21 July 2011

Pinda: Sina taarifa kujiuzulu kwa Jairo

Na Gladness Mboma, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amesema kuwa hana taarifa zozote za kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. David Jairo anayehusishwa na vitendo
vya rushwa katika upitishwaji wa bajeti ya wizara hiyo.

Bw. Pinda alieleza hayo jana mjini hapa alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua maonesho ya vifaa vya maabara katika viwanja vya bunge.

“Sina taarifa zozote, nami nimeona kwenye gazeti labda amepeleka barua hiyo huko,” alisema.

Jana kulikuwa na taarifa tata kwenye vyombo vya habari, baadhi vikisema Bw. Jairo amejiuzulu, huku vingine vikimkariri akisema  kwa sasa si wakati mwafaka kwake kusema chochote kuhusu tuhuma hizo wala kama ana mpango wa kujiuzulu au la.

lakini gazeti moja la kila siku jana liliandika habari kwa uzito mkubwa likisema tayari Bw. Jairo alikuwa amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumwomba ajiuzulu kutokana na kashfa dhidi yake.

Tuhuma za Bw. Jairo kuhusishwa na vitendo vya rushwa, ziliibuliwa bungeni na Bi. Beatrice Shelukindo (CCM) baada ya kuwasilisha barua iliyoonesha Bw. Jairo akizitaka taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kushanga sh. milioni 50 kila moja (jumla sh bilioni 1) kwa ajili ya kutoa kuwalainisha watu mbalimbali ili bajeti ya wizara hiyo ipitishwe na bunge.

Fedha hizo zilitakiwa kutumwa Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye akaunti namba 5051000068 iliyopo benki ya NMB, tawi la Dodoma.

Sehemu ya barua hiyo inasomeka: “Kama ilivyo wakati wa kuwasilishwa hotuba ya bajeti, maofisa mbalimbali wa wizara na taasisi zilizo chini yake huambatana na viongozi waandamizi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala yanayojitokeza wakati wa mjadala wa hotuba hiyo.

“Ili kukamilisha mawasilisho ya hotuba hiyo, unaombwa kuchangia jumla ya sh 50,000,000. Fedha hizo zitumwe Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye akaunti namba 5051000068 iliyopo benki ya NMB, tawi la Dodoma. Baada ya kutuma fedha hizo, wizara ipewe taarifa kupitia ofisi ya DP kwa uratibu,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Kutokana na tuhuma hizo, Waziri Mkuu, Bw. Pinda alikiri kuwa ni nzito na kutoa hoja ya kuondoa bungeni hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo.

Baada ya kuondoa hoja hiyo, wizara hiyo sasa inatarajiwa kuwasilisha bajeti yake Agosti 13 mwaka huu.

6 comments:

  1. Kwa upande wangu sijaona tuhuma zozote za rushwa kwenye barua hiyo kwani kinachoonekana hapa ni tafasri binafisi kuwa pesa hizo zilitarajiwa kuwalainisha wabunge jambo ambalo barua hiyo haijasema hivyo. Nikweli nikawaida ya wizara zote wakati wa kupitishwa kwa bajeti ya wizara husika maafisa kutoka ktk wizara husika humiminika Dodoma kwa ajiri ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayojitokeza ni ukweli usiopingika kama barua hiyo inavyojaribu kusema. Hakuna hata sehemu iliyotaja wazi kuwa wabunge watapewa kiasi hicho cha pesa, sana sana tunachoweza kuhoji ni matumizi mabaya ya kiasi hicho cha pesa lakini rushwa is too remote to be invoked at this stage.

    ReplyDelete
  2. wacha ufisadi wako wewe,huoni kama ni rushwa hiyo. hiyo Geological survey na wizara zinhusiana nini na hizo pesa amepewa nani.
    acheni kuturudisha nyuma kila siku kwa kuwa umeshiba rushwa unajenga hoja haina miguu wala kichwa thats ufisadi tu, think of Poor tanzanians....

    ReplyDelete
  3. Mchangiaji wa mwanzo usituzingue. Zingatia:

    +Kifungu gani cha sheria kimempa Katibu Mkuu huyo kuchomoa fedha kwa makampuni yaliyo chini ya wizara yake.

    +Iwapo imebainika agizo hilo ni halali, kwa nini fedha hizo zisiwekwe kwenye akaunti ya Wizara.

    + Iikigundulika agizo hilo ni halali, lazima libadilishwe maana linaingiliana na utendaji na uwajibikaji

    ReplyDelete
  4. Weye mchnagikaji wa pili ndo mbumbu wa mambo ndo wale mnaoendesha endesha tu,ni kweli barua haijazungumzia suala la rusha.
    kinachopaswa hapa ni kweli hizo pesa zilitumika kama ilivyokusudiwa?
    Vilevile ningependa ni mlaumu kidogo waziri mkuu, kwa hali ile sidhani kama alistahili ile nafasi
    labda mniambia tulio sikia kali zake kupitia vyombo vya habari zilipotoshwa ki uhalisia alipaswa atumie busara zaidi na si vile maanake alishahukumu

    ReplyDelete
  5. Wachangiaji wa pili na wa tatu wanaonekana hawajui kuwa wakati wa bunge la bajeti viongozi wa mashirika yaliyo chini ya wizara fulani wanatakiwa kufika bungeni kusaidia kujibu hoja za wabunge.

    Pia hawafahamu kua Geological Survey of Tanzania (GST) ipo chini ya wizara ya nishati na madini na kwa kua bunge linakutania Dodoma hela za matumizi ya wizara na idara hua zinatumwa kwenye akaunti hiyo

    Barua ya David haionyeshi hata chembe kua hizo hela zinachangishwa ili zitolewe kama hongo. Je ni kweli hiyo barua ilikwenda kwenye taasisi 20? Ni uongo mtupu kwa kua wizara hiyo haina taasisi/idara 20.Hebu chunguza kwanza kabla ya kukurupuka kama pinda

    ReplyDelete
  6. Some of those bafoons supporting the apparent theft are as crooked as a snake with a diarrhea. Ukisikia vibaraka wa mafisadi ndio hawa. Lousy bootlickers who warship thieves. The whole lousy ministry is thoroughly corrupt. Period!

    ReplyDelete