25 June 2012
INUKA yatoa mafunzo kwa wanachama wake
Na Grace Ndossa
TAASISI inayotoa Mikopo kwa Wanawake Wajasiriamali nchini (INUKA), imetoa mafunzo kwa wanachama wake kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na hatua za kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Mkurugenzi Mtendaji wa INUKA, Bw. David Msuya, aliyasema hayo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo hayo na kusisitiza kuwa lengo ni kuwawezesha wanachama wao ili wafikishe elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari.
“Elimu hii itawawezesha wanachama kufahamu jinsi ya kutoa elimu hii kwa wanafunzi wa shule ambazo zitafikiwa, ukosefu wa elimu ni kikwazo cha mapambano dhidi ya VVU na matumizi ya dawa za kulevya.
“Elimu hii inatolewa na wataalamu wetu ambapo wanachama walioshiriki mafunzo haya, wataanza kuitoa katika shule husika zilizopo mijini na vijijini Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani,” alisema Bw. Msuya.
Aliongeza kuwa, vijana wengi wamekuwa wakijiungta na mitandao inayotumia dawa za kulevya bila kujua madhara yake.
Mwenyekiti wa INUKA, Bw. Peter Yongolo, aliwataka wanachama hao kutoa elimu hiyo hata kwa jamii inayowazunguka kwani vijana na wananchi wengi wanakufa kutokana na UKIMWI.
“Mnapaswa kuwa mabalozi wazuri kila sehemu mnayokwenda ili wanafunzi waweze kuelewa athari za matumizi ya dawa hizi pamoja na kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya VVU,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment