya mawasiliano ambao tayari imeanza kutekeleza majukumu yake na inaratibiwa na TCRA kwa mujibu wa sheria na kanuni za mawasiliano ya kietroniki na posta.
Awali akieleza mapitio ya sera na uanzishwaji wa Tume ya Taifa ya TEHAMA anasema wizara imechukua hatua za makusudi za kupitia ili iweze kuzingatia mabadiliko ya teknolojia yanayotokea ulimwenguni na kuweza kwenda na wakati na upande wa utekelezaji wake serikali imeunda tume itakayoelekeza na kuratibu masuala hayo.
Anasema, ushirikiano kati ya Tanzania na Kampuni ya IBM kupitia Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia imekamilisha mazungumzo na kampuni hiyo na kusaini mkataba makubaliano wenye lengo la kuanzisha ushirikino katika masuala ya TEHAMA nchini.
Sambamba na hilo aligusia mafanikio yaliyopatikana katika Mfumo wa anwani za makazi na simbo za Posta na utekelezaji wake kuendelea mpaka sasa.
"Mfumo wa makazi na simbo za posta unatoa fursa kwa kila mkazi wa Tanzania kuwa na anwani kamili ambayo itaweza kumtambulisha vyema zaidi kuliko hivi sasa ambao wengi wetu tunatumia masanduku ya posta ambayo ni machache yaliopo nchini.
"Aidha mfumo huu una umuhimu katika utoaji wa vitambulisho vya taifa na pia utarahisishaji katika ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kodi za majengo, pamoja na uandikishaji wa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo sensa," anasema Prof. Mbarawa.
Asisitiza kuwa, mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka mfumo wa anolojia kwenda dijitali yataanza ifikapo saa 06:00 usiku ya tarehe 31 ambapo urushwaji wa matangazo mbalimbali kupitia television yatarushwa kwa mfumo wa dijitali.
Bw. Mbarawa anataja mafanikio mengine yaliyoyapatikana ni kufankiwa katika ujenzi wa Taasis ya Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela ambayo mpaka sasa imedahili wanafunzi 83 ambapo 53 wamedahiliwa kusoma shahada za uzamili na 30 shahada ya uzamivu.
"Uanzishwaji wa taasisi hii ni jambo ni jambo kubwa la kujivunia kutokana na uharaka katika kukamilika ujenzi na kuweza kudahili wanafunzi," anasema.
Katika Sera ya Taifa ya Utafiti na Maendeleo anasema inatoa muongozo wa namna ambavyo haki za watafiti, wagunduzi na wabunifu zitaweza kulindwa ili waweze kunufaika na juhudi walizozifanya.
Kwa sasa sera imeweka bayana namna ambavyo ushirikiano katika utafiti na maendeleo utakaofanywa katika ngazi ya taifa, kanda na kimataifa.
Kwa upande wa sera ya Taifa ya Bayoteknolojia, mkakati wa kutekeleza sera hiyo umeshandaliwa na masuala waliyo yazingatia ni pamoja na kuwepo kwa matumizi salama ya bayoteknolojia, uendelezaji wa rasilimali watu, na suala la maadili katika matumizi.
Anasema, serikali imetoa shilingi bilioni 7 kwa ajili ya utafiti na maendeleo ili kuongeza ufanisi kwa watendaji.
"Upatikanaji wa fedha hizi italeta mabadiliko makubwa ikilinganishwa na upatikanaji ulivyokuwa miaka iliyopita ambapo shughuli za utafiti na maendeleo zinapatikana kwa kiasi kidogo sana," anasema.
Anasema, fedha hizo zimeweza kuendeleza rasilimali watu katika masuala ya itafiti ambapo takribani wataalam 295 wameweza kufadhiliwa.
Anasema aidha fedha hizi zimeweza kufanya ukarabati na pia ujenzi wa miundombinu ya utafiti ikiwa pamoja na maabara na vifaa muhimu vya utafiti.
Anaongezea kuwa fedha hizo zimesaidia kufadhili tafiti 52 ambazo zinaendelea kufanyika katika taasisi mbalimbali za utafiti kulingana na vipaungele vilivyokubalika kitaifa.
"Ongezeko la tengeo na upatikanaji fedha za utafiti na maendeleo unaifanya nchi yetu kuwa moja ya nchi nyingine barani Afrika zinazoweka umuhimu mkubwa katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu, hususani masuala ya utafiti na maendeleo," anasema.
Anasema, upo mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mkoani Mbeya ambapo taratibu za kuanzisha Chuo Kikuu zimeanza na zinaendelea vizuri.
Katika suala la kuendeleza kusimamia matumizi salama ya nguvu za atomiki wizara kwa kushirikiana na Tume ya nguvu za atomikina na Shirika la nguvu za Atomiki Duniani na wadau wengine, imeandaa kanuni zinazohusu uchimbaji, usafirishaji, na uhifadhi wa mabaki ya madini hayo.
Anasema juhudi zinafanywa kupanua matumizi salama ya nguvu za atomiki na ambavyo yatasaidia kutatua matatizo ya msingi yanayoikabili Tanzania.
Anasema, changamoto katika wizara ni pamoja na kuwepo kwa uhaba wa wataalamu wasiokuwa na viwango vya elimu vinavyotakiwa.
Pia uelewa mdogo juu ya masuala ya sayansi na teknolojia na maendeleo ya uchumi hivyo elimu zaidi inahitajika kwa umma ili kufikia malengo na kwa kasi ya kutosha.
Amewasisitiza wafanyakazi wa wizara hiyo kuwa na tabia ya kupima afya zao ili kujitambua kama wameathirika na VVU.
"Na wale wanaoishi na VVU wajitokeze ili Wizara iweze kuwahudumia kwani ni jukumu la letu kuwahudumia wafanyakazi."anasema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment