21 June 2012

Waziri ataka UMMESETA iunde Twiga Stars B



Na Heri Shaaban, Pwani

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenela Mukangara amesema Mashindano ya Shule za Sekondari (UMISSETA) ya mwaka huu yatatumika kuunda timu ya pili ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars).

Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo yaliyofanyika juzi mjini Kibaha, Waziri Fenela alisema haina budi kuunda timu B ya wanawake kwa kutumia wachezaji watakaopatikana katika michuano hiyo.

"Ombi langu la mapendekezo haya, najua litatekelezwa mara moja ili tuwe na timu mbili za wanawake za soka ili zije kuwa tishio siku za baadaye.

"Nimeshudia mechi ya mpira miguu ya wanawake kwa timu za Kanda Nyanda za Juu Kusini, iliyofungwa mabao 10-1 dhidi ya Kanda Mashariki ambazo zimeonesha mpira mzuri," alisema.

Alisema mashindano hayo ni chachu ya kuibua vipaji vya wanamichezo mbalimbali, ndiyo maana mwaka huu michezo hiyo imewashirikisha wadau mbalimbali katika sekta hiyo, ili waweze kuangalia vijana wenye vipaji.

Waziri huyo alisema michezo ni ajira inatakiwa kutambua mchango wake, hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISSEMI kwa ushirikiano na Wizara ya Mafunzo ya Ufundi zinatakiwa kufanikisha mashindano hayo ambayo ndiyo chachu ya kupata wachezaji wa timu ya Taifa wa baadaye.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Jumanne Sagin amezuia walimu wakuu kuuza maeneo ya viwanja vya shule badala yake vibaki kwa ajili ya michezo.

No comments:

Post a Comment