Zena Mohamed na Zourha Malisa
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia Bw. Leonard Mwihilo
kwa kosa la kutumia cheo cha Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, Bw. Ernest Chale, kuwatapeli wananchi kwa kutumia nyaraka feki za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema Bw. Mwihilo alikamatwa na watendaji wa manispaa hiyo katika eneo la Kisutu baada ya kwenda kukusanya fedha kwa wafanyabiashara.
Bw. Mwihilo aliweka ahadi ya kwenda kukusanya fedha katika maduka ya wafanyabiashara siku ya tukio na kuwekwa mtego ambao ulifanikisha kukamatwa kwake,¢®¡¾ alisema.
Kwa upande wake, Bw. Chale alisema ni mara ya pili kwa Bw. Mwihilo kukamatwa akiwa na nyaraka mbalimbali zinazofanana na chama hicho kama mihuri feki na barua zikiwa na saini tofauti.
Alisema baada ya kukamatwa mara ya kwanza, walimalizana kichama bila kufikishana katika vyombo vya sheria kama ilivyo.
Wakati huo huo, Kamanda Kova alisema majambazi watatu wamekamatwa na jeshi la polisi katika maeneo tofauti Jijini Dar es Salaam akiwemo dereva wa teksi Bw. Rajabu Yahya (31), kukutwa na silaha aina ya SMG, yenye namba 'N'.34-MT-3072, ikiwa na risasi 29.
Alisema Kikosi cha Kupambana na Uharifu Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wakiwa doria eneo la Kiwalani, walipokea taarifa kuwa kuna majambazi wana silaha aina ya SMG.
Majambazi hao walikuwa wakitumia gari ndogo yenye namba za usajili T 968 BSH, aina ya Toyota Carina, kwamba wamepora pesa kwenye gari inayomilikiwa na Kampuni ya Chibuku, yenye namba za usajili T 841 DHT.
Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, walifanya msako na kufanikiwa kukamata gari hiyo likiwa na jambazi huyo ambapo msako wa kuwatafuta wengine unaendelea.
Jambazi mwingine ni Bw. Kadini Kitoni (30), mkazi wa Vingunguti ambaye alikamatwa eneo la Tazara akiwa na gari aina ya Toyota Dyana Pick Up, yenye namba za usajili T 316 BWW, ikiwa na matairi 10 ya gari, yenye ukubwa wa saizi 305/80.
Kamanda Kova aliongeza kuwa, majambazi wengine walikimbia baada ya gari hilo kusimamishwa na msako wa kuwatafuta unaendelea.
Alisema jambazi wa tatu ni Bw. Said Mohamed (50), mkazi wa Mbagala Kiburugwa ambaye alikamatwa na nyaya za umeme zenye urefu wa mita 900, mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na uharibifu wa miundombinu ya shirika hilo na upelelezi wa kuwatafuta wenzake unaendelea.
No comments:
Post a Comment