31 March 2011

Yanga FC yaitia kiwewe Simba

*Yaichapa Azam mabao 2-1

Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya Yanga, imezidi kuipa presha Simba katika kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu bara, baada ya kuichapa Azam FC mabao 2-1, katika mchezo uliopigwa
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi 43 huku vinara wa ligi hiyo, Simba wakiwa na pointi 45 na Azam ikibaki katika nafasi ya tatu kwa pointi 37.

Kufungwa kwa Azam kumeiweka katika matumaini finyu ya kushika nafasi ya pili na kucheza michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwani imeendelea kubaki nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 huku ikiwa imebakiwa na michezo miwili mkononi ambayo kama ikishinda yote itafikisha pointi 43 ambazo tayari Yanga inazo huku Simba ikiwa imezipita.

Katika mechi hiyo Azam FC ndiyo iliyoanza kupata bao dakika ya tatu lililowekwa kimiani na John Boko aliyeunganisha krosi ya Suleiman Kassim, baada ya uzembe wa mabeki wa Yanga walioufanya wakati wakiwa katika harakati za kuokoa.

Yanga ndiyo ilianza kubisha hodi langoni mwa Azam ambapo dakika ya pili ilifanya shambulizi la nguvu lakini hata hivyo mshambuliaji raia wa Zambia, Davies Mwape alishindwa kutikisa nyavu.

Dakika ya 12, Tegete nusura aisawazishie timu yake baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu na mpira kurudi kati na kuokolewa na mabeki.

Yanga iliendelea kuibana Azam ambayo ilionekana kumuacha Boko peke yake mbele na katika dakika ya 41, Tegete aliisawazishia timu yake baada ya mabeki kujichanganya na kipa Vladimir Niyonkuru akishindwa la kufanya.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuingia kwa nguvu na kutafuta mabao, ambapo dakika ya 56 nusura Yanga wapate bao baada ya kona iliyochongwa na Nurdin Bakari kugonga mwamba wa juu na kumkuta Tegete ambaye alifumua shuti kubwa lililotoka nje ya uwanja.

Juhudi za Yanga zilizaa bao la ushindi dakika ya 60 baada ya Tegete kuipatia timu bao baada ya kukutana na mpira uliotemwa na Niyonkuru ambaye alishindwa kuzuia shuti la Mwape.

Mwamuzi Said Ndege alilazimika kumtoa dokta wa Yanga kwa kadi nyekundu kutokana na kuingia uwanjani na kuanza kuzozana na wachezaji wa Azam FC.

Dakika ya 82 Azam ilikosa bao la wazi baada ya mshambuliaji, Kalimangonga Ongala aliyeingia badala Suleiman Kassim kushinda kuitumia nafasi nzuri ya kufunga.

No comments:

Post a Comment