22 July 2011

TFF yasita kutoa kibali cha Mgosi

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), imetuma maombi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji Mussa Hassan 'Mgosi' wa Simba, ili aichezee timu hiyo katika mashindano mbalimbali,  lakini TFF imesita kutoa hati hiyo.

Hatua hiyo imetokana na TFF, huenda kuingiwa na wasiwasi kwa kuwa,  Motema Pembe imeomba hati hiyo ikionesha Mgosi ni mchezaji wa ridhaa, huku wakisema wamekubaliana kila kitu na Simba,  jambo ambalo shirikisho hilo limeahidi kwanza izungumze na Simba, ndipo watoe kibali hicho.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema klabu hiyo imetuma maombi hayo kupitia Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu ya nchi hiyo (FECOFA), hivyo TFF kabla ya yote imeaanza kufanya mazungumzo na Simba, na ndipo ifikie uamuzi wa kuitoa.

"Klabu hiyo imetuma maombi hayo ikimwombea Mgosi kama mchezaji wa ridhaa na sio Proffesional kama ilivyozoeleka, hivyo ni lazima kwanza tuwasiliane na Simba, na baada ya hapo tutajua kitakachofuata," alisema Wambura.

Walipotafutwa viongozi wa Simba kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala, kupitia siku yake ya kiganjani alidai yupo benki, hivyo apigiwe baadaye, lakini hata hivyo hiyo baadaye alizima simu.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, simu yake ya kiganjani iliita zaidi ya mara tano bila kupokelewa.

Mbali na hilo, Wambura alisema klabu zote 14 za Ligi Kuu ya Bara zimewasilisha usajili wa wachezaji wao kwa ajili ya ligi hiyo iliyopangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20, mwaka huu.

Alisema juzi saa sita usiku, ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha majina hayo na kwamba, klabu za Ruvu JKT Stars, Oljoro JKT na Kagera Sugar, ndizo zilikuwa za kwanza kuwasilisha, ambapo zilileta saa tisa alasiri).

Alisema baada ya timu hizo kuwasilisha, timu nyingine ziliendelea kumiminika, ambapo Simba ilipeleka saa 1.30 usiku, na saa tatu baadaye Yanga iliwasilisha na Coastal Union ndio klabu ya mwisho kufanya hivyo ambapo iliwasilisha saa 5.58, dakika mbili kabla ya suala hilo kufungwa.

No comments:

Post a Comment