KILA kukicha suala la posho limekuwa likichukua suala jipya huku kila mmoja akiibuka na kuongea lake.
Viongozi wamekuwa wakitupiana mpira kuhusu suala la posho jambo ambalo limekuwa likiwakanganya wananchi kutokana na viongozi hao ambao wanadhamana kubwa kutokuwa na kauli ya pamoja.
Kutokuwa na kauli ya pamoja kwa suala moja kwa baadhi ya viongozi serikalini kunaonyesha mapungufu na udhaifu mkubwa sana ndani ya serikali.
Japo kila binadamu ana mapungufu yake lakini ukweli ni kwamba tunapofanya kazi kwenye taasisi au shirika moja tunapaswa kuwa makini na mambo kabla ya kuyatoa kwa umma wa Watanzania.
Naweza kusema kutofautiana kwa viongozi hao kunaonyesha wazi kwamba viongozi hao huwa wanafanyakazi pasipo mawasiliano jambo ambalo halipaswi kuwa.
Utakubaliana na mimi kwamba mawasiliano ni kitu cha muhimu sana na ili kazi ziweze kuendelea mawasiliano yanahitajika.
Naamini kwamba kabla maamuzi ya kutangazwa jambo fulani ili umma wa Watanzania wafahamu ni lazima kwanza wahusika wakae na kukubaliana sasa tutasema haya na haya hatusemi.
Nasema kwamba mnawachanganya wananchi katika hili la posho kwa kuwa hivi karibuni aliibuka Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, na kuwaeleza wahariri wa vyombo vya habari kwamba jukumu la kuidhinisha ongezeko la posho ameachiwa yeye na ndiyo mwenye jukumu la kusaini au kutosaini.
Lakini kabla ya Bw. Pinda kusema hayo, alianza Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda kwa kuwaeleza waandishi wa habari kwamba posho zimepanda kutoka sh. 70,000 hadi sh.200,000 na tayari wabunge wamekwishaanza kulipwa.
Bi.Makinda hakuishia hapo aliendelea kuweka wazi kwamba Rais Kikwete ameshatoa kibali chake na mbunge atalipwa katika vikao tu.
Wakati wananchi wa kada mbalimbali wakiendelea kuhoji na kupinga uhalali huo wa ongezeko la posho za wabunge ,aliibuka tena Bw. Pinda kwa mara nyingine na kuwaeleza wabunge kwenye vikao vya utangulizi kwamba tayari Kikwete alikuwa ameidhinisha ongezeko la posho za vikao.
Tukiwa tunaendelea kutafakari hilo, Rais kupitia Kurugenzi yake ya Mawasiliano ilitoa taarifa za kukanusha kwamba Rais hajabariki ongezeko hilo la posho.
Katika taarifa hiyo iliekeza kwamba rais anakubaliana na hoja ya nyongeza ya posho kwa wabunge, lakini amewataka wabunge kutumia kikao cha sasa cha bunge kulizungumzia upya suala hilo.
Kufuatia kutofautiana kwa viongozi hao cha kujiuliza ni nani mkweli kati ya Bi.Makinda, Bw.Pinda na rais na tumuamini nani kwa kile wanachosema.
Naweza kusema ukweli tunaweza kupata kwa wahusika ambao ni wabunge lakini sina uhakika na hilo kwani hata nao wanaweza kutudanganya kwa kuhofia kwamba wakisema ukweli mwisho wa siku wanawezakuponzwa na ukweli huo.
Suala la posho sasa limegeuka kuwa utata mtupu kutokana na viongozi wakubwa kutofautiana kwa kauli na huku kila mmoja akimbebesha mzigo wa lawama mwenzake.
Japo wananchi tunaendelea kupiga kelele kupinga nyongeza hiyo lakini hata kama wameanza kupata potelea mbali lakini ninachojiuliza hapa ni kwa nini viongozi hao watofautiane, hawaoni kama wanatuchanganya kwa kushindwa kwao kutueleza ukweli.
Binafsi nadhani posho zimeongezwa na wabunge wamekwishaanza kulipwa viwango hivyo, lakini kwa kuwa kila mmoja anaogopa kushutumiwa ndio maana kauli zao zimekuwa zikitofautiana ili mradi tu watupeleke kisiasa.
Rais ambaye kwa mujibu wa katiba ndiye muamuzi wa mwisho kwenye suala hilo anaanza kutupa mpira, je, tumueleweje au ndo tusema anakwepa jukumu lake.
Kitendo cha Rais kusema kwamba suala hilo lijadiliwe kwenye kikao cha sasa cha bunge si kuhalalisha, hivi unadhani kweli wabunge hawa wa Tanzania tuliowachagua wanaweza wasijiongezee posho hizo?
Inawezekana kweli kumuachia fisi mfupa ili hali unafahamu fika kwamba fisi huyo ana njaa na anautamani sana mfupa huo, sasa suala la rais kuwaachia wabunge kujadili suala la posho, hivi unadhani wabunge hawatapitisha.
Kimsingi sitaki kueleza kama posho ni halali au vipi, ila ni kwa nini viongozi hao wanatofautiana katika kutoa maelezo.
Utata huo unanifanya niamini kwamba ndani ya serikali kila mtu anaweza kukurupuka kuongea kile anachoona kinafaa kuongea bila kuwasiliana na wenzake.
Ukweli ni kwamba kinachotakiwa kufanya ili kuepuka kutofautiana ni lazima wahusika wahakikishe kwamba kabla ya kufikia uamuzi wa kuujulisha umma kitu fulani ni lazima mawasiliano yawepo.
Kuwepo kwa mawasiliano baina ya wahusika kutasaidia sana na hata pale mmoja anapokosea ni rahisi kusahihisha kuliko hili la posho kwani ni vigumu kulisahihisha.
Bw. Pinda, Bi. Makinda na Rais msijikanyage kuhusu suala la posho kama mmeshindwa kutoa maamuzi basi sikilizeni ushauri wa wananchi waliowachagua kwa kuwaunga mkono kuzipunguza zaidi badala ya kuongeza.
No comments:
Post a Comment