08 December 2011

Kampuni ya Wind EA yapewa leseni kuzalisha umeme

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati ya Maji (EWURA), imeipatia leseni ya uzalishaji umeme wa upepo Kampuni ya Wind East Africa ili kuzalisha nishati hiyo
nchini.

Akizungumza katika makabidhiano ya leseni hiyo jana, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw.Haruna Masebo, alisema hatua ya kuidhinisha kampuni hiyo imetokana na kuridhika na utendaji wake na kukidhi vigezo.
Bw.Masebo alisema kampuni hiyo imeweza kufuata masharti yote yaliyowekwa na kuwa kampuni ya kwanza nchini kuingia katika biashara ya uzalishaji nishati ya umeme.

“Ni faraja kubwa kuona kuwa kampuni inayomilikiwa na wazawa kuingia katika biashara hii, tumeridhika na mipango yao hasa baada ya kukamilisha masharti yote yaliyowekwa pamoja na uhifadhi wa mazingira,” alisema Bw.Masebo

Alisema kibali hicho ni cha miezi 30 na wanatarajia kuona matunda mazuri ya kuondoa tatizo la nishati ya umeme nchini.

Naye Mkurugenzi wa Wind EA, Bw. Rashid Shamte, alisema wanafuraha kupata kibali hicho na Watanzania watarajie kuwa tatizo hilo litaisha mara baada ya kukamilika kwa mradi huo.
Bw.Shamte alisema pamoja na kupewa miezi 30, wanatarajia kukamilisha mradi huo mapema iwezekanavyo mara baada ya kukamilisha mikakati yao ikiwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB).
Alisema wamezingatia masharti yote yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kutoathiri mazingira ya eneo la mradi huo tofauti na miradi mingine.

“Tumekuwa makini mno na hilo kwani tuna wataalamu wa hali ya juu, tunashirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha uzalishaji wa megawati 100 za umeme kwa Watanzania,” alisema Bw.Shamte.
Alisema walifanya utafiti wa mradi huo mwezi Novemba mwaka jana na Wizara husika iliwajibu kuridhishwa na maendeleo na mikakati yao Februari mwaka huu.

No comments:

Post a Comment