02 February 2011

Shule binafsi wataka matokeo kidato cha nne yafutwe

Na Agnes Mwaijega

CHAMA cha wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya serikali (TAM0NGSCO) wametaka matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2010 yafutwe na
mtihani usahihishwe upya kwa sababu hawakuridhishwa na utaratibu uliotumika katika usahihishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Benjamin Nkonya alisema utaratibu wa usahihishaji wa mtihani kwa mwaka jana haukuwa mzuri kwa sababu ulichukua muda mfupi kutokana na bajeti ya baraza la mitihani kuwa ndogo.

Alisema hali hiyo imetokana na vyanzo vyake vya mapato kupungua baada ya serikali kuondoa ada za mitihani kwa shule zote za serikali, hivyo kulifanya baraza kuwa na uwezo mdogo wa kusimamia kazi ngumu za kusahihisha mitihani.

Alisema kutokana na mitihani hiyo kusahihishwa kwa kipindi kifupi, wana mashaka kama karatasi za watahiniwa wote zilipitiwa na kusahihishwa ipasavyo.

Bw. Nkonya alisema kutokana na shule za sekondari kuongezeka kwa kasi nchini ufanisi katika sekta ya elimu umedorora na kusababisha kiwango cha elimu kushuka.

"Katika kipindi cha miongo takribani mitatu iliyopita Watanzania tumeshuhudia ongezeko la shule nyingi za sekondari.

"Ongezeko hilo limesababisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kushuka kwa asilimia 22 kutoka asilimia 72 mwaka 2009 hadi 50 mwaka 2010," alisema.

Alisema kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu kumetokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wa watahiniwa.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kubadilika badilika kwa mitahala ya masomo bila wizara ya elimu kuwashirikisha wadau wao, migomo ya walimu kuhusu madai yao na uchache wa walimu.

Bw. Nkonya alisema ili kupata undani juu ya suala hilo chama chao kinapendekeza mtihani wa kidato cha nne kurudiwa kusahihishwa kikanda na kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza viwango vya ufaulu katika mitihani mbalimbali.   

Alisema kushuka kwa kiwango cha ufaulu kumekuja kipindi ambacho asilimia ya bajeti inayokwenda katika sekta ya elimu inaongezeka karibu kila mwaka.

Alisisitiza kuwa kuongezeka kwa bajeti katika sekta ya elimu bila kubadili mfumo wa usimamizi wake kamwe hakutaleta mafanikio.

Juhudi za gazeti hili kumpata Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani, Dkt. Joyce Ndalichako kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda.

3 comments:

  1. Nategemea wasomi hutatua matatizo kwa kuangalia chanzo cha matatizo, sikutegemea kuona hawa wanahangaika na matokeo ya matatizo. Leo mtafuta mtihani, wanafunzi watafanya mwingine nao utakuwa na makosa mtafuta tena, kesho mtafuta tena. Jamani hangikeni na chanzo cha matatizo siyo matokeo ya matatizo.
    Chanzo cha matatizo na Raisi wetu aliyendwa katika katika sector zote. Yaani uwezo wake ni mdogo sana. hilo ndo tatizo la kuhangaika nalo. Kazi Tunayo.

    ReplyDelete
  2. Kweli kazi tunayo, mpaka sasa sijamsikia waziri wa elimu akitoa tamko lolote kama vile haya hayamhusu. Rais pia hasemi chochote?

    Nakubaliana kabisa na mtoa hoja. Hawa wanafunzi hawajatendewa haki, kama kweli mitihani imesahihishwa kwa muda mfupi. Maisha yao yamedhulumiwa kwani muda ktk maisha haurudi nyuma. wengi watarudia mitihani. watapoteza mwaka na pesa kibao kwa kosa la serikali.

    Pamoja na kutafuta mzizi wa matatizo ambao ni wa muda mrefu, suluhisho la muda mfupi kwa ajili ya hawa watotot ni nini? Serikali itujibu.

    ReplyDelete
  3. Yakulaumiwa ni serikali kwa kudhoofisha elimu.Kufuta matokeo na kusahihisha upya haitaongeza kiwango cha elimu ya watahiniwa.Ili kuwatendea haki hawa vijana wetu, serikali ikubali gharama ya wote waliofeli warudie darasa na waje wafanye mtihani tena 2011.

    ReplyDelete