18 July 2011

UN yatoa misaada Somalia

MOGADISHU,Somalia

UMOJA wa Mataifa UN kwa mara ya kwanza umepeleka misaada katika maeneo yanayokabiliwa na ukame nchini Somalia  ambayo yapo chini ya udhibiti wa  wanamgambo wa
kikundi cha kiislam, Al Shaabab ambacho kinasadikika kuwa na mahusiano na mtandao wa kigaidi wa  al-Qaeda tangu kilipoondoa vikwazo vya misaada nchini humo.

Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mtaifa UNICEF Bi. Rozanne Chorlton alisema jana kuwa msaada huo umetolewa baada ya wapiganaji wa al-Shabab kuahidi kuwapa ushirikiano wafanyakazi wa UN na akasema kuwa hatua hiyo itayashawishi mashirika mengine kutoa misaada hiyo ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa UNICEF,ndege za shirika hilo zimeshawasili katika  mji wa Baidoa,uliopo umbali wa zaidi ya kilometa 200 kutoka katika mji mkuu wa  Mogadishu zikiwa na shehena za chakula na madawa.

Bi.Chorlton ambaye ni mwakilishi wa UNICEF nchini humo alisema kuwa wanamgambo wa al-Shabab wameshawakikishia kuwa shirika hilo litaendesha shughuli zao bila kuingiliwa.

Hatua hiyo imekuja wakati Uingereza ikiahidi kutoa msaada wa pauni milioni 52.25 kama msaada wa dharura katika maeneo yote yaliyokumbwa na ukame.

Hata  hivyo Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya misaada aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza  BBC kuwa nchi yake haitahusika na wanamgambo hao wa al-Shabab ambao wanadhibiti eneo kubwa la  Somalia.

Waziri huyo wa misaada, Bw. Andrew Mitchell yupo ziarani kutembelea kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Kenya ili kujionea jinsi ukame ulivyosababisha janga kubwa katika pembe ya Afrika ambalo halijawahi kuonekana katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ambapo inakadiliwa kuwa watu takribani milioni 10 wameathirika kwa janga hilo.

Wanamgambo wa Al-Shabab,ambao wanashikilia eneo kubwa katikati na Kusini mwa Somalia walipiga marufuku mashirika yote ya misaada ya kigeni  miaka miwili iliyopita wakiyashutumu kwa kupinga Uislamu kabla ya kuondoa marufuku hiyo siku kumi zilizopita.

"Wametuhakikishia kuwa shughuli zetu zitaendeshwa bila kuingiliwa na hivyo ni kwamba tutaweza kuwafikia watu wote ambao wanahitaji msaada muhimu,"Bi. Chorlton aliiambia BBC.

No comments:

Post a Comment