13 December 2011

CCM yashauriwa kuanzisha kampuni kujiendesha

Na George Boniphace,Mwanza

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeshauriwa kuanzisha kampuni ya uzalishaji itakayokiwezesha kujipatia mapato na kuondokana na hali ya kuwa ombaomba kwa matajiri. Ushauri huo
ulitolewa hivi karibuni na mmoja wa wanachama wa chama hicho mkoani hapa, Bw. Emmanuel Manoni, wakati akizungungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa.

Bw. Manoni alisema kutoka na CCM kukosa miradi ya kuiingizia fedha baadhi ya matajiri nchini ndio sasa wamekuwa sauti ya chama hicho hivyo kukivuruga.

Alihoji tabia ya wafanyabiashara wengi kukikimbilia chama hicho huku wakiwa na sifa mbaya katika kazi zao ikiwemo kukwepa kodi za serikali na kujihusisha na magendo.

"Wafanyabiashara hao wanapokuwa wamefanikiwa kuingia ndani ya chama huwa na sauti na maamuzi makubwa kuliko wanachama wengine wasiokuwa na mali hali ambayo inasababisha chama kuyumbishwa," alisema Bw. Manoni

Alisema iwapo chama hicho kitafanikiwa kuwa na kampuni yake ya uzalishaji itakiwezesha kufanya shughuli zake kwa uwazi na kulipa kodi za serikali.

“Kwa sasa chama hiki tunashindwa kujiendesha wenyewe kwa vile hata miradi yenyewe iliyopo haiingizi faida, wajanja wamewahi na tutaendelea kuwa chini ya matajiri wafadhili wa chama hicho.

Sisi wakulima na wafanyakazi tutakohoa lini kama chama hiki tumepokonywa na wafanyabiashara?",Alihoji Bw. Manoni.

Alisema historia ya CCM ilipoanzishwa  ilikuwa chama cha wakulima na wafanyakazi na kuwakilishwa na nembo ya chama hicho ya jembe na nyundo ambayo haijabadilika.

Alidai hivi sasa makundi hayo mawili ya wakulima na wafanyakazi wameenguliwa katika chama hicho kwa kunyimwa nguvu na wafanyabiashara jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wake.

Alisema katika miaka ya 80 na kuendelea CCM ilianzisha miradi mbali mbali ya kiuchumi kupitia shirika lake la SUKITA na kuhoji fedha za miradi hiyo zilipo kwa sasa.

Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa upangishaji wa majengo yake na kwamba fedha zilizokuwa zikipatikana enzi hizo ilitumika kuimarisha chama hicho.

Alisema wapo wajanja wanaohujumu chama hicho kwa kutafuna fedha kidogo zinazotokana na miradi hiyo na kuwafananisha na mchwa ndani ya ubao.

No comments:

Post a Comment