23 November 2011

Maandamano makubwa kumpinga JK Jumamosi

*Yatahusisha asasi 180,TUCTA, wenye VVU
*Ni kumshinikiza asisaini muswada wa katiba
*Kikwete afurahia kukutana na CHADEMA

Na Benjamin Masese

WANAHARAKATI wa asasi za kiraia zaidi ya 180, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Jukwaa la
Katiba Tanzania, wameandaa  maandamano makubwa yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi, wiki hii ili kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asitie saini muswada wa mchakato wa katiba mpya.

Tamko la kuitishwa kwa maandamano hayo lilitolewa Dar es Salaam jana na wanaharakati hao kwa hoja kuwa muswada wa katiba mpya uliopitishwa bungeni wiki iliyopita hauna nia njema kwa wananchi wa Tanzania.

Miongoni mwa waliothibitisha kushiriki maandamano hayo ni vyama vyote vya watu walemavu, wanaoishi na UKIMWI na taasisi za kiimani.

Akitoa tamko hilo Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Bw. Deus Kibamba alisema asasi za kiraia zaidi ya 180 zimethibitisha kushiriki maandamano hayo na zinaendelea na ushawishi wa kuwataka wananchi washiriki.

Bw. Kibamba alisema iwapo mchakato muswada uliopitishwa utasainiwa na  Rais Kikwete kama ilivyokusudiwa, basi kuna hatari kubwa ya rasimu ya katiba itakayopatikana kukataliwa na wananchi wakati wa kura ya maoni, kwa kuwa wanaharakati watakuwa wameeneza sumu kwa wananchi.

"Matokeo yake ni kupoteza fedha nyingi za umma na kuendelea kulitia hasara taifa, huku wananchi wakitaabika kwa umaskini," alisema.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo jukwaa limeona ni vema kulinusuru taifa na kuwawezesha wananchi kuamua wenyewe kuhusu hatma ya maisha yao, kwa kuandaa maandamano nchi nzima yatakayoshirikisha wananchi ili kutoa kilio chao.

Alisema maandamano hayo yatafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na yanaratibiwa na jukwaa hilo.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam yataanzia viwanja vya Mnazi Mmoja saa mbili na kuelekea katika viwanja vya Jangwani.

Bw. Kibamba alisema  hakuna sababu yoyote ya maandamano hayo kuhitaji kibali cha polisi na hawatarajii kwenda kukiomba kwa sababu muswada wa mabadiliko ya katiba uliopitishwa umebeba adhabu ya jinai na vitisho kwa wananchi.

"Suala la kibali ni dhana potofu wala, hatuna nia ya kukiomba... hatuna muda wa kwenda kuonana na makamanda wa kila mkoa, jukumu hilo ni la IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) na sisi tumempa taarifa na yeye," alisema Bw. Kibanda.

Alisema polisi wanatakiwa watumie intelejensia yao kubaini kama kutakuwa na upungufu wa amani katika maandamano hayo.

Alisema kilichofanyika bungeni ni kinyume ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayotoa uhuru wa wananchi kutoa maoni yao.

"Tunatoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya amani ya kumtaka Rais Kikwete asitie saini muswada huo, kwani wananchi wengi watakuwa wamekosa fursa ya kushiriki mchakato wa katiba kuanzia hatua ya msingi, vinginevyo wengi tutajikuta tuko jela na hivyo kujenga chuki baina ya serikali na wananchi na matokeo yake ni uvujifu wa amani," alisema na kuongeza;

"Tuhamasishane wanawake na wanaume, vijana na wazee, wakulima na wafugaji, wafanyakazi na viongozi wa taasisi zote za kiimani, polisi hasa brass band tunaomba watuongoze kwenda viwanjani, lengo letu kuu ni kujenga msingi mzuri kwa ajili mwafaka wa kitaifa kupitia ushiriki wa Watanzania wote."

Bw. Kibamba alisema kama kweli Rais ni msikivu na mpenda wananchi wake na amani ya nchi kwa ujumla, basi hatasaini muswada huo.

Alisema Rais akifanya hivyo atakuwa ametumia uamuzi wa busara kuliko wakati mwingine wowote wa uongozi wake.

Bw. Kibamba alisema kitendo cha muswada huo kusomwa mara ya pili kabla ya kufikishwa kwa wananchi wa maeneo yote ya nchi ni kujenga msingi mbovu wa katiba ya nchi.

Alisema wabunge walioshiriki muswada huo wajiulize kama nyumba inayojengwa ina msingi imara na kama itadumu.

Msimamo wa TAMWA

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya, alisema anasikitika kuona wabunge wanawake bungeni, wanageuka vipashio, wakizungumza kwa jazba, kubezana wao na vyama vyao na ndio maana wamepitisha muswada uliobeba adhabu ya jinai na vitisho.

Bi. Nkya alisema  wanalaani mapema matamshi yaliyokuwa yakitolewa na wabunge na viongozi wengine wa serikali, ambayo asilimia kubwa yalikuwa yanapotosha ukweli.

"Tunalaani matamshi na matamko yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa serikali na wabunge dhidi yetu na kauli hizo zimetolewa kiitikadi zaidi kwa kuwa hazielezi ukweli wa jambo," alisema na kuongeza;

"Niwajulishe wabunge kwamba walichokifanya ni kama kujenga nyumba ya msingi wa uyoga au keki, pia wafahamu hawajatendea haki wananchi wao na ndio maana wengine wanaona aibu kwenda kuwaeleza hilo."

Bi. Nkya alisema wabunge walishindwa kujadili muswada badala yake walijadili majukwaa, majina ya watu na vyama vya siasa, huku wengine wakionekana kama vipashio vya mijadala na kujisahau.

Msimamo wa TUCTA

Naye Naibu Katibu Mkuu TUCTA, Bw. Herzon Kaonya, alisema ikiwa Rais atasaini mkataba huo itakuwa ni kielelezo sahihi cha kuwapuuza wananchi wake.

Aliongeza kuwa kwamba watachukua hatua mbadala ya kukusanya maoni kwa wananchi ikiwa muswada huo utasainiwa.

Bw. Kaonya alisema kuna uwezekano mkubwa wa mfumo uliotumika kupitishwa muswada huo ndio utakaotumika kutafuta maoni kwa wananchi.

Alisema kawaida ya watawala barani Afrika hupenda kujiwekea vitu ambavyo hulinda maslahi yao na kuwaandaa watoto wao kuendelea kushika nyadhifa huku wakiwapuuza wananchi.

"Nasema serikali itambue kwamba iliwekwa madarakani na wananchi na itaondolewa na wananchi hao hao," alisema. 

Msimamo wa TGNP

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Issu Malya, alisema serikali imevurunda, hivyo haikuwatendea haki wananchi.

"Watu wanafanya maamuzi kwa itikadi za vyama, bila kujua kuwa vyama vitakufa na wananchi watabaki, nyumba zitabomoka, lakini watu wataendelea kuwepo, kwa kweli naweza kusema kuna upepo mchafu umeingia nchini na ndiyo unawasumbua viongozi na kushindwa kujua wanachokifanya," alisema.

Wanaharakati hao wametoa msimamo huo huku Rais Kikwete, akiwa ameishatangaza kusaini muswada huo mapema akishirikiana na Rais wa Zanzibar.

Tamko hilo la wanaharakati limetolewa ikiwa ni siku siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza majina ya watu sita watakaokwenda Ikulu kuzungumza na Rais Kikwete, kuhusu sakata hilo la katiba.

25 comments:

  1. Nawapongeza kuandaa maandamano iwe kwa amani ya yawe na utulivu. Lakini wasiwasi wangu bila kupata kibali au kuwataarifu Polisi ina maana sio tunadharau katiba iliyopo au?Je, ikitokea vurugu,uporaji au uvunjifu wa amani- maana ktk kundi la mamba na kenge wamo je, itakuwa jukumu la nani?Tusiwe na jazba ni muhimu wanausalama wakawepo ili kudhibiti hao wanaotaka kubadhilisha dhana nzima ya maandamano ya Amani yakawa ni vurugu!!

    ReplyDelete
  2. KWANI NYERERE ALIPOKUWA ANAPIGANIA UHURU NA HAKI YA WATANGANYIKA ALIOMBA KIBALI KWA NANI ZAIDI YA WANA NCHI?HII NI VITA KATI YA WATAWALA NA WATAWALIWA.WANANCHI TUTAKUJA,NA MWISHO WA SIKU TUTAWAKATA VIDOLE VYAO.

    ReplyDelete
  3. Makala hii ni ndefu lakini sioni mantiki katika taarifa hii. Sijui kama mwandishi anajua nini alitakiwa awaarifu wananchi kwani naona naye anapiga porojo tu Nilidhani ataeleza kwa kina ni nini ambacho waandamanaji wanaona kilikosewa bungeni. Chambua kwa kina point by point kilichoko katika mswada na eleza kilicho na makosa katika hayo na waandamanaji waonyeshe walitaka mswada usomeke namna gani

    ReplyDelete
  4. ninaunga mkono! ninaongeza taasisi nyingine ya 19...familia ya wanadodoma (wanyausi)!!! hili tumedhamiria!!! hatutakua nyuma, tutakua sambamba, nchi yetu ...tutaijenga wenyewe!!! na tena ndugu zangu tunayo haja ya kuhoji hapo baadae, tumhoji rais huyu akiishang'oka...kwamba kwanini aruhusu watu kutumia nguvu na muda mwingi kudai jambo lililowazi kabisa...!!?? ...tutamhoji, mamlaka zitachunguza kama anakesi ya kujibu hapo!! kama kweli umechaguliwa na wananchi na nchi unayoiongoza ni ya kidemokrasia kwa mujibu wa katiba iliyopo, kwa jambo kama hili rais anasubiri watu waende ikulu kumnong'oneza.., ye kiziwi!??? yupo nchi gani ambapo watu wanalia yeye hasikii ila hadi ujumbe umwendee?!!!

    ReplyDelete
  5. Naungana Kabisa na Wanaharakati wa Asasi za Kiraia,TUCTA,Tamwa,TGNP,na jembe chama cha Chadema kuwa na Msimamo huo Swala la kuburuzwa watanzania leo hii halipo na sijui kwanini JK hataki kuliona hilo.Wabunge wa CCM na Serikali ya JK Imechoka.

    ReplyDelete
  6. ndugu wajinga viongozi na wabunge wetu,watanzania wenzetu.
    serikali hii ni ya mpito ama ni ya kikoloni.
    mbona tanzania haitendei haki watu wake na inapelekwa ki dictator.tuanze katiba.ni mali ya nani?ufisadi ni kuvunja sheria,ama wizi.kama kweli maana yake ushahidi upo.kazi ya mahakama ni nini ikiwa mwamuzi wa haya yote ni ccm ,nape , sita na wengine wachache.nani wao katika hii inchi hata watudanganye kila siku.wacheni upumbavu na toshekeni na mishahara yenu .maisha yenu nyie mdanganyao watu kwa madaraka tuliyo wapa.mvueni mmoja gamba tuone basi. ama sainini mswada huo tuone basi.
    pelekeni ulimbukeni wenu kwenu maumbwa wakubwa nyie

    ReplyDelete
  7. Nawapongeza kuandaa maandamano iwe kwa amani ya yawe na utulivu.

    Lakini wasiwasi wangu bila kupata kibali au kuwataarifu Polisi ina maana sio tunadharau katiba iliyopo au?

    Je, ikitokea vurugu,uporaji au uvunjifu wa amani- maana ktk kundi la mamba na kenge wamo je, itakuwa jukumu la nani?

    Tusiwe na jazba ni muhimu wanausalama wakawepo ili kudhibiti hao wanaotaka kubadhilisha dhana nzima ya maandamano ya Amani yakawa ni vurugu!!

    ReplyDelete
  8. Nashindwa kulewa awa wanaharakati. Hao wananchi ndio hao waliochagua wabunge kibao wa CCM unategemea utapata nini kutoka kwao?

    ReplyDelete
  9. Ninyi waandishi wa habari hamtutendei haki sisi wananchi wa kawaida. Hii makala yako umeiandika kiimla.Jamani waandishi wa habari, jaribuni kutuandikia angalau habari zenye upembuzi yakinifu.
    Mfano, unaandika ''Akitoa tamko hilo Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Bw. Deus Kibamba alisema asasi za kiraia zaidi ya 180 zimethibitisha kushiriki maandamano hayo na zinaendelea na ushawishi wa kuwataka wananchi washiriki'' kama kweli ungekuwa mwandishi mathubuti ungejitahidi kuzijua na kuzitaja katika makala yako hizi asasi zaidi ya 180 zinazoshiliki maandamano badala yake umetaja asasi sita tu. kwa mwandishi aliyemakini na kazi yake ungetaka kujua ni asasi zipi kama mwenyekiti wa jukwaa la siasa anavyodai na kufatilia kujua mwitikio wa hizo asasi ukoje.
    Habari yako inaibua maswali mengi ambayo hayana majibu kwa msomaji kutokana na ukosefu wa upembuzi yakinifu.
    Jaribu kuachana na uandishi wa habari wa mtindo wa Copy & paste

    ReplyDelete
  10. Hata mimi pia naunga mkono wanaharakati,kwanza wabunge wa chama tawala hawajawatendea haki wananchi kwa kupitisha mswada uataoleta matatizo siku za usonina si kwamba hawajui wanajua ila tu ni kutaka kutetea maslahi yao.pili hata rais naye kama atasaini huo mswada naye pia si kitu kwa wananchi namshauri atumiae busara,hekima zake bila kuangalia itikadi ya chama chochote.sasa hivi robo tatu ya nchi wanapiga kelele maswada huo asiusaini jamani "wengi wape"hata tunapomchagua kiongozi fulani wa ngazi ya juu kama rais lazima tuangalie kwanza sifa:je ni mtanzania,anafaa na zingine nyingi lakini bila kusahau sifa mama je anakubalika na wananchi? sasa wananchi hawataki usaini mswada na wewe unasaini je utakuwa umewatendea haki unawatawala?au kwa vile wamekuchagua basi uanaweza kufanya lolote unalotaka bila kumpa uhuru mwananchi wa kutoa maoni kama katiba inavyosema.mwsho nasema suleiman wa biblia alipoambiwa na mungu achague mali na hekima alichagua "Hekima"maana ndiyo iliyomuongoza ktk kutawala nchi ile hekima ni kila kitu ktk maisha ya mwanadamu.

    ReplyDelete
  11. Hakuna sabubabu ya kutousaini mkataba,Rais ni msikivu na mwenye kuelewa lililobaki kwa wapinzani kuona Rais hafanikiwi katika utendaji wake.
    Kwa jumla upande wapili wa Muungano wameridhia inatosha kusainiwa bila matatizo yeyote,wasiotaka kuona katiba inapita ni wale wasijuwa ni serikali ya Muungano na asili yake ilipoanza huko nyuma.

    ReplyDelete
  12. Maneno mengi yamesemwa n aviongozi wastaafu na wananchi wapenda amani wa nchi hii lakini wasiwasi wangu ni kwamba viongozi huwa na tabia yakudharau wananchi pindi wanapokuwa madarakani lakini wakitoka wanaona mapungufu mengi,mfano jaji mkuu mstaafu Samatta amelitambua hilo sasa hivi upungufu wa katiba,hivyo hakuna tofauti ukimsikia Kombani akisema haoni tatizo kuhusu katiba hii tuliyonayo na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Werema. Cha msingi wananchi tusonge mbele kudai katiba ya kweli ambayo msingi wake uwe kwa ajili ya wananchi na rasilimali zao na siyo kutafuta kinga ya watu kukaa madarakani bila kuleta tija yoyote isipokuwa siasa nyingi zilizojaa hadaa na maneno mengi mapya yakutunga yasiyo na manufaa yoyote 'eti Tumethubutu,tumeweza na sasa tunasongo mbele' mbele yenyewe inayobeba ujumbe hakuna, wananchi ndio tunazidi kuishi kwa matumaini kama wagonjwa mahututi.

    ReplyDelete
  13. Hifi hao Wabunge waliokubali huo musuada wa katiba ni wazima kisaikolochia!? siamini kama wako sawa!.. make wao wametawaliwa na viposho wanavyo pata humo Bungeni kiasi kwamba wananchi waliowachagua hawadhaminiki kwao tena!!!!!....musishangae eti katiba imekidhi kwa "CHAMA NA VIONGOZI HASWA RAIS" wananchi waliowachagua wako upande gani? au ndo munaturudisha enzi za UKOLONI? kuwanyenyekea viongozi na kuendelea kuwa watumwa kwenu!?. ina maana viongozi nyie ni MARIKANI NA WANANCHI NDIO WATANZANIA SIO?. Watanzania hamasikeni kwa kusoma magazeti, kuangalia taarifa, kuingia kwenye mitandao na habari muhimu ili kuwa na mawaso yenye TIJA katika hii KATIBA YA KIJAMBAZI musisubiri kuambiwa na mwenzako wala rafiki mjionea wenyewe...

    ReplyDelete
  14. Ndugu zetu wa Tanzania bara mnataka nini sasa. Jee mmechoka na amani?Zanzibar tulikuwa hivyo hivyo kama nyinyi , wengi walikufa, walipoteza kazi na mali zao na mwisho tukaamuwa tukae pamoja na tujenge Zanzibar yetu.ninawashauri mfikie muafaka kwa mchakato huu wa katiba
    November 23,2011 1.25pm

    ReplyDelete
  15. NYIE MNAOJIITA WANAHARAKATI (MIMI NAWAITA CHADEMA B) NI NINI HASA KILICHOKOSEWA KATIKA MCHAKATO HUU WA KATIBA? MSIWAPOTEZEE MUDA WANANCHI.NAWAASA WA TZ WENZANGU TUSIIGE TU MAMBO TUSIYOYAJUA HAO VIONGOZI WA CHADEMA "B" WANAPOKEA NA WANAKULA MAMIILIONI YA PESA ZA KUTOKA NJE.NYIE MTAISHIA KUPIGWA JUA NA HATA KUPIGWA VIRUNGU NA POLISI.NAJUA WENGINE WANAFUATA TU MKUMBO.NDIYO MAANA HATA VIONGOZI WA CHADEMA WAMEONA HAYO MAANDAMANO HAYAWATAISIDIA KITU,NDIYO MAANA WAMEAMUA KUMUANGUKIA RAIS

    ReplyDelete
  16. ...nadhwni hapa kuna ule usemi unao thibitisha kwamba binadamu ameumbwa na usahaulifu wakupindukia.Kumbukeni watanzania wenzangu wakati wa harakati za kura ya vyama vingi asilimia 20% ndio iliyosema OK kwa vyama vingi na BABA wa TAIFA ndie alie watetea na akawalazimisha watawala wetu wasiwapuuze.Mtetezi wetu MTUKUFU aliye jua kusoma alama za nyakati hatunae tena duniani,watawala wanafikra zile zile kidumu kile kilichoua nyenzie.Nawakumbusha kwamba ile asilimia 20%(kwa sasa ni zaidi ya 60%) ndio hiyohiyo inataka isikilizwe na ndipo demokrasia ya kweli itatamalaki.Hivi kama mswaada ule ungesomwa tena kwa mara ya kwanza tena baada ya kukamilika kwa usanifu wa lugha halafu ukapitishwa tena kwa wananchi walio wengi hata kwa kuona tu,ingekua ni hasara ya kiasi gani kwa taifa wakati akina Jairo na wengine wana ponda mipesa ya wasaga lami na wavuaja jasho na damu? Hivi Rais wetu anapotamba kwamba anfuata nyayo za watangulizi wake bila soni mbona anashindwa kuzisoma alama za nyakati,kwa taarifa yake washauri wake wanamzodoa na wanamgo'nga na hushangilia kila anapotoa hotuba tatanishi kama ile ya majuzi PTA hall.

    ReplyDelete
  17. Hawa jukwaa la Katiba hawana jipya, Bilashaka huyu Kibamba na wenzake hawajui na hawaelewi taratibu na Kanuni na Njia ipi iliyosahihi katika kufia hatua hii ya Muswada. Huyu na wote hawa wanatumiwa ili kuona kwamba Uundaji wa Katiba Mpya HAUFANIKIWI kwa Maslahi ya hao waliowatuma. Waeleze Wapi Palipokosewa na Parekebishwe vipi. OOHH hawajafikiwa Wananchi wengi. Wakati wa Mchakato wa Awali wao walikuwa wapi? Waache Tume iundwe na Wanachi tuliowengi tutoe Maoni yetu kwa uwazi. Sasa wanachotaka Hawa Jamaa ni Nini? Mbona hawasemi hicho kilichokosewa zaidi ya kuwatwisha Mzigo Wananchi? Hivi Hawa wanawanchi gani wanaowatetea? Kama sio Uongo na Uchochezi huu?
    Naliomba Jeshi la Polisi Wasiwaogope waanze nao mapema hata sasa kabla hawajaanza kutuvurugia Amani na Utulivu wetu. WAKAFUTE HUKO KWA KUANDAMANIA WAENDE SOMALIA:

    ReplyDelete
  18. Wakaandamane kwa Mama zao, Wananchi gani wanaowatetea? Tunasubiri kwa Hamu hiyo Tume ije Tutoe Maoni ya Katiba Tuitakayo ya Miaka 50 ijayo. Hawa wasiosema pamekosewa wapi wabaki Hivyohivyo. Hatuwaelewi ni Vibaraka tu Hawa akina Kibamba kama wametumwa na hao wanowaleta fedha za kuendesha NGO zao tutaonana mbele ya Safari. WAJINGA WAKUBWA MIBICHWA ILIYOFILISIKA KIFKRA:

    ReplyDelete
  19. Ni dhahiri kuwa sasa watawala wetu hawataki tena uwepo wa amani nchini kwetu. Hii jeuri ya Rais na washauri wake akina Kombani, Warema, na huyu mama wa Bunge ni ya kutisha.
    Hawa ni watu nadhani waliokwenda shule bila kuelimika.
    Kama hawajaona dalili kuwa wnanchi wamechoka na ubabe wao, the mimi nawashangaa sana. Alama za nyakati zinaonyesha wazi kuwa sasa hivi kuna volcano inayongojea kufumuka nchini mda wowote, na uamuzi usiokuwa wa busara kuhusu katiba ya nchi unaweza kuwa chanzo cha kuifumua hiyo volcano.
    Na siku hiyo volcano ikilipuka hapatakuwa na nguvu zozte za kuizuia. Sanasana watu wengi watapoteza maisha yao na mali zao. Kuirejesha nchi kwenye amani itachukua mda refu sana.
    Na hii ikitokea. historia haitamsamehe JK, Kombani, Warema na Makinda.
    Moshi umeanza kufuka bado moto tu, na inaelekea hawa ndio watakaohusika kuuwasha huo moto.
    Ewe Mungu iepushe nchi yetu na balaa hii.
    Amen

    ReplyDelete
  20. Jambo lililo jema ni kuwa watu wengi wenye upeo mkubwa wa fikra ikiwa ni pamoja na wasomi, wanaharakati, majaji wastaafu, wafanyakazi, wanavyuo, wameonesha wazi kutokuridhishwa na taratibu na maudhui ya sheria hii. Rais na hata wabunge wa CCM wanajua kabisa kuwa mswada huu una kasoro nyingi lakini wanatumia umbumbu wa Watanzania wengi kwa faida ya CCM. Kama unatafuta uwepo wa mizania ya usawa na haki, na katiba iliyo njema, mswada huu hauna sifa hata chembe ya kutuelekeza huko. Kinachofuatia baadaye ni kanuni tu lakini katiba yenyewe ni huu mswada. Maana mswada huu utakapokuwa sheria, ndiyo unaoelekeza tume itachaguliwa vipi, nani atachagua, watu wa namna gani, bunge la katiba litakuwaje, nani watakuwa wabunge wa bunge la katiba, kura ya maoni itapigwa vipi, na nani atasimamia kura ya maoni. Hakuna mahali popote Duniani ambapo katiba inaandikwa na mtu mmoja yaani Rais. Kufuatana na mswada huu, katiba hii kwa sehemu kubwa itakuwa imeandaliwa na Rais, wananchi wanakuwa kama washauri tu. Rais ndiye anachagua watu wake wa kukusanya maoni, wakikusanya wanamletea yeye, yeye ndiye ataamua kitu gani kipelekwe kwenye bunge la katiba, wajumbe wenyewe wa bunge la katiba anachagua yeye, yeye kwa kupitia tume yake ndiye anayeandaa rasimu - wananchi watakapopelekewa watakachotakiwa kukipigia kura ni NDIYO au HAPANA. Huu upuuzi unaweza kufanyika Tanzania tu lakini si mahali popote ambapo kuna wananchi wenye akili.

    ReplyDelete
  21. Wanaharakati NKYA,MALYA,KUNA MWINGINE YUKO TUCTA KAJIFICHA NAYE NI KATIKA HAOHAO JAMAA WA KILIMANJARO. HEBU TUWACHUNGUZE MAISHA YAO WANAYOISHI HAWA JAMAA NI YA ANASA KAMA YA HAO WANAOWAPINGA AU NI KAMA YA KINA MAHTAMA GHANDI ALIYEISHI KIMASIKINI KUWATETEA WANYONGE WA INDIA? MTANZANIA CHUNGA SANA,USIKATAE WITO WA KUSHIRIRIKI ILA KATAA KAMA MAONI YAKO KAMA HAYAJAZINGATIWA YATAKAPOPITISHWA WAKATI WA KURA YA MAONI. MTU HAKATAI WITO HUKATAA ANALOAMBIWA. HAWA WANAHARAKATI WANAKULA MABILIONI YA MAPESA KUTOKA KWA WAZUNGU ILI KUENDESHA SHUGHULI ZAO AMBAZO HAWAZIOFANYI ILA WANAJITAJIRISHA WAO NA FAMILIA ZAO SASA INAPOFIKA MAHALI KAMA H APO KWENYE KATIBA NDIPO WANAJITOKEZA KUWATHIBITISHIA WAZUNGU KUWA WANAFANYA KAZI.NENDENI MAHAKANI NA POLISI MUONE DHULUMA ZINAZOFANYWA HUKO KWA WATU WASIO NA KIPATO,HAWA JAMAA HAWAONEKANI HUKO,WANANGOJEA KUWATUMUMIKIA MABWANA ZAO WA ULAYA NA CHADEMA KAMA HIVYO KUANDAA MAANDAMANO. MLAANIWE NA HIZO PESA ZIWE NDIO MOTO WENU WA KUWATEKETEZA.

    ReplyDelete
  22. Kama akili zimegandamana kama zege , mtasema na kuwaelewesha , watabaki hivyo hivyo , hadi siku watakapoona nchi inageuka kuwa MISRI, NDIPO WATAZINDUKA. Sasa hawajui wala kuelewa kazi yao ni kubishia mambo yaliyo dhahiri, katiba siyo ya RAIS ni wananchi, hebu fikiria LIBYA masikini Gadafi yuko wappi?umeme bure, ukioa serikali inakuchangia, mafuta ya gari serikali inalipa asilimia kadhaa,na mambo mazuri chungu mzima tunayoyatabikia TZ, serikali ya Gadafi iliwafanyia watu wake, lakini walifika mahali wakasema " IMETOSHA" sembuse sisi masikini tuliokalia kigoda cha dhahabu tukiwa tumeshika bakuli lililosukwa kwa makuti kuomba-omba. hizo ndo alama za nyakati , kwa kuanzia ndo huku kwenye katiba, tuiandike mpya itakyoondoa viraka vya kuleana , kiongozi akiiba analelewa tu, nashangaa mtu aanaelaumu wanaharakati.Ujue katiba ukiikosea mwanzo ndio umekuwa mtumwa wa maamuzi yako kwa muda usioujua.

    ReplyDelete
  23. Wewe pumba unayozungumzia Misri na Ghadaffi. Zungumza ya Kilimanjaro wanavyohujumu uchumi wa nchi hii na iko siku watu watasema inatosha tutawashughulikia. unasema akili zimegandana kama zege zako je umezipima huenda wewe ni kichaa kabisa.

    ReplyDelete
  24. TUSICHEZE KAMALI KUPATA KATIBA MPYA NI JAMBO LA MSINGI SANA INABID TUJIVUNIE KUWA TANZANIA KWAN NCHI YETU INAKILA KITU ILA HATUJAPATA MUONGOZO MZURI[KATIBA ] JAMBO ZURI HALIHTAJI PAPALA WANAOFANYA PAPALA KUTUNGA KATIBA YA NCHI SIO WAZALENDO TUWE MAKINI WATANZANIA SALA NA MAOMBI NDIO SILAHA YA KUJIPATIA KATIBA NZURI NA YENYE MANUFAA KWA KILA MTANZANIA.

    ReplyDelete
  25. tuchambulieni kwa kina mswada kabla ya kushawaishi maandamano.mswada hauonekani.mliouona tuonesheni umekosewa wapi?hebu tumieni gharama kuuweka hadaharani na mapungufu yake na lipi lingekuwa mbadala wake.basi kwa kufanya hivyo mtapata kibali cha wananchi kushiriki maandamano hayo

    ReplyDelete