02 May 2012

'Wenye pesa waivuruga CCM'

Na Esther Macha, Mbeya

WAZIRI wa zamani wa Ardhi, Bw. Gidion Cheyo, amesema dhana ya kujivua gamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni nzuri ili kukinusuru chama lakini baadhi ya wanachama wenye fedha wamegeuza maana ya dhana hiyo kwa maslahi binafsi.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa juu wa CCM Taifa unapaswa kuwa makini na wanachama wa aina hiyo vinginevyo dhana hiyo itaendelea kupotoshwa badala ya kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Bw. Cheyo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Ileje, mkoani Mbeya kuanzia mwaka 1992-2010, alisema CCM bado haijapoteza mvuto wala mwelekeo kama inavyoaminika.

Akizungumza na Majira kijijini kwake Mlale, wilayani Ileje, Bw. Cheyo ambaye amewai kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi kuanzia mwaka 1995-2005, alisema CCM ni chama makini kinachoendelea kutetea haki za wanyonge.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha wanachama wetu ambao wamepoteza mwelekeo wanawekwa pembeni, watu wengi wanasema CCM imepoteza mwelekeo, watu wachache ndio wanasababisha hali hii hivyo lazima waenguliwe na kuvuliwa nyadhifa walizonazo ndani ya chama,” alisema.

Hivi karibuni, kumekuwepo na mvutano wa mara kwa mara npamoja na tuhuma zisizokitakia mema chama hicho hivyo kusababisha hofu kwa watu wenye mapenzi nacho.

Wakati vuguvugu la uchaguzi ndani ya chama hicho linaendelea kushika kasi, Bw. Cheyo amesema kama watamhitaji yupo tayari kuwania nafasi yoyote ili aweze kukinusuru chama hicho.

Alisema wapo viongozi wengi wastaafu ambao kama mchango wao utahitajika, wapo tayari kutoa ushauri ambao utasaidi kukiimarisha chama hicho.

No comments:

Post a Comment