09 September 2011

Kivumbi chatimka jimboni Igunga

*CUF sasa yakata rufaa NEC dhidi ya CCM, CHADEMA
*CHADEMA waanza kampeni kwa kuwavaa Mkapa, Kafumu
*Mkapa atamba akisema kazi ni moja tu ni kushinda


Na Waandishi Wetu, Igunga

CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimeendelea kuwakomalia wagombea wa CCM na CHADEMA kwa kukata rufaa dhidi yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa
madai kuwa ni watumishi halali wa umma hivyo hawastahili kuwania kiti hicho.

Rufaa ya CUF inakuja siku moja tu baada ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo Bw. Protace Magayane, kutupilia mbali pingamizi la awali la chama hicho dhidi ya  wagombea ubunge wa CCM na CHADEMA.

Akiwasilisha rufaa hiyo jana saa 8.30 mchana, mgombea ubunge wa CUF Bw. Leopold Mahona, akifuatana na mwanasheria wake ambaye pia ni Ofisa wa Haki za Binadamu na Sheria wa chama hicho Bw. Hashim Mziray, alisema anamini haki itatendeka kwa kuondolewa kwa wagombea hao.

Alitaja sababu za rufaa hiyo kuwa ni Dkt. Peter Kafumu (CCM) ni mfanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini na huku mgombea wa CHADEMA Bw.Joseph Kashindye, akiwa Mkaguzi wa Shule Wilaya ya Igunga.

"Tumewasilisha rufaa yetu kwa sababu msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Igunga, ameshindwa kuwaengua Dalaly wa CCM na Kashindye wa CHADEMA kwa sabau bado ni waajiriwa wa Serikali. Kutokana na Ibara ya 72 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wagombea hawa wanatakiwa kuenguliwa," alisema Bw.Mziray.

Ofisa Uchaguzi Jimbo la Igunga Bi. Martha Bayo alipokea rufaa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa uchaguzi wa jimbo hilo Bw. Magayane na kuahidi kuwa itashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo Bw. Protace Magayane ametupia mbali pingamizi la CUF kutaka wagombea Ubunge wa CCM na CHADEMA waenguliwe kwa madai kuwa ni watumishi wa serikali na bado hawajaandika barua ya kujiuzuru nyadhifa zao.

Akiwa katika Kijiji cha Igurubi ambapo alianzia kampeni zake jana, mgombea huyo alitaja barabara inayotoka kijijini hapo hadi mjini Igunga na daraja la mto Mbutu kuwa kipaumbele chake cha kwanza iwapo atachaguliwa na kuomba siku 400 tu baada ya uchaguzi kukamilisha ahadi hiyo iwapo atachaguliwa.

Alisema Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, Rais Jakaya Kikwete na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Bw. Rostam Aziz, waliahidi kujenga barabara hiyo na daraja la mto Mbutu bila mafanikio.

Alisema ana uchungu mkubwa na daraja hilo la mto Mbutu kwa madai kuwa ndugu zake wawili pia walipoteza maisha wakati wakivuka mto huo hivyo ni lazima awakomboe wananchi hao na adha hiyo ya muda mrefu.

CHADEMA wazindua kampeni

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe, amezindua rasmi kampeni za chama hicho kwa kumnadi mgombea wake Bw. Joseph Kashindye huku akiweka wazi kuwa CCM imefikia hatua za mwisho kufa.

Akihutubia umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza jana Bw. Mbowe alisema umati huo ni ushahidi tosha kuwa huo ndio ukweli kwa kukubalika kwa chama chake na kwamba kitashinda kiti hicho.

Alisema mgombea huyo ni risasi nyingine bungeni hivyo kuwataka wananchi kumchagua ili akaongeze nguvu bungeni na kwamba umasikini ambalo sasa ni janga la taifa halikuletwa na Mungu bali CCM.

Alisema nchi hivi sasa inatawaliwa na wageni kutoka nje na kwamba taifa limegeuka kuwa ombaomba huku kila mmoja akilalamika na kwamba ni aibu kwa serikali kuomba vyandarua vya mbu nje.

Akitoa takwimu alidai, wakati Rais wa awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, anaondoka madarakani serikali ilikuwa inakusanya bilioni 25 kwa mwezi na kwamba maisha ya mtanzania yalikuwa nafuu kuliko sasa.

Alisema mafuta ya taa kupandishwa bei ni aibu kwa  serikali kushindwa kusimamia sheria na kuwataka wana Igunga kuichagua CHADEMA.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Willibrod Slaa, alimshukia vikali Dkt. Kafumu na Rais mstaafu wa awamu ya Benjamin Mkapa, akidai  wamekuwa wakisimamia ufisadi ndani ya serikali kwa nyakati tofauti.

Alisema Dkt. Kafumu alishindwa kujiuzulu kutoka Wizara ya Nishati na Madini akidai kuwa wizara hiyo imegubikwa na kashfa ya rushwa na yeye anafahamu.

Alidai Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa kwa akimtuhumu kuwa alifanya biashara akiwa Ikulu kwa kuanzisha kampuni ambayo alidai ilimnufaisha yeye binafsi chini ya mwamvuli wa Ikulu. “Akija hapa mdaini pango kwa kuwa alifanya biashara akiwa Ikulu wakati ile ni mali
ya wananchi,”alisema Dkt. Slaa.

Alisema kuwa Dkt. Kafumu amekuwa akidai kuwa anapigana na ufisadi lakini huku ni kuwadanganya wananchi kwa kuwa alipaswa ajiuzulu kutokana na tuhuma za rushwa zilizoikumba wizara yake hasa katika sekta ya madini.

Dkt. Slaa aliwataka wananchi hao ambao walikuwa wamefurika katika uwanja wa Sokoine kumchagua Bw. Joseph Kashindye ili aweze kulinda rasilimali za Wana Igunga katika Halmashauri ili kupunguza panya waliopo wanaozitafuna.

Kwa upande wake Bw. Kashindye alisema ameamua kuacha ualimu ili kufuata nyayo za Baba wa taifa Mwalimu Julias Nyerere,aliyeacha ualimu kuwasaidia watanzania na yeye ameamu kuacha ualimu ili kutetea maslahi ya wana Igunga Bungeni.

Alisema fedha zilizokuwa zikipalekwa jimboni umo ilikuwa zimekuwa zikitumika vibaya na kwamba yeye akichaguliwa atazifuatilia huku akitoa mfano kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na Hesabu za Serikali (CAG) alibaini wizi wa sh. bilioni tatu mwaka huu.

Mkapa atua na kutangaza ushindi wa CCM

Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Benjamin Mkapa, aliwasili mjini Igunga jana
jioni na kutangaza rasmi kwamba kazi yake ni moja nayo ni kuitangazia CCM ushindi kwa kuwa ina cha kujivunia.

Rais Mkapa ambaye alisafiri kwa njia ya barabara kwa kile alichoita kuwa ni kutaka kukagua maendeleo makubwa yaliyofikiwa hivi sasa ndiye atakayefungua kampeni za CCM za Jimbo la Igunga
jumamosi.

"Nimewasili Igunga, wana Igunga kazi ni moja, ni ushindi tu," alisema Rais Mkapa wakati akisalimiana na wananchi baada ya kupokelewa katika kijiji cha Makomero kilometa
nane kutoka mjini Igunga.

"Nashukuru sana kuona kwamba mara hii nimefika hapa Igunga kwa kupita barabara ya lami, mara ya mwisho nilipita kukiwa vumbi tu, jamani haya si
maendeleo? alihoji Rais Mkapa huku akishangiliwa na wananchi.

Mkapa aliwataka wananchi wa Igunga kujitokeza kwa wingi Oktoba 2 mwaka huu kupiga kura na kuhakikisha wanampigia mgombea wa CCM Dkt. Peter Kafumu na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wamechagua maendeleo. "La msingi ni hilo mengine nitawaambia tutakapokutana katika mikutano ya kampeni, yapo mengi sana," alisema.

Msafara wa Mkapa ulipokelewa na magari yaliyozungukwa na vijana waendesha pikipiki na baiskeli. Kabla ya kuzindua kampeni za CCM katika viwanja vya Kumbukumbu ya Samora mjini Igunga leo Mkapa atakuwa na shughuli mbalimbali za kampeni na baada ya uzinduzi wa kampeni hizo ataendeleo na mikutano kesho yake.
Imeandaliwa na Peter Mwenda, Benjamin Masese na Moses Mabula

10 comments:

  1. BARABARA HIZO ZIMEJENGWA NA PESA ZA KODI ZA WANANCHI WOTE CHADEMA, TLP,CUF, CCM NA WASIO NA VYAMA NI AIBU KWA MZEE MKAPA KUSEMA CCM NDIO ILIJENGA WAKATI NI PESA ZA KODI ZA WANANCHI WOTE ZILITUMIKA KWENYE KUJENGA BARABARA NA WANANHCI NDIO WANAOSTAHILI PONGEZI KWANI BILA WAO BARABARA ISINGEKUWEPO NA SIYO CCM.

    ReplyDelete
  2. Ni mipango ya ccm kuhakikisha ujenzi wa barabara nchi nzima sio huko tu ni nchi nzima na sio suala hata wa chadema wanalipia kodi ya ujenzi. EEEEE MUNGU SHINDA HAO MAJANGILI YA KICHAGA NCHI HII IKISHIKWA NA HAO TUTAANGAMIA

    ReplyDelete
  3. CCM OYEE, CCM ITASHINDA KWA KUWA INASTRATEGY

    ReplyDelete
  4. Pole Bw.Mohamedi kwa kutokuelewa kazi ya chama kuongoza serekali .Viongozi wanateuliwa na chama kuratibu na kufanikisha sera zote za chama kwa manufaa ya Watanzania wote,ningependa uelewe Ccm i nasimamia na kila jema lazima ijisifie nami pia naipongeza kwa hilo,vyama vya upinzani hamuna sera ya kuishinda CCM watu wote wanalipa kodi serekalini hawapeleki ccm na serekali ipo sambamba na utawala wa CCM,hayo ndio matokeo yakutokuelewa siasa haya we loloma na sema KIDUMU CHAMA CHA AMANI KIITWACHO CCM

    ReplyDelete
  5. Ccm bado itabaki kuwa Ni Chama Cha Wezi hata mpinge. Kwa MTU mwenye akili timamu huwezi kushabikia upuzi kama wa Mkapa. Hata Mkapa hana aibu. Matatizo haha yote wameyaleta wao. CCM Ni sifuri kabisa hata ikishinda bado Ni Chama cha Wezi na Mafisadi. Msijikaze kutetea kwa unafiki huku watu wanateseka.

    ReplyDelete
  6. Huyu jamaa anyetetea CCM lazima ni mwizi. Na atahukumiwa kwa hilo na kwa sababu ya ubinafsi wake.

    E mungu msaidie uelewa huyu mp umbavu wa ccm

    ReplyDelete
  7. Mimi ninawashangaa watu wanaposhindwa kuona mambo mema ambayo selikari yetu kwa uongozi wa viongozi waliopita na wale waliopo sasa madarakani(sisemi ya kwamba wote wamefanya istahilivyo) kwani binadamĂș ni binadamu tu hawezi kuwa bila upungufu. Mema na mapungufu ya uongozi chini ya CCM mimi nimeyaona. Miaka 50 ya Uhuru wetu inaonyesha wapi tulipotoka na wapi sasa tupo na pia kuna mtazamo wa wapi tunapokwenda. Nawashangaa watu wanaoiponda nchi yetu na kujaribu kulinganisha eti na nchi nyingine kwa hili au lile. Marekani walipata uhuru wao miaka 200 iliyopita lakini hata leo nao wanahangaika na hali ya uchumi na hata umasikini. Mataifa mengi mengine hata nchi za Ulaya zina matatizo yake. Serikali ya Ugiriki imefanya kuomba mkopo maana nayo ilipungukiwa ; Wagriki si walianza hata kuandika mapema zaidi ya sisi. Wana Igunga msisikie mambo ya ushabiki wa vyama chagueni mtu atakayesimama pamoja nanyi kutafuta maendeleo ya Igunga na nchi yetu. Na yule mtakayemchagua basi mjue ya kwamba ni mwanadamu kama ninyi tena mshirikiane naye na hata kukosoa pale aendapo mrama. Hata hivyo naipongeza CCM kwa yale mema iliyoyafanya na kwa yale mapungufu rekebisheni.

    ReplyDelete
  8. ccm itazamishwa! imechoka na imetawaliwa na ufisadi na udhaifu katika kuukemea ufisadi.

    ReplyDelete
  9. Rostam kama alifanya mazuri ni kwanini alijiuzulu ubunge Igunga?
    CCM kama inajiamini ni kwanini inamtumia Mkapa kumnadi mgombea wake Igunga?
    Fedha za kodi za Watanzania ndiyo zilitumika kuijenga Igunga Kiufisadi! Tunahitaji chadema Ikazisimamie raslimali za Wananchi Igunga zilizoporwa maeneo mbalimbali ya nchi na Rostam pamoja na chama chake.

    ReplyDelete
  10. Ananymous Said mwanzo wa hoja zako nilidhani kuna mantinki ndani yake lakini kadiri unavyoendelea ndivyo unavyo zidi kupolomosha pumba, kwani unanataka kuniambia huelewi ni kwa sababu zipi ziliozo pelekea kufanyika kwa ucha guzi huo mdogo wa Igunga kweli unataka kuniambia kuwa hujuwi ni kwa sababu ya wengine kuona wenzao wanawazidi kwa matone?

    ReplyDelete