30 September 2011

Ajali yaua tisa Mbeya

Esther Macha, Mbozi

WATU tisa (9) wamekufa papo hapo na wengine 12 kujeruhiwa vibaya kufuatia ajali mbaya iliyohusisha basi dogo la abiri aina ya Toyota Hiace lenye namba za
usajili T 219 ASQ kugongana uso kwa uso na gari aina ya Landcruiser(Prado) T 155 ACQ katika barabara ya Mbeya-Tunduma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Bw. Gabriel Kimoro alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 1:30 jioni katika Kijiji cha Chimbuya, Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.
 
Alisema dereva aliyekuwa akiendesha basi alishindwa kulimudu gari hilo kutokana na mwendo kasi na hivyo kuanza kuyumba kutoka upande wake hadi upande wa pili ambako aligongana uso kwa uso na gari hilo lililo kuwa likielekea Tunduma kutokea Mbeya.
 
Mkuu wa Wilaya aliwataja waliokufa na ambao wametambuliwa na ndugu zao kuwa ni Anna Mbembela na mwanaye Mariam Mrema na Rahabu Mwaijumba na mwanaye Leah Said.
 
Wengine ni Binaisa Mwashiuya, Baraka Mwansite na dereva wa basi Charles Kumbi. Bi. Agness Mpoli alifia njiani wakati akikimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.
 
Alisema majeruhi wa ajali hiyo ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya Vwawa ni Frank Simbeye (25) mkazi wa Chimbuya ,Emmanuel Sanga (16) mkazi wa Mlowo, Agness Anthony (28) mkazi wa Mbeya na wanawe wawili, Jackiline Christopher na Victor Christopher.
 
Majeruhi wengine ni Anastazia Mtumbo (19) mkazi wa Tunduma na Richard Ezekiel ambaye ni mtoto wa miezi 10 na Chenny Mwembe (25) mkazi wa Chimbuya.

Watu walioshuhudia ajali hiyo walidai kuwa Prado ilikuwa likiendeshwa na mmiliki wake, Emmanuel Kaila ambaye amelazwa katika Hosptali ya Sifika mjini Vwawa akipata matibabu kutokana na kujeruhiwa vibaya.
 
Walisema kuwa katika eneo hilo kulikuwa na trekta ambalo lilikuwa limebeba tanki la maji ambalo halikuwa na taa na dereva wa basi dogo alitaka kulipita.

Kwa upande wake Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya, Bw. Advocate Nyombi alithibitisha kutokea kwa ajali na kusema kuwa suala la la ajali ni la wadau wote kushirikiana ili ajali hizo zipungue.

Aidha alisema kuwa Mkoa wa Mbeya umekuwa na ajali nyingi, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa tatizo la ajali linapungua haraka.

No comments:

Post a Comment