15 July 2011

Uongozi TAFIRI walalamikiwa kukamata gari la mfanyakazi

Na Jovin Mihambi, Mwanza

MFANYAKAZI wa Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), mkoani Mwanza, Bw. Mayalla Kachwele, ameulalamikia uongozi wa taasisi hiyo kukamata gari lake aina ya
Toyota Mark II, yenye namba za usajili  T 441 AHZ kinyume na taratibu.

Akizungumza na Majira juzi, Bw. Kachwele alisema Agosti 2009, alinunua gari hilo na kupata vielelezo vyote ikiwemo kadi ya gari na nyaraka zote kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema gari hilo alilisajili kwa ajili ya biashara ya teksi na kuomba kibali kwa uongozi wa TAFIRI ili kulaza gari hilo katika eneo la taasisi.

“Nilishtushwa na uongozi wa taasisi kunituhumu kuwa nimehusika na wizi wa zaidi ya sh. milioni 10 ambazo zilidaiwa kuingizwa katika akaunti ya mshahara wangu kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam na kudai fedha hizo ndizo zimetumikia kununulia gari yangu” alisema.

Alisema ni kweli kuna fedha iliyoingia katika akaunti yake ambazo hazihusiani na fedha za taasisi hiyo ambapo suala hilo, lilipelekwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani hapa na Jeshi la Polisi ambao baada ya kufanya uchunguzi wao, walisema hakukuwa na ushahidi wowote wa kumtia hatiani hivyo iliamuliwa apewe gari lake.

Aliongeza kuwa, wakati suala hilo likifanyiwa uchunguzi, uongozi wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa Benki NBC, walichota fedha zaidi ya sh. milioni 2.8 katika akaunti yake na hadi sasa fedha hizo hazijulikani zilipo.

“Nauomba uongozi wa TAFIRI Makao Makuu Dar es Salaam, kuingilia kati suala hili ili niweze kupata gari langu ambalo uongozi wa taasisi Mkoa, unalishikilia bila ushahidi wowote unaoonyesha kuna fedha zimeibwa kutoka taasisi hiyo kuanzia makao makuu hadi mkoani hapa.

Kwa upande wake, Ofisa mmoja kutoka Makao Makuu ya taasisi hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kusema kuwa hakuna fedha yoyote iliyoibwa katika mishahara ya Septemba 2010.

Ofisa Utumishi wa taasisi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Asmala Beleko, alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo kutoka kwaBw. Kachwele na kusema suala hilo linamngoja Mkurugenzi wa
TAFIRI kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam ili aweze kulipatia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment