21 June 2012
Vifaa vipya Yanga vyaanza kazi
Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wapya wa Yanga, Said Banahuzi na Juma Abdul 'Baba Ubaya', wameanza mazoezi na timu hiyo yanayoendelea katika Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam na kufanya timu hiyo kuzidi kuimarika.
Wachezaji hao wamesajiliwa msimu huu wakitokea Mtibwa Sugar ambapo wameungana na nyota mwingine, Nizar Khalfan katika kuhakikisha wanaimarisha timu hiyo inayojiandaa na michuano ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Bara.
Gazeti hili lilishuhudia wachezaji hao wakifanya mazoezi ya pamoja na wenzao ambao walianza tangu Jumatatu wakiwa chini ya Kocha Msaidizi, Fredy Felix 'Minziro' huku mashabiki wakionekana kuvutiwa nao.
Pamoja na kufanya mazoezi hayo, lakini kivutio kikubwa kilikuwa kwa Baba Ubaya ambaye hucheza beki wa kushoto, alikuwa akionesha umahiri wake katika kuuchezea mpira na kupiga pasi zenye uhakika.
Beki huyo ambaye ni tunda na Kituo cha Michezo cha Tanzania (TSA), baada ya kuonesha uwezo mkubwa akiwa kituoni hapo ndipo aliposajiliwa na Mtibwa akiichezea timu ya vijana (U-20) lakini msimu uliopita alipandishwa na kuchezea timu ya wakubwa.
Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Minziro alisema anapata matumaini mapya baada ya kuona kila kukicha wachezaji waliosajiliwa na timu yake wanakuja, hivyo ataanza programu ya mazoezi siku si nyingi.
Alisema wachezaji waliokuwa katika timu ya Taifa (Taifa Stars) bado hawajaanza mazoezi, lakini ana imani baada ya siku chache za kupumzika watajiunga na wenzao kufanya mazoezi.
Timu hiyo ndiyo mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, ambalo walilitwaa mwaka jana chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Sam Timbe lakini baadaye alifukuzwa na mikoba yake kuchukuliwa na Kostadin Papic.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment