02 March 2011

Mbunge kusaidia mashindano Klabu Bingwa

Na Amina Athuman

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa, ameahidi kutoa zawadi ya medali 40 kwa mabondia wanaoshiriki mashindano ya ubingwa wa Taifa wa
ngumi za ridhaa, yanayoendelea katika Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

Jumaa ambaye ni mdau wa michezo na bondia wa zamani katika uzito wa middle, jana alikwenda kuangalia mashindano hayo ambayo yanashirikisha timu kutoka mikoa 24 ya Tanzania Bara.

Akiwa katika ukumbi huo, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Meja Mstaafu Michael Changalawe alimweleza changamoto zinazoyakabili mashindano hayo.

Miongoni mwa changamoto alizotajiwa ni pamoja na na ukosefu wa medali kwa mabondia, ambao watafanya vizuri katika uzito tofauti, ukata wa fedha za kuchapisha vyeti kwa timu zote pamoja na zawadi.

"Mimi ni mdau mkubwa wa mchezo huu, changamoto nimeziona hivyo nitahakikisha nazipeleka bungeni, ili uweze kurudisha heshima yake kama ilivyokuwa zamani," alisema Mbunge huyo.

"Nia kubwa ni kuhakikisha malengo yaliyowekwa na BFT yanafikiwa, nitawashawishi wabunge wenzangu waweze kuhudhuria mashindano mbalimbali ya ngumi za ridhaa," alisema.

Alisema mchezo wa ngumi una nafasi kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa kama wadau mbalimbali, wataona umuhimu wa kufadhili mashindano yanayoandaliwa na BFT.

No comments:

Post a Comment