17 October 2011

'Taja wauaji albino upate mil.5/-'

Na Waandishi Wetu, Mwanza

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema ametangaza bingo ya sh. milioni tano kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa ya watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya walemavu
wa ngozi (Albino) pamoja na wale wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya vikongwe.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Bw. Liberatus Barlow alisema amepokea taarifa kutoka kwa IGP Mwema jana kwamba awatangazie wananchi wa mkoa huo kuwa yeyote atakayetoa taarifa ya watu wanaojihusisha na mauaji hayo na kufanikisha kutiwa nguvuni atapokea zawadi ya sh. milioni tano kutoka Jeshi la Polisi.

Ahadi hiyo ya IGP Mwema imekuja siku moja baada ya mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyangh'wale B iliyoko wilayani Geita, Bw. Adam Robert (14 kunusurika kuuawa baada ya kukatwa vidole vitatu.

Mwanafunzi huyo alinusurika kifo baada ya mtu mmoja ambaye hadi sasa anatafutwa na polisi kufika nyumbani kwa Bw. Robert akidai kuwa alikuwa anatafuta ng'ombe wake ambaye inadaiwa kuwa aliibwa na kundi la watu na kufichwa nyumbani kwa Bw. Robert.

Akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari, Kamanda Barlow alisema baada ya mtu huyo kupelekwa kwenye zizi la ng'ombe na kufanya ukaguzi na kugundua kuwa hakukuwa na ng'ombe wake kama alivyodai kufichwa katika zizi hilo alipatiwa hifadhi ya kulala katika mji huo na wakati wa usiku mgeni huyo alipewa hifadhi zote ikiwemo maji ya kuoga na kushiriki na Bw. Robert chakula cha usiku.

Kamanda Barlow alisema baada ya mgeni huyo kupatiwa chakula cha usiku majira ya saa moja, Baba mtoto huyo, Bw. Robert aliondoa vyombo kupeleka jikoni na nyuma yake alisikia kilio cha mtoto wake aliyemtaja kuwa ni Adamu akilia kuomba msaada kwamba anashambuliwa na mgeni kwa kutumia panga.

Kwa mujibu wa Kamanda Barlow, Bw. Robert alirudi na kukuta mtoto analia huku akiwa tayari amekatwa vidole vitatu vya mkono wa kulia kuanzia kidole gumba huku akiwa amejeruhiwa mkono wa kushoto majeraha ambayo yalisababishwa na kukatwa na panga.

Kamanda Barlow alisema muuaji huyo hadi sasa anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi mbalimbali wilayani Geita na kuwataka wananchi kuondokana na imani potofu kwamba viungo vya albino vinaweza kuwaletea utajiri.

"Hivi kweli viungo vya albino vinaweza kuleta utajiri gani? Mbona nchi ya Afrika Kusini ambako ndiyo nchi ya kwanza katika uchimbaji dhahabu kusini mwa Afrika imekuwa na utajiri mkubwa kutokana na madini ya dhahabu lakini hawatumii viungo vya albino," alihoji Kamanda huyo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Under The Same Sun ambalo linajishughulisha na kutetea haki za Albino, Bi. Vick Ntetema, alilaani na kukemea vitendo hivyo vya kuwinda walemavu hao kama wanyama pori na kuongeza kuwa shirika lake liko bega kwa bega na serikali katika kukomesha vitendo hivyo.

Wakati huo huo Mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Evarist Ndikilo alisema hayuko tayari kupokewa na kashfa za ukatili ya mauaji ya albino na kuagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kuhakikisha wahusika wanakamatwa mara moja.

"Hili ni tukio la kusikitisha na mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza siko tayari kupokelewa kwa taarifa za mauaji ama ukatili dhidi ya albinio, siko tayari kabisa," alisisitiza Mkuu huyo wa mkoa.

No comments:

Post a Comment